Mlandege yapata matumaini Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Mlandege imepata ushindi wa mechi mbili mfululizo baada ya kuifunga Kipanga bao 1-0 katika mchezo uliopita kabla ya kuichapa KMKM mabao 2-0.
BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM, Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri Ramadhan China, amesema kikosi chake kinaanza kuimarika taratibu, jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri katika michezo ijayo.
Mlandege imepata ushindi wa mechi mbili mfululizo baada ya kuifunga Kipanga bao 1-0 katika mchezo uliopita kabla ya kuichapa KMKM mabao 2-0.
China amesema siri ya ushindi huo ni kuwaheshimu wapinzani wao, kuwanyima nafasi ya kucheza kwa uhuru na kuzuia wasitawale mchezo, akieleza kuwa walitambua uwezo wa wapinzani wao katika kucheza mpira. Amesema ushindi huo wa mfululizo umerejesha motisha na hamasa ndani ya kikosi chake, huku wachezaji wakianza kupata imani zaidi ya kufanya vizuri katika michezo inayofuata.
“Sasa tunaanza kujipata, japo bado hatujawa vizuri kikamilifu. Hata hivyo, naamini muda si mrefu tutarudi katika kiwango chetu kilichozoeleka, kwani msimu huu tulianza ligi kwa kusuasua,” amesema. Ushindi huo umeipandisha Mlandege hadi nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11, huku KMKM ikishuka kutoka nafasi ya saba hadi ya nane ikiwa na pointi 10.