Prime
Miloud ashindwa kujizuia kwa Pacome

YANGA imefanya mauaji jijini Mbeya ilipoivuruga Tanzania Prisons kwa mabao 5-0, kisha fasta ikageuka na kurejea Dar es Salaam usiku wa jana ili kujiandaa na safari ya kwenda Zanzibar kuvaana na Dodoma Jiji, Jumapili, lakini kuna kitu kimetamkwa na kocha wa timu hiyo, Miloud Hamdi ambacho ni kama salamu za mapema kwa wapinzani wanaotarajiwa kukutana na kikosi hicho.
Wababe hao wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 76, baada ya mechi 28, mbele ya Simba yenye alama 75 kwa idadi kama hiyo ya mechi, imesaliwa na mechi tatu, zikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho (FA) kabla ya kufunga msimu na kote inatetea ubingwa.
Yanga itacheza na Dodoma Jiji Jumapili hii visiwani Zanzibar, kisha siku tatu baadae itarejea jijini Dar es Salaam kumalizana na Simba katika Dabi ya Kariakoo kabla ya kurudi tena visiwani kuvaana na Singida Black Stars katika pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho litakalopigwa Juni 29.
Hata hivyo, kuna kitu kimeonyeshwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua katika mechi mbili zilizopita akiwa ndiyo kwanza amerejea kutoka kwenye majeraha ambacho kimemfanya kocha Hamdi kushindwa kujizuia na kufunguka kama wapinzani hawakuwa makini wataumia.
Hamdi alisema Pacome ni fundi hasa na sasa anakwenda kusumbua soka la Tanzania na kukoshwa na namna alivyofunga mabao mawili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya maafande wa Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Dar es Salaam.
Miloud alisema Pacome ana miguu yenye ufundi na akili yenye ubunifu mkubwa kwa sasa akili ya kiungo huyo imerudi kazini na mashabiki wa timu hiyo watafurahia uwepo wake katika timu hiyo inyosaka taji la 31 kwa jumla la Ligi Kuu na la nne mfululizo kwa msimu huu kama italibeba.
"Pacome ni mmoja ya wachezaji Bora ambao tuko nao kwenye kikosi chetu, ukiangalia miguu yake ina sanaa ya mpira na akili yenye utulivu mkubwa," alisema Hamdi na kuongeza;
"Kama unavyoona akili yake imetulia na amerudi kwenye ubora wake, bahati mbaya Ligi inaelekea mwisho lakini namwona ni mchezaji bora ambaye Watanzania wamebahatika kumuona akicheza hapa.
Tuna timu nzuri ambayo wenzake wanajua anataka nini na wafanye kipi kushirikiana kutengenezea ushindi Yanga. Kila mchezaji anaonyesha ana hamu ya kufanya kitu kuisadia timu, tunataka kumaliza Ligi kwa kishindo kikubwa lakini kitu muhimu ni kitumiza malengo yetu."
Msimu huu Pacome amefunga mabao 11 akitoa asisti 9 na kufanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 20 ndani ya mechi 24 za ligi alizocheza akitumia dakika 1,464 na kuiacha Yanga ikiwa kileleni ikisaka taji la nne mfululizo la michuano hiyo na la Kombe la FA ikitinga fainali dhidi ya Singida Black Stars.