Mgunda: Sasa Mjipange

Muktasari:
- Mechi mbili zilizopita dhidi ya Mbeya City iliyomaliza kwa Simba kushinda mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji waliyoshinda bao 1-0 hazikuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo ambao waliona timu yao haikuwa katika kiwango bora.
UNAAMBIWA Simba hivi sasa ni full mziki wapinzani wajipange.
Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amesema kurejea kwa wachezaji hao kikosini kutaongeza nguvu kubwa ya mapambano katika mechi zijazo.
Mechi mbili zilizopita dhidi ya Mbeya City iliyomaliza kwa Simba kushinda mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji waliyoshinda bao 1-0 hazikuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo ambao waliona timu yao haikuwa katika kiwango bora.
Safu ya ulinzi ya Simba hasa beki ya kati ndiyo ilikiwa ikiwachanganya zaidi mashabiki kwani iliruhusu mashambulizi mengi langoni kwao.
Tangu kuumia kwa Henock Inonga Desemba 30 mwaka jana, kwenye mchezo dhidi ya Prisons,kocha wa Simba, Robertino Oliveira alikuwa akiwapanga Joash Onyango na Mohammed Quattara au Kennedy Juma na Quattara lakini hata hivyo bado zilionekana kutoelewana hasa timu yao inaposhambuliwa.
Lakini kurejea mazoezi leo kwa Inonga kutawapa ahueni mashabiki wa Simba wanapoelekea kuikabili Coastal Union Jumamosi
Inonga, Moses Phiri na Peter Banda wamerejea kikosini baada ya kuwa nje ya uwanja tangu Desemba mwaka jana, kutokana na kuwa majeruhi.
Phiri aliumia misuli ya miguu katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Desemba 21 kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Inonga alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Prisons wakati Banda alikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu Novemba 9 mwaka jana baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars.
Phiri mwenye mabao 10, alikosa michezo minne ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, Prisons, Mbeya City na Dodoma Jiji pamoja na ile ya kirafiki katika kambi ya wiki moja waliyoweka Dubai hivi karibuni wakati Inonga alikosa michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Dodoma Jiji.
Wachezaji hao leo Jumatano Januari 25 wamefanya mazoezi vizuri kwenye Uwanja wa MO Simba Arena Bunju huku wakionekana kuwa fiti.
Mgunda alisema kurejea kwa wachezaji hao waliokuwa majeruhi inatia moyo na inaleta faraja.
"Wachezaji wanaporudi kikosini kutoka kwenye majeruhi ni jambo jema kwani yale malengo tuliyojiwekea tunakwenda kuhakikisha yanatimia kwa sababu kuna nguvu wataongeza, " alisema Mgunda na kuongeza.
" Kama ulivyoona Inonga na Banda wamefanya mazoezi yote na timu mwanzo mwisho hivyo sasa namba imeongezeka, Phiri yeye amefanya kidogo na kutoka nje kuendelea na mazoezi mengine chini ya mtaalam wa mazoezi kulingana na majeraha yake.
Pia Mgunda alisema licha ya wengi kuilamu safu ya ulinzi kuwa na makosa sana katika mechi za hivi karibuni kutokana na kutokuwepo Inonga, lakini wanatakiwa kujua watu hawafanani
"Mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa na wenye mapungufu, ili timu nyingine ishinde lazima mwingine akosee hivyo naamini tu ni mapungufu yaliyojitokeza kwenye safu ya ulinzi katika michezo iliyopita lakini sasa tupo fiti.
"Siku zote watu hawalingani na hata katika mpira ipo hivyo, wote hawawezi kulingana uwezo.
" Kila mtu ana uwezo wake na watu wanapocheza pamoja muda mrefu sehemu moja wanakuwa wamezoeana na mwingine anapokuja na kuchukua nafasi hawawezi kuwa sawa kwa muda mfupi kwani hata hao waanaocheza kila siku kuna wakati wanafanya makosa, " alisema Mgunda.