Mgeusa Katibu Mkuu mpya TFF
Muktasari:
- Mgeusa ameteuliwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika jijini Dar es Salaam, akichukua nafasi iliyokuwa ikikaimiwa na Oscar Mirambo, tangu Oktoba 1, 2025, akimrithi Wilfred Kidao.
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Rais wake, Wallace Karia, imefanya mabadiliko mbalimbali ya uongozi, baada ya kumteua Evans Mgeusa kuwa Katibu Mkuu mpya wa shirikisho hilo kuanzia leo Septemba 28, 2026.
Mgeusa ameteuliwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika jijini Dar es Salaam, akichukua nafasi iliyokuwa ikikaimiwa na Oscar Mirambo, tangu Oktoba 1, 2025, akimrithi Wilfred Kidao.
Kidao aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, alimaliza mkataba wake Septemba 30, 2025, kisha nafasi hiyo ikakaimiwa na Mirambo ambaye hata hivyo kupitia kikao cha leo kilichofanyika jijini Dar es Salaam kimemteua Mgeusa kurithi mikoba hiyo.
Kabla ya uteuzi huo, Mgeusa alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA), huku pia akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF), nafasi aliyoteuliwa na Rais, Wallace Karia.
Kwa upande wa Mirambo aliyeondolewa katika nyadhifa hiyo, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu, huku Mustapha Yusuph akiteuliwa Mkurugenzi mpya wa Fedha wa shirikisho hilo kuanzia leo Septemba 28, 2026.
Mustapha ameteuliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Fedha wa TFF, akichukua nafasi iliyoachwa na Cornel Barnabas, aliyetangazwa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), tangu Februari 28, 2026.
Katika mabadiliko hayo, Kurugenzi ya Sheria, Habari na Masoko imegawanywa kuwa tatu tofauti, huku waliopewa jukumu la kuongoza ni Hassan Njama, anayekuwa Mkurugenzi wa Biashara na Masoko na Boniface Wambura anayekuwa Mkurugenzi wa Sheria.
Kwa upande wa Clifford Ndimbo anakuwa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, akiendelea na majukumu yake kama kawaida ya kushika nafasi hiyo muhimu, kwa lengo la kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu taasisi.