Mexime atajwa kuchukua mikoba ya Ndayiragije TRA
Muktasari:
- Uamuzi huo wa TRA United kuachana na Ndayiragije umekuja kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
TRA United imeachana na Kocha wake Mkuu, Etienne Ndayiragije, uamuzi uliotangazwa jana, Jumatatu, Septemba 7, 2026 saa siota usiku.
Uamuzi huo wa TRA United kuachana na Ndayiragije umekuja kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
"Uongozi wa TRA United Sports Club unachukua fursa hii kumshukuru kwa dhati Kocha Ndayiragije kwa mchango wake mkubwa, weledi, na huduma ya kipekee aliyoitoa kwa timu katika kipindi chote alichokuwa sehemu ya klabu.
"Tunampongeza na kumtakia kila la kheri na mafanikio mema katika hatua inayofuata ya maisha na taaluma yake ya ukocha. Klabu itaendelea kuwasiliana na wanachama, mashabiki, na wadau wake kuhusu hatua zaidi inazohusiana na uongozi wa benchi la ufundi la timu," imesema taarifa ya TRA United.
Katika mechi tano za Ligi Kuu msimu huu ambazo Ndayiragije ameiongoza TRA United, timu hiyo haijashinda hata moja, ikitoka sare tatu na kupoteza mbili.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kuwa Kocha atakayerithi mikoba ya Ndayiragije ni Mecky Mexime.