Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpole: Sijutii ofa za Simba, Yanga

EPL Pict

Muktasari:

  • Wakati fulani jina la Mpole lilikuwa likitajwa sana katika mijadala ya usajili, hasa baada ya kuonyesha uwezo wa kufunga mabao na kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu msimu wa 2021/22 akiweka kambani mabao 17.

KATIKA soka kuna wakati mchezaji anang’ara na kuwa gumzo kutokana na kiwango chake, lakini kadiri muda unavyokwenda, kiwango kinaweza kubadilika na kumweka katika mazingira tofauti na yale aliyokuwa nayo awali.

Hata hivyo, kwa mshambuliaji wa Tanzania, George Mpole, kupanda na kushuka kwa kiwango si jambo linalopaswa kumfanya mchezaji apoteze uelekeo wa maisha yake.

Mpole, ambaye amewahi kuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wakivutia macho ya mashabiki wa soka nchini, anasema hajutii maamuzi aliyofanya katika safari yake ya soka, ikiwamo ofa alizowahi kupata kutoka kwa vigogo wa soka la Tanzania, Simba na Yanga.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mpole amefunguka kuhusu maisha yake nje ya uwanja, shughuli za kilimo anazozifanya anapokuwa mapumzikoni, ushindani wa Ligi Kuu Bara, nafasi ya washambuliaji wazawa na namna jina lake linavyomsaidia hata katika shughuli nyingine za maisha.


MPO 01

HAJUTII OFA ZA SIMBA, YANGA

Wakati fulani jina la Mpole lilikuwa likitajwa sana katika mijadala ya usajili, hasa baada ya kuonyesha uwezo wa kufunga mabao na kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu msimu wa 2021/22 akiweka kambani mabao 17.

Simba na Yanga ni miongoni mwa klabu zilizowahi kuhusishwa na ofa za kumhitaji mshambuliaji huyo, lakini Mpole anasema hana majuto kuhusu maamuzi aliyofanya katika kipindi hicho.

Anasisitiza katika maisha ya soka, kila mchezaji hupitia mazingira yake na kufanya maamuzi kulingana na hali inayomzunguka kwa wakati husika.

“Kwa kweli sijutii ofa hata moja. Wakati ule yalikuwa ni mambo ya wakati huo,”   anasema Mpole.


MPO 02

KUHUSU KIWANGO CHAKE

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tanzania Prisons anasema kiwango cha mchezaji kinaweza kupanda au kushuka kulingana na mazingira tofauti, hivyo si sahihi kupima mafanikio yake kwa kuangalia kipindi kimoja au msimu mmoja.

Anasisitiza jambo la msingi ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia malengo na kutambua kuwa soka ni kazi ambayo kupitia hiyo wachezaji wengi wanategemewa na familia zao.

“Siangalii sana grafu ya kiwango changu kwa sababu inaweza kupanda na kushuka. Kuna wakati utakuwa juu sana na wakati mwingine utakuwa katikati au chini.

“Kikubwa ni kupambana na kuzingatia malengo, kwa sababu hii ndiyo kazi yetu na kuna familia zinazotutegemea,” anasema.


MPO 03

MAPUMZIKO NI KILIMO

Tofauti na baadhi ya wachezaji wanaotumia muda wao wa mapumziko kujipumzisha tu, Mpole anasema anaporudi nyumbani kwao Mbeya, hupenda kuwa pamoja na familia na kujihusisha na shughuli za kilimo.

Anasema kilimo ni sehemu ya maisha ya watu wa eneo analotoka, hivyo hata akiwa mchezaji wa soka, bado anaona umuhimu wa kuendelea na shughuli hiyo anapopata nafasi.

“Kwetu sisi ni watu wa kilimo. Ukiwa nyumbani na umepumzika, unajihusisha na kilimo na ufugaji. Mimi nashika jembe, napanda, napalilia na kuvuna,” anasema.

Mpole anafafanua maisha ya mchezaji yanahitaji kutambua wakati wa kufanya kila jambo. Anapokuwa mazoezini au uwanjani, akili yake huwa kwenye soka, lakini anapokuwa nyumbani, anaelekeza nguvu zake katika shughuli nyingine.


MPO 04

UMAARUFU UMEMFUNGULIA MILANGO

Mpole anakiri  kutokana na soka limemsaidia katika shughuli nyingine za maisha, hasa linapokuja suala la kupata fursa zinazohusu kilimo.

Anasema wakati mwingine watu wanapomtambua kutokana na jina lake, wanaweza kumpa nafasi au masharti yanayomrahisishia kufanya shughuli zake.

Anatoa mfano wa kupata shamba la kulima kwa gharama nafuu kuliko ambavyo angeweza kulipata katika mazingira mengine.

“Jina limenisaidia sana. Kwa mfano, mtu anaweza kunipa shamba nilime bure au akanikodishia kwa bei nafuu. Kuna vitu ambavyo vimenisaidia kutokana na jina nililojijengea,” anasema.

Hata hivyo, Mpole anasema watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti kuhusu mtu kutokana na jina lake hasa wanaosema ni jeuri, lakini si kila wanachokifikiria ndicho kinachoakisi maisha yake halisi.

Anasisitiza wanaomfahamu kwa undani, hasa familia yake, ndio wanaoweza kuelewa zaidi tabia na maisha yake ya kila siku.


MPO 05

WAZAWA WANAWEZA

Akizungumzia ushindani kati ya washambuliaji wazawa na wageni, Mpole anaamini wachezaji wa Tanzania bado wana uwezo wa kufanya vizuri, licha ya kuwepo kwa mitazamo kwamba washambuliaji wa ndani hawana makali.

Anasema wakati mwingine mazingira ya ushindani na nafasi anazopewa mchezaji vinaweza kuathiri namna anavyoonekana, hivyo ni muhimu kuangalia takwimu kwa kuzingatia muda aliocheza na nafasi alizopata.

Kwa mfano, anasema mchezaji aliyefunga mabao 10 katika mechi 30 alizocheza dakika zote 90 anaweza kuwa katika mazingira tofauti na yule aliyefunga idadi hiyo hiyo huku akicheza dakika chache katika baadhi ya mechi.

Naamini wanashindana. Ukiangalia wachezaji wazawa, unaweza kukuta mmoja amefunga mabao nane, mwingine tisa na mwingine kumi. Huo ni ushindani mzuri. Ingekuwa hawafikii hata mabao mawili au matano, hapo ungeweza kusema kuna changamoto kubwa,  anasema.

Kwa Mpole, tathmini ya mshambuliaji haipaswi kutegemea idadi ya mechi tu, bali pia dakika alizocheza na nafasi alizopata za kuonyesha uwezo wake.