Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbelgiji Simba afunguka mazito

Muktasari:

  • Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ameanza kuwalisha mbinu vijana wake, akionekana wazi mipango yake ni kuwa na ukuta wa chuma utakaowanyima mabao washambuliaji wenye uchu kama Donald Ngoma, Amissi Tambwe na wengine waliopo timu pinzani.

WAPINZANI wa Simba katika Ligi Kuu Bara, iwe Yanga, Azam na wengine someni hapa; Na kama mtaamua kupuuza basi jiandaeni tu kuumia.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ameanza kuwalisha mbinu vijana wake, akionekana wazi mipango yake ni kuwa na ukuta wa chuma utakaowanyima mabao washambuliaji wenye uchu kama Donald Ngoma, Amissi Tambwe na wengine waliopo timu pinzani.

Aussems mwenye mkataba wa mwaka mmoja, amefanya mambo makuu mawili katika kikosi chake kilichojichimbia kambini mjini hapa, mambo hayo ni kutaka timu icheze ikiwa na mabeki wanne, lakini pia timu yake kushinda kwa mabao mengi.

Akizungumza na Mwanaspoti lililojichimbia Uturuki kufuatilia kambi hiyo ya vijana wa Msimbazi, alisema hatajali awali timu hiyo ilikiwa ikitumia mfumo upi kwa sababu anajua anachokifanya ndani ya kikosi alichonacho sasa kambini hapa.

“Kwa vyovyote itakavyokuwa mfumo wa aina yoyote, ila nyuma nataka kuwa na mabeki wanne yaani inze nne, iwe 4-3-3, 4-4-2, 4-5 -1 na nyingine lakini iwe hivyo,” alisema Aussems.

Alisema anataka mpira uchezwe kuanzia nyuma na si wa kubutua, anataka pasi ndogo na ndefu lakini zenye malengo na zinazofika, huku wakihakikisha lango lao linakuwa salama dhidi ya washambuliaji wasumbufu.

“Kingine ni kuhakikisha timu inafunga mabao zaidi ya moja. Sitaki tukicheza mechi halafu tunashinda kwa idadi ndogo ya mabao,” alisema Aussems.

Aussems alidai ameona wachezaji alionao wana vipaji na kuwa watafundishika hivyo hategemei kwamba watamwangusha.

Awali Simba ilikuwa ikitumia mfumo wa mabeki watatu nyuma uliotambulishwa kwa mara ya kwanza na kocha Mrundi Masoud Djuma, ambaye ni Msaidizi wa sasa wa Mbelgiji huyo aliyechukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre.

MAZOEZI YAKE SASA

Alianza na programu ya fitnesi kuona wachezaji wanakuwa vizuri na sasa ni fiziki kidogo mbinu (taktiki) na ufundi (tekniki).

“Ili upate timu nzuri ni lazima uwe na wachezaj wenye nguvu wanaoweza kufanya lolote katika mapambano na baada ya hapo mambo mengine yatafuata,” alisema Aussems.

Katika mazoezi ya kucheza amekuwa akitumia sehemu ndogo ya uwanja umbali wa mita 30 kutoka langoni na upana huo na kutaka timu zicheze pasi moja mpaka tatu.

Timu moja inaweza kuwa na wachezaji sita mpaka saba.

Simba inaendelea na mazoezi yake katika uwanja wa hoteli ya The Green Park ambao, watautumia kesho kuvaana na Moulaoudia Oudje ya Morocco, mechi ambayo awali ilielezwa ungechezwa jana kabla ya kubadilishwa.

Mkizubaa mtafungwa sana kwa vichwa

Kocha Patrick Aussems alitumia kipindi kizima cha muda wa masaa mawili kufundisha mipira ya kichwa tu na katika hilo, beki Sergio Wawa alikuwa kinara.

Tukio hilo lilifanyika katika mazoezi ya juzi Jumapili jioni. Walianza kwa kufanya mazoezi ya kupasha moto misuli ndipo wakahamia huko.

Ambapo Kocha Ausemms aligawa vikosi vinne na akatengeneza uwanja wenye ukubwa wa mita 30 na kutaka kila timu isimame kwenye pembe moja.

Baada ya hapo timu mbili zinakuwa zinarusha mipira na mbili zinapiga vichwa kufunga golini kwa staili ya zigizaga huku wakibadilishana.

Katika zoezi hilo ndipo beki wa kati Muivory Coast akaibuka kinara kutokana na uwezo wake wa kufunga mipira ya kichwa.

Akitolea ufafanuzi Aussems alisema, huo ulikuwa ni mpango wa kuhakikisha wanafanyia kazi yale anayohitaji.

“Nilifanya makusudi ili kuona uwezo wa kila mmoja katika upigaji na wamefanya vizuri,” alisema Aussems.

Kwa upande wa Wawa alisema hiyo ni kawaida tu: “Hata siogopi kupiga mipira ya kichwa, mimi ni beki wa kati natakiwa niwe vizuri katika hilo.”

Salamba katisha hadi kwa Waturuki

KUNA jamaa mmoja ni mtaalamu wa kunyoosha misuli, anaitwa, Can Guler basi bwana anapomwona straika wa Simba, Adam Salamba mazoezini roho yake inasuuzika kabisa.

Jamaa huyo ni Mturuki na kwa kipindi chote amekuwa akifanya kazi na Simba akiwasaidia wachezaji katika mambo mengine na mazoezini pia.

Lakini, alipoulizwa kwa siku zote ulizokaa na Simba ni mchezaji gani anamvutia akasema; “Acha kabisa Salamba ni mkali.”

Na katika kuonyesha anamjua vizuri anataja jina lake vizuri kabisa: “Nimekaa na Simba kwa kipindi kifupi, kwa upande wangu, mchezaji ninayemkubali ni Salamba, napenda anavyocheza yuko vizuri.”

“Ana umbo zuri, anajua kufunga na anajua mpira kwa ujumla ndiyo maana nasema kwangu mimi Salamba ni bora,” alisisitiza Guler.

Aisee Djuma kumbe bado wamo

Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma usijaribu kabisa kumchukulia poa, jamaa kama ataamua kuvaa jezi na kushuka uwanjani, madogo wa chips kuku lazima waumizwe. Jamaa bado wamo sana kwenye soka asikuambie mtu.

Djuma aliyeiongoza Simba tangu msimu uliopita, jana Jumatatu asubuhi, aliamua kuingia ndani uwanjani na kuanza kucheza pamoja na wachezaji huku akionyesha kwamba bado ni mkali katika kusakata kabumbu.

Katika mazoezi hayo ambayo Kocha Mkuu, Patrick Aussems aligawa vikosi vinne na Djuma akachezea kimoja.

Lakini walipokuwa uwanjani unaweza kusema ni miongoni mwa wachezaji hao kwa sababu hakukuwa na tofauti, aligawa pasi za kufika na kukaba.

Staili waliyokuwa wanacheza ni mtoano hata hivyo kikosi chake kilimaliza na cha pili wakivuna pointi saba, huku vinara wakiwa ni kikosi kilichoongozwa na Meddie Kagere ambaye amesajili msimu huu akitokea Gor Mahia ya kule Kenya.

Shilton kaamua kuwaambia mapema

Kocha wa makipa wa Simba, Mohammed Muharami ‘Shilton’ ametamba kuwa kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, hakitaruhusu mabao zaidi ya 10 licha ya kujua ligi ni ndefu na ngumu kwelikweli.

Shilton alisema makipa wake kwa msimu uliopita waliruhusu mabao 13 katika mechi 30, lakini anataka safari hii idadi ishuke hadi iwe chini ya 10 na anayebisha ataona kwa vitendo.

“Umeona msimu uliopita Aishi aliruhusu mabao 13 tu, lakini kwa namna itakavyokuwa msimu huu mabao tutakayofungwa hayatazidi 10,” alisema Shilton ambaye alionekana kujiamini wakati wa kutaoa msimamo huo mbele ya Mwandishi wa Mwanaspoti.

“Mimi ndiye najua kuna makosa mengi nayafanyia kazi na mabadiliko makubwa ambayo nimeyapunguza kwa sehemu kubwa na naendelea kufanyia kazi.”

Hata hivyo, pamoja na Moharami kutamba, hajaweka wazi ni kipa gani atakayemtumia kufanikisha malengo yake hayo na kusisitiza yeyote anaweza kuanza

Mlipili azua hofu Msimbazi

BEKI wa kati, Yusuf Mlipili ameshindwa kumaliza mazoezi ya pamoja na wenzake jana Jumatatu kutokana na maumivu.

Mlipili alifika mazoezini na kuanza kufanya pamoja na wenzake lakini muda ulipozidi kwenda hali ikawa mbaya.

Amesema, tatizo lilikuwa ni kuchafuka kwa tumbo tangu jana (juzi) usiku.

Hata hivyo anaendelea vizuri na anaamini ataendelea na mazoezi.

“Tumbo tu lilisumbua kidogo lakini sasa naendelea vizuri, ‘freshi’,” alisema Mlipili.