Mayele afunga, KMKM ikilala nyumbani 3-0
Muktasari:
- Mechi hiyo ya hatua ya kwanza, ilishuhudiwa winga Hamdou Elhouni akianza kuifungia Al Ahli Tripoli dakika ya 20, baada ya kipa wa timu hiyo, Ayman Al-Tihar kupiga mpira mrefu na kumfikia mfungaji.
FISTON Mayele amefunga bao moja wakati Al Ahli Tripoli ya Libya ikiondoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMKM katika mechi ya mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa leo Jumamosi Septemba 5, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mechi hiyo ya hatua ya kwanza, ilishuhudiwa winga Hamdou Elhouni akianza kuifungia Al Ahli Tripoli dakika ya 20, baada ya kipa wa timu hiyo, Ayman Al-Tihar kupiga mpira mrefu na kumfikia mfungaji.
Wakati KMKM ikijiuliza, Mayele akafunga bao la pili dakika ya 22, kisha dakika ya 27, beki wa kati Hocine Dehiri akaongeza la tatu kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona.
Licha ya KMKM kuwa nyumbani, lakini ilionekana kama wageni baada ya kupokea mashambulizi mengi hasa kipindi cha kwanza na kujikuta ikienda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 3-0.
Kwa upande wa KMKM, ilitengeneza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza lakini hazikuzaa matunda.
Kipindi cha pili kilikuwa tofauti kidogo baada ya kupungua mashambulizi na kufanya mechi kumalizika kwa wageni Al Ahli Tripoli kuondoka na ushindi huo wa mabao 3-0.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumamosi ijayo Septemba 12, 2026 nchini Libya ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya pili ya mashindano hayo na kwenda kucheza dhidi ya mshindi kati ya Hilal Alsahil ya Sudan na Welwalo Adigrat kutoka Ethiopia.
KMKM ina kazi kubwa ya kufanya mechi ya marudiano ambapo itahitaji kushinda 4-0 ili kufuzu hatua ya pili na kufikia mafanikio yake ya msimu uliopita katika mashindano hayo ilipovuka hatua ya kwanza, lakini ikakwamia hatua ya pili.