Mateso ya Neymar yalitabiriwa tangu mwaka 1778
Muktasari:
Wiki mbili zilizopita, mchezaji anayeitwa Neymar alikuwa tayari kutoa kiasi cha Pauni 17 milioni mfukoni kuipa PSG ya Paris ili arudi zake Barcelona.
AKUMBUKWE mwandishi maarufu wa Kifaransa, François-Marie Arouet aliyejulikana zaidi kwa jina la Voltaire. Umauti ulimkumba katika Jiji la Paris, Ufaransa, Mei 30, 1778. Alizungumza siku moja kuhusu pesa katika kauli iliyompatia umaarufu.
Alisema: “Usidhani pesa ni kila kitu. Au usidhani kila kitu utakachofanya katika maisha basi ni kwa ajili ya pesa.” Unaweza kutabasamu pindi unapofikiri kwamba kauli yake imefanya kazi Paris hapohapo miaka 241 baadaye.
Wiki mbili zilizopita, mchezaji anayeitwa Neymar alikuwa tayari kutoa kiasi cha Pauni 17 milioni mfukoni kuipa PSG ya Paris ili arudi zake Barcelona. Alitaka pesa yake iisaidie Barcelona ili arudi zake Barcelona kucheza soka. Amechoshwa na nini Paris? Mchezaji anayelipwa zaidi PSG. Mchezaji aliyehamia kwa mbwembwe miaka miwili iliyopita akiwa ametua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Charles de Gaulle akiwa na ndege binafsi iliyombeba yeye, mpenzi wake, mtoto wake na wazazi wake.
Anaishi uzunguni mwa Paris. Analelewa kama mtoto mdogo na PSG. Anaoga noti za matajiri wa Kiarabu walioinunua PSG. Amechoshwa na nini zaidi? Hauwezi kujua kilichomchosha mpaka uwe Neymar. Na hauwezi kujua kilichomchosha mpaka umkumbuke Voltaire.
Wakati mwingine pesa ni muhimu sana kama hauna. Ukishakuwa nazo zinapoteza umuhimu. Na kama unazo kisha unaboreka na jambo au unakuwa na afya isiyo njema, basi inaumiza zaidi. Unajiuliza, kwanini pesa hainisaidii? Unarudisha maisha yako katika utu.
Neymar ‘anamiss’ kucheza klabu yenye hadhi na historia nene kama Barcelona. Anajiona mamluki wa pesa. Anajiona hayupo katika sehemu sahihi pale PSG. Mwanzoni alijua angepata pesa zaidi. Alikuwa anatarajia angekuwa mfalme. Inawezekana alipata vitu hivyo, lakini hisia za kuwa Barcelona ni kubwa kuliko pesa.
Ndio maana alikuwa yuko tayari kukatwa mshahara ili arudi Barcelona. Ndio maana alikuwa tayari kutoa pesa zake za mfukoni arudi Barcelona. Ni hisia za ajabu lakini za kweli.
Kuna wachezaji wengi ambao unaweza kusema ni mamluki lakini walipata bahati nzuri kwamba hawakuonja kucheza timu kubwa na zenye historia nene, mashabiki lukuki duniani kote kama Barcelona au Real Madrid.
Naweza kukupa mfano. Kevin de Bruyne, David Silva, Sergio Aguero. Wote hawa ni mamuluki wa pesa kwa kuchezea Manchester City. Timu ambayo haina historia kubwa na nene. Lakini wameweza kuganda Manchester City kwa sababu hawakuwahi kugusa Barcelona wala Real Madrid.
Kama wangeweza kucheza katika timu hizo hapo kabla nadhani baadaye wangetamani kurudi. Lakini wana bahati kwamba walicheza katika timu ambazo hazikuwatamanisha sana kurudi. Neymar amewahi kucheza Barcelona na anajua wazi kwamba ufalme wao ni zaidi ya pesa.
Ni hisia hizi ndizo ambazo zinamtesa. Majuzi nilisoma mahala kwamba Neymar alilia alipogundua uhamisho wake wa kurudi Barcelona katika dirisha lililofungwa Jumatatu usiku pale Ulaya ulikuwa umekwama.
Anajiona mateka wa pesa tu. Kwa ukubwa wa jina lake, licha ya pesa anazolipwa lakini anajiona mateka kucheza katika ligi ya tano kwa ukubwa Ulaya baada ya Hispania, England, Italia na Ujerumani.
Anajiona mateka kwenda kucheza pambano dhidi ya Amiens ugenini katika Uwanja wa La Licorne unaochukua mashabiki 12,097. Wiki inayofuata unakwenda kucheza katika Uwanja wa Raymond Kopa unaotumiwa na Klabu ya Angers ukichukua mashabiki 18,752.
Unatamani kucheza sambamba na Lionel Messi katika pambano kali dhidi ya Atletico Madrid au Valencia, ama Villarreal au lile la El Clasico dhidi ya Real Madrid. Haupati fursa hii. Hii ni zaidi ya pesa. Kama pesa unakuwa umeshapata.
Neymar alianza kupata pesa tangu akiwa na Santos. Alinunua boti la kifahari ‘yacht’ lenye thamani ya Pauni 10 milioni tangu akiwa na Santos. Labda hakuridhika zaidi na zaidi alipoenda Barcelona. Lakini sasa yupo PSG amegundua pesa sio kila kitu. Amerudi kulekule alikosema Voltaire miaka 241 iliyopita.
Nadhani akili yake haitatulia mpaka atakaporudi Hispania katika dirisha la Januari au mwishoni mwa msimu. Ni suala la muda tu. Nadhani huu utakuwa mwaka wake wa mwisho kucheza Paris. Ilishindikana kuhama katika dirisha hili lakini sidhani kama itashindikana mwishoni mwa msimu huu. Bahati nzuri PSG inaujua ukweli huu.
Na kama itashindikana kurudi Barcelona namuona Neymar akitaka hata kwenda Real Madrid. Hakitakuwa kitu kibaya kwake. Bado atakuwa katika timu ambayo ataamini kuwa itamrudisha katika hadhi yake. Bado ni timu ambayo kama akitwaa nayo chochote atahesabika katika mafanikio kuliko kuchukua mataji 10 mfululizo akiwa na PSG pale Ufaransa.
Unapojaribu kufanya kila kitu katika maisha ya kusaka pesa mkumbuke, Voltaire. Utajifunza jambo. Kama ungekuwa unaishi nyumba moja na Neymar katika maeneo ya uzunguni Paris ungejiuliza, maisha yanataka nini zaidi ya pesa? Ukiingia katika moyo wake ndio utajua kuna mambo mengine hayanunuliwi na pesa.