Matatizo makubwa ya Simba yafichuka
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Aden Rage
MWANDISHI WETU SIMBA inahitaji kushinda mechi zake zote nane zilizosalia kwenye mzunguko wa pili kufikisha pointi 55 lakini ikiombea angalau Yanga ikipoteze mechi tatu mfululizo na Azam ikipoteze mbili na kutoa sare. Azam yenye pointi 36 ikishinda mechi zake zote zilizosalia itakomea kwenye pointi 60 wakati Yanga ikifanya hivyo hivyo itamaliza na pointi 66 ambazo Simba haiwezi kuzifikia kwa sasa. Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti kuhusiana na mwenendo wa Simba umebaini mambo makubwa sita ambayo ni kikwazo kwa Simba ndani na nje ya uwanja na kupelekea timu hiyo kuyumba kiasi cha kuhatarisha utetezi wa ubingwa wake. Benchi la ufundi Uchunguzi unaonyesha kwamba kumeibuka mgawanyiko baina ya wachezaji ambapo baadhi hususani wakongwe wanadai hawamuelewi Kocha Mkuu, Patrick Liewig na walipendelea kuendelea kufanya kazi na Mserbia aliyetimuliwa Milovan Cirkovic. Wachezaji hao wanadai kwamba Liewig ameingia na mambo mengi mapya ambayo ni vigumu kuyashika kwa kipindi kifupi ambacho Simba inahitaji kutetea ubingwa wake na kufanya vizuri kimataifa. Wachezaji wanapotolewa uwanjani wanakosa nidhamu. Haruna Moshi 'Boban' alipotolewa mechi ya Libolo alikwenda moja kwa katika vyumba vya kubadilishia nguo. Alipotolewa katika mechi dhidi ya Mtibwa alikwenda katika benchi kisha akaenda chumbani moja kwa moja. Ramadhan Chombo 'Redondo' ambaye alitolewa nje katika kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Kiggi Makasi naye alikwenda moja kwa moja chumbani. Morali iko chini Mmoja wa mabeki mahiri wa Simba amekiri kwamba morali imeshuka ndani ya kikosi hicho ambapo watu wanafanya tu ili mradi siku ziende ndio maana hata ufanisi umepungua tofauti na awali. Mchezaji huyo alidokeza pia kuwa baadhi ya wachezaji hawaaminiani ndani na nje ya uwanja ndio maana hawapendani na wana misimamo tofauti kuhusiana na hali ya mambo inavyokwenda kwao wenyewe na ndani ya benchi la ufundi. Kiongozi mmoja wa Simba anashutumiwa kwa tabia ya kuwagawa wachezaji. Kuna wale anaowapenda na kuwaona muhimu zaidi na mara nyingine anawapa fedha nyingi kuliko wale asiowapenda. Uongozi Uchunguzi unaonyesha kwamba baadhi ya wachezaji wananung'unika kwamba wanapewa ahadi nyingi na uongozi wa juu ambazo zinaishia kuwa siasa tu na hazitekelezeki kwa wakati jambo ambalo linawakatisha tamaa na kuwapunguza nguvu. Habari zinadai kwamba baadhi ya wachezaji wanafanya makusudi ili kuonyesha udhaifu uliopo. Straika Simba inamtegemea straika mmoja tu Felix Sunzu ambaye hata hivyo bado hajawa fiti kutoka kwenye majeruhi. Lakini hata anapocheza, Sunzu hapati tena huduma muhimu kama alizokuwa anapata wakati wa Emmanuel Okwi. Simba ilimuuza Okwi kwa Etoile ya Tunisia na kutumia dola 40,000 na kumnunua kipa Abel Dhaira ambaye sasa anasugua benchi. Endapo Simba ingemnunua straika wa gharama hiyo ni wazi kwamba angewabeba zaidi wakati huu kuliko kumnunua Dhaira ambaye licha ya uhodari wake lakini bado kipa namba moja, Juma Kaseja ameonyesha bado wamo. Mshambuliaji Abdallah Juma ambaye alikuwa mkali akiwa na Ruvu Shooting anaonekana kutoaminiwa na mashabiki wake pamoja na benchi la ufundi kiasi cha kutumia muda mwingi jukwaani. Beki wa Kati Beki ya kati imekuwa tatizo kubwa kwa Simba na imejaribu kombinesheni zaidi ya tano lakini bado hazijaisaidia. Walianza kumchezesha Lino Musombo na Juma Nyosso. Lino Musombo na Shomari Kapombe. Juma Nyosso na Komanbilli Keita, Keita na Shomari Kapombe, Keita na Paschal Ochieng, Nyoso na Kapombe hata Hassan Hatibu na Kapombe lakini bado zimegoma na zinaruhusu magoli jambo ambalo linaonyesha dhahiri kwamba haijawa makini kwenye usajili wa idara hiyo. Kumpoteza Kelvin Yondan kumewaatiri zaidi ukizingatia kuwa beki huyo amekwenda kuitia nguvu zaidi safu ya ulinzi ya watani wao, Yanga ambao wanaongoza ligi huku wakiwa wamefungwa mabao 12 tu. Kazimoto vs Kiemba Ni viungo tegemeo wa Simba lakini morali yao imeshuka na hawako kwenye fomu kama siku za nyuma ndio maana hata mashambulizi ya Simba yamekuwa yakipooza na hayafanyiki ya maana tena. Kupooza kwa wachezaji hao wawili kumeipoozesha na Simba na kufanya tatizo la mastraika lionekane kwa upana zaidi. Kazimoto ameanza kucheza vibaya hata katika timu ya taifa ambapo katika mechi dhidi ya Cameroon alipwaya na kutolewa. Amri Kiemba pia alikuwa amepwaya katika mechi hiyo ya Cameroon. Chipukizi kama Jonas Mkude na Christopher Edward walikuwa majeruhi na pia hawako kwenye fomu. Uti wa mgongo Simba imewasajili beki, Komanbilli Keita, kiungo Mussa Mude lakini bado hawajaonyesha kitu kipya kwenye timu hiyo kiasi cha kuonyesha kwamba pengo la Emmanuel Okwi, marehemu Patrick Mafisango na Kelvin Yondani bado lipo. Wakati Mudde akionekana kucheza taratibu, Salumu Kinje anaonekana kukosa maarifa uwanjani. Katika pambano dhidi ya Libolo aliingia kuchukua nafasi ya Boban lakini hakuwa na mchango wowote uwanjani. Keita ameanza kucheza mara nyingi lakini bado hana utulivu na anakosa kujiamini anapokuwa na mpira kiasi cha mashabiki wa Yanga kumbabaisha kwa kelele nyingi.