Masoud Cabaye atua jeshini
Muktasari:
- Cabaye amefikia uamuzi huo baada ya Polisi Tanzania kuchelewa kukamilisha mazungumzo ya kumsajili, jambo lililomfanya kiungo huyo kugeukia JKT Tanzania ambayo imefanikiwa kupata saini yake kwa msimu ujao.
KIUNGO Masoud Cabaye amejiunga na JKT Tanzania kwa mkataba wa mwaka mmoja, akitua kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Tanzania Prisons.
Cabaye amefikia uamuzi huo baada ya Polisi Tanzania kuchelewa kukamilisha mazungumzo ya kumsajili, jambo lililomfanya kiungo huyo kugeukia JKT Tanzania ambayo imefanikiwa kupata saini yake kwa msimu ujao.
Kiungo huyo mkabaji amekuwa miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu katika eneo la kiungo, akianza safari yake ya soka la ushindani kwenye ngazi ya juu baada ya kupandishwa kikosi cha kwanza cha Azam FC kutoka Azam Academy.
Cabaye alipata nafasi hiyo wakati kikosi hicho kikifundishwa na kocha Zeben Hernandez, kabla ya kutolewa kwa mkopo ili kupata uzoefu zaidi wa kucheza katika kiwango cha juu.
Baada ya kipindi hicho cha mkopo, Cabaye alijiunga na KMC FC ambako alidumu kwa takribani misimu mitatu na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika eneo la kiungo la timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni.
Mwaka 2024, Cabaye aliondoka KMC na kuhamia Mbeya kujiunga na KenGold FC, iliyokuwa imepanda Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza na KenGold haukuwa mwepesi baada ya timu hiyo kushindwa kubaki kwenye ligi na kushuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2024/25.
Baada ya changamoto hiyo, Cabaye alihamia Tanzania Prisons ambako alifanikiwa kurejesha kiwango chake na kuwa sehemu ya kikosi kilichopambana katika Ligi Kuu Bara.
Baada ya kumaliza mkataba wake na Prisons, Cabaye sasa ametua JKT Tanzania, akitarajiwa kutumia uzoefu wake kuimarisha eneo la kiungo la Maafande hao katika msimu mpya.
Taarifa kutoka kwa mtu wake wa karibu zilisema kuwa: “Cabaye ameshajiunga na kikosi hicho na tayari ameanza kujinoa kwa ajili ya kazi atakayokuwa nayo msimu ujao.”