Mashami afichua faili la Tchakei Dodoma Jiji
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Mashami alisema licha ya ubora wa mchezaji huyo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao, lakini anahitaji muda wa ili kuanza kucheza, kwa sababu alichelewa kuungana na wenzake kwenye maandalizi ya msimu.
KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Vincent Mashami amesema licha kukamilisha uhamisho wa kiungo mshambuliaji Marouf Tchakei raia wa Togo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, lakini bado hajawa fiti zaidi kucheza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mashami alisema licha ya ubora wa mchezaji huyo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao, lakini anahitaji muda wa ili kuanza kucheza, kwa sababu alichelewa kuungana na wenzake kwenye maandalizi ya msimu.
“Hakuna asiyejua ubora wa Tchakei lakini hakuwa na maandalizi mazuri ya msimu kwa maana ya Pre Season, ingawa baada ya mapumziko ya mechi zijazo za kimataifa ni matumaini yetu ataanza kucheza na kuisaidia timu,” alisema Mashami.
Mashami alisema kupata mchezaji aina ya Tchakei ni moja ya usajili bora uliofanyika na timu hiyo, kutokana na uwezo wa kufunga na kutengenezea wachezaji wenzake pia nafasi za upatikanaji wa mabao.
Nyota huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza, Julai 1, 2023, akitokea AS Vita Club ya DR Congo na kujiunga na kikosi cha Singida Fountain Gate, kisha dirisha dogo la Januari 2024, alijiunga na Ihefu ambayo kwa sasa ndio Singida Black Stars.
Msimu wa 2023-2024 ambao ni wa kwanza kwa nyota huyo kucheza hapa nchini, alifunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara, akianza kwa kuifungia Singida Fountain Gate mabao matano, kisha alipohamia Ihefu kwa sasa Singida Black Stars aliifungia manne.
Msimu wake wa pili ambao ni wa 2024-2025, alichangia mabao 10 ya Singida Black Stars baada ya kufunga sita na kuasisti manne, huku msimu wa 2025-2026 ukiwa mgumu zaidi kwa nyota huyo kutokana na kumaliza akiwa na bao moja tu la Ligi Kuu.
Bao hilo alilifunga katika sare ya Singida ya 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji kwa penalti ya dakika ya 90+3 baada ya Yassin Mgaza kukitanguliza kikosi hicho kwa penalti pia ya dakika ya 83, mechi iliyopigwa Januari 16, 2026.
Nyota huyo amewahi kucheza pia Gbikinti FC de Bassar na ASKO Kara zote za kwao Togo kisha kujiunga na AS Vita Club ya DR Congo.