Mashabiki Ligi Kuu Zanzibar waonya
Muktasari:
- Onyo hilo limetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Zanzibar kwa kusema mwenendo unaojitokeza viwanjani hauna misingi ya nidhamu, heshima na usalama.
BODI ya Ligi Zanzibar (ZLB) imewaonya mashabiki wanaohudhuria viwanjani kushuhudia michezo ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar kuacha vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwemo matusi, vurugu na kuingia katika maeneo yasiyoruhusiwa uwanjani.
Onyo hilo limetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Zanzibar kwa kusema mwenendo unaojitokeza viwanjani hauna misingi ya nidhamu, heshima na usalama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na bodi hiyo Septemba 28, 2026, mashabiki wanapaswa kuheshimu uamuzi wa waamuzi na kuepuka kuzozana nao kwa kutumia lugha za matusi.
Bodi hiyo ilieleza kuwa, Sura ya 28 ya Kanuni za mashindano mwaka 2026 imeweka hatua dhidi ya vitendo vya kuwatukana au kuwakashifu waamuzi, makamisaa na wasimamizi wa mchezo, pamoja na kuingia uwanjani kwa mashabiki wasioidhinishwa.
“Tunawaelekeza mashabiki kutokaa katika maeneo yaliyotengwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na maafisa wa mchezo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Bodi ilisisitiza kuwa ushabiki wa timu hauwezi kuwa kinga dhidi ya Kanuni za Mashindano, hivyo kila anayehudhuria mchezo anawajibika kwa mwenendo wake.
Hatua zingine zitakazochukuliwa ni pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa, upangaji wa matokeo na kubeti. Bodi imeahidi kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria na kukanusha uvumi kuhusu ukiukaji wa kanuni.
Wakati huo huo, klabu zimekumbushwa umuhimu wa kushirikiana na kamati ya uendeshaji na usimamizi, makamisaa, waamuzi na vyombo vya usalama kuhakikisha mashabiki wanazingatia kanuni.
Bodi hiyo imesema, haitasita kuchukua hatua zilizo ndani ya mamlaka juu ya ukiukaji wa kanuni za mashindano utakapothibitishwa, huku masuala yaliyo chini ya mamlaka ya vyombo vingine yakipelekwa kwenye vyombo husika kwa hatua stahiki.