Manqoba amtumia ujumbe mzito Aziz KI
Muktasari:
- Mngqithi amesema hayo leo Jumatano AGosti 19, 2026 kwenye mkutano na waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja kabla ya Yanga kucheza mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, huku akieleza kuwa bado anaendelea kukifanyia tathmini kikosi chake na kutaka kwanza kuwafikisha wachezaji wote katika kiwango bora cha utimamu wa mwili kabla ya kitu kingine.
KOCHA wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz KI, atalazimika kupigania nafasi yake kikosi cha kwanza, akifichua kuwa katika hatua hii ya msimu hakuna mchezaji anayepaswa kujiona ana uhakika wa kucheza.
Mngqithi amesema hayo leo Jumatano AGosti 19, 2026 kwenye mkutano na waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja kabla ya Yanga kucheza mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, huku akieleza kuwa bado anaendelea kukifanyia tathmini kikosi chake na kutaka kwanza kuwafikisha wachezaji wote katika kiwango bora cha utimamu wa mwili kabla ya kitu kingine.
“Tunataka kuwafanya wote wafikie kiwango kizuri, lakini katika hatua hii ya msimu ni vigumu kufanya mabadiliko makubwa kwa sababu bado tunaangalia ni aina gani ya wachezaji tunaowahitaji na kila mmoja anaweza kutupa nini,” amesema Mngqithi.
Amesema katika michezo ya mwanzo ya msimu, hususani mitano ya kwanza ni vigumu kufanya hitimisho la haraka kuhusu wachezaji watakaokuwa chaguo la kwanza kwa sababu bado anahitaji muda wa kuwaona na kutambua mchango wa kila mmoja ndani ya mfumo wake.
Kauli hiyo inamgusa Aziz KI ambaye amerejea Jangwani akiwa na historia nzuri katika klabu hiyo lakini sasa anakutana na ushindani mpya ndani ya kikosi ambacho Mngqithi anakiona kuwa na ubora na wachezaji wengi wenye uwezo.
Aziz KI amerejea Yanga akitokea Al-Ittihad Tripoli ya Libya, baada ya awali kuichezea Wydad Casablanca ya Morocco. Yanga imemrejesha kiungo huyo baada ya kufanya mazungumzo ya uhamisho na Al-Ittihad huku taarifa zikihusisha dili hilo na kiasi cha Dola 450,000 na mkataba wa miaka miwili.
Kiungo huyo aliyeitumikia Yanga kwa misimu mitatu ambayo ni 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025, alikuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza kabla ya kuuzwa kwenda Wydad ambapo huko hakuwa na muda mrefu, baada ya miezi sita akahamia Al-Ittihad, kisha amerejea Yanga.
Akiwa Yanga, msimu wa 2023-2024 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 21, huku pia msimu huo akiwa Mchezaji Bora wa Ligi (MVP). Kurejea kwake, mashabiki wa Yanga wanatarajia nyota huyo kuonyesha makali yake kama awali.
Akizungumzia nguvu ya kikosi chake, Mngqithi amesema haoni sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu ushindani wa nafasi, akisisitiza kuwa kila mchezaji anapaswa kuonyesha uwezo wake.
“Sidhani kama hii ni timu yenye tatizo la ushindani. Tuna timu imara sana, tuna wachezaji wengi na kila mmoja anatakiwa kupigania nafasi yake, kama ambavyo mchezaji yeyote mzuri anapaswa kufanya,” amesema.
Mngqithi pia amegusia kuwasili kwa wachezaji wapya na namna wanavyoweza kuongeza ushindani ndani ya kikosi, akisisitiza kuwa jambo hilo litakuwa na faida kwa Yanga kwa sababu kila mchezaji atalazimika kufanya kazi zaidi ili kupata nafasi.
“Naamini tuna timu yenye nguvu sana. Kuna wachezaji wengi wenye uwezo na kila mmoja anapaswa kupigania nafasi yake. Natumaini wachezaji wote watakaocheza msimu huu wataweza kupata nafasi kwa wakati wao, lakini kwa sasa ninaamini tuna timu yenye nguvu,” amesema.
Kwa upande wa mashabiki, Mngqithi amesema wana nafasi kubwa katika mafanikio ya Yanga, akiwataka kuendelea kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono timu hiyo huku akiwatambua kama mchezaji wa 12 kutokana na nguvu wanayoipa timu wakati wa michezo.
Mbali na Aziz KI, Yanga wachezaji wapya walioingia dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 15, 2026 ni Juma Issa Abushiri kutoka Fountain Gate, Hussein Juma Mihambo (Mashujaa FC), Abdulnasir Assa 'Gamal' (Mashujaa FC), Mohamed Mussa (Mashujaa FC), Erick Mwijage (KMC FC), Cheikh Ibrahima Toure (Al-Jabalain FC), Albert Kangwanda (Red Arrows FC), Housseine Zakouani (Al-Zulfi SFC), Suleiman Mbarouk (JKU FC), Peter Shalulile (Mamelodi Sundowns FC), Fred Duval Ngoma (Olympique de Safi), Oumar Farouk Comara (Golden Arrows FC) na Seleman Mwalimu 'Gomez' (Wydad Casablanca).