JICHO LA MWEWE: Kina Mayele walivyomfukuza mzee Mpili kimya kimya

JICHO LA MWEWE: Kina Mayele walivyomfukuza mzee Mpili kimya kimya

NCHI ina vituko hii. watu wanakuja wanaondoka. Walikuja kina Pierre Liquid wakaondoka zao. Kuna wakati akaja Mzee Mpili. Huyu alitamba sana kwa sababu alijihusisha na soka, halafu katika klabu mashuhuri nchini, Yanga.

Siku hizi havumi. Vipaza sauti havimfuati sana. Umashuhuri wake umeondoka. Kwanini alikuwa mashuhuri? Alikuwa anajaribu kuzishinda akili za watu wa Yanga wakati timu yao ikiwa mbovu. Halafu akajaribu kuzishinda akili za watu wa Yanga wakati timu yao ikiwa katika mpito.

Yaani wakati ule Yanga wakiwa hawana timu kama waliyonayo sasa hivi, alikuwa anajaribu kuwaaminisha kwamba kuna mambo yanaweza kufanyika nje ya uwanja kama yeye akiiandaa mechi na kisha mtani wao Simba aliyekamilika akafa ndani ya dakika 90.

Ikaja ile mechi ya bao la Zawadi Mauya, Mzee Mpili akachukua ujiko wake. Simba ilishambulia kadri ilivyoweza lakini bao likabakia lilelile. Siku mbili baadaye ikaonekana hata wachezaji wa Simba walikuwa na hofu na Mzee Mpili. Niliwahi kumsikia mahala, Clatous Chama akidai kwamba alikuwa haielewi ile mechi. Akaiita mechi ya Mzee Mpili.

Ujiko wa Mzee Mpili ulianza kuondoka pale Kigoma. Pambano la fainali za ASFC kati ya Simba na Yanga. Nilikuwepo uwanjani na mashabiki wote walikuwa wakimzungumzia Mzee Mpili kabla ya pambano kuanza. Taddeo Lwanga aliwalaza Yanga mapema kwa bao moja la mpira wa kichwa. Yanga waliondoka uwanjani kimya kimya huku wakinong’onezana uongo wa Mzee Mpili na mikwara yake ambayo aliipiga kabla ya mechi.

Msimu huu Yanga wakaamua kutengeneza kikosi imara. Akaja Fiston Mayele, Khalid Aucho, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Djuma Shaban, Djigui Diarra na wengineo. Yanga ikasimama juu ya Simba kwa kuonyesha kiwango kizuri uwanjani. Kuanzia katika ligi hadi katika mechi za ASFC. Huu ndio ulikuwa ni mwisho wa Mzee Mpili na majigambo yake ya kushinda mechi nje ya uwanja.

Yaani huwashawishi watu wa Yanga kwamba mabao ya Mayele yanatokana na kazi ya Mzee Mpili anapokwenda Ikwiriri? Hapana. Yaani uwashawishi watu wa Yanga kwamba pasi nyingi zinazopigwa na kina Bangala na Aucho pale katikati zinatokana na kazi ya Mzee Mpili?

Wazee kama hawa huwa wanapata umaarufu mkubwa pale meli inapokaribia kuzama. Kwa mfano, katika mechi zote tatu dhidi ya Simba msimu huu, Yanga waliingia uwanjani huku wakionekana wana uwezo mkubwa wa kushinda kuliko Simba.

Na mara zote ambazo Mzee Mpili alikuwa anatamba ni pale ambapo Simba walikuwa wanaingia uwanjani katika pambano dhidi ya Yanga huku wakiwa na asilimia kubwa ya kushinda. Basi tu ni vile mechi zao zinakuwa ngumu na ndio maana zilitupa nafasi ya kuona ushindi kwa Yanga katika mechi kama zile za mabao ya Ben Morrison na Mauya.

Lakini tazama pambano ambalo Yanga walicheza na Simba pale Mwanza hivi karibuni. Kila mtu alikuwa anahisi kwamba Yanga walikuwa wanaenda kushinda mechi. Kambi ya Simba ilikuwa imeathiriwa na majeraha na aina fulani ya kuparaganyika. Yanga walionekana kuwa imara kila idara.

Katika hali kama ile Simba walimhitaji zaidi Mzee Mpili wao kuliko Yanga. Hatukumsikia Mzee Mpili akiongea lolote katika hizi mechi. Asingepata umaarufu kwa sababu watu walikuwa wanamuamini zaidi Mayele kuliko yeye. Fei Toto akashinda mechi. Mwisho wa Mzee Mpili umefika. Anaweza kurudi tena kama Yanga akirudi kuwa na timu mbovu hapo siku za usoni. Kwa sasa anaweza kutulia zake Ikwiriri akitafakari namna gani maisha yalimnyookea wakati akiwa katika ubora wake.

Alipata matangazo ya biashara, alifuatwa na waandishi kila kona. Alijiona staa kweli kweli. Ukweli ni kwamba angeombea tu Yanga waendelee kuwa na timu mbovu ilikuwa tukuzwe zaidi na zaidi. kwa hali ilivyo sasa sioni kama atatajwa katika siasa za soka nchini.

Kitu kingine ambacho kingeweza kumpa umaarufu Mzee Mpili, lakini sasa hakitawezekana ni uchaguzi wa Yanga. Inavyoonekana Yanga watapitia katika uchaguzi mwepesi zaidi waliowahi kuufanya katika historia ya klabu yao. Kwa mfano, nafasi ya urais inagombewa na mtu mmoja tu, Injinia Hersi Said. Kwanini? Wanaamini kwamba ameifanyia timu hiyo makubwa kwa kupitia kampuni ya GSM inayoongozwa na miongoni mwa matajiri wakubwa nchini, Ghalib Mohamed. Katika siasa za uchaguzi kama hizi kina Mzee Mpili walikuwa wakitumika zaidi kushawishi makundi kuhusu nani wa kumchagua kuiongoza klabu. Kwa hali ilivyo sasa inaonekana wanachama na mashabiki wamesimama pamoja kumuunga mkono Hersi.

Hata wale ambao hawamuungi mkono Hersi wanapata uvivu wa kuongea hadharani kuhusu dhamira zao. Wanawaogopa wanachama wenzao ambao wanaamini kwamba GSM waliwatoa shimoni wakati ule klabu ilipokabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi.

Mzee Mpili hata akisimama upande wa GSM atajikuta anasimama katika upande wa watu wengi ambao unatarajiwa kushinda. Mzee Mpili hata akiamua kumpinga Hersi anaweza kujikuta anageuka kituko. Labda kama Yanga hii nzuri ingekuwa imeshindwa kumfunga mtani.