Makonda atoa ufanuzi gharama za uwanja wa Arusha
Muktasari:
- Wabunge hao walikuwa wamehoji ongezeko la gharama za ujenzi wa uwanja huo, pamoja na utaratibu wa kumpata mkandarasi mmoja bila kuwepo kwa ushindani katika zabuni.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amejibu hoja za baadhi ya wabunge kuhusu gharama za ujenzi wa Uwanja wa Arusha, akieleza kuwa ongezeko la fedha za mradi huo limetokana na mabadiliko ya mahitaji na viwango vya ujenzi vinavyotakiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Wabunge hao walikuwa wamehoji ongezeko la gharama za ujenzi wa uwanja huo, pamoja na utaratibu wa kumpata mkandarasi mmoja bila kuwepo kwa ushindani katika zabuni.
Akichangia mjadala bungeni jana, Makonda alisema gharama za ujenzi zimeongezeka kutokana na mabadiliko ya mipango ya mradi na matakwa ya CAF kufuatia maandalizi ya pamoja ya Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa mashindano ya soka ya AFCON 2027.
Alisisitiza kuwa Uwanja wa Arusha haupaswi kulinganishwa moja kwa moja na viwanja vingine nchini, akieleza kuwa umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyohitajika kwa mashindano hayo.
Akitoa mfano wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, alisema ulijengwa kati ya mwaka 2005 na 2007, huku Serikali mwaka 2021 ikiwa imeweka makadirio ya Sh187 bilioni, bila kodi, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha.
Alisema mpango huo uliendelea kutekelezwa, lakini baada ya CAF kuweka masharti ya viwango vya viwanja vitakavyotumika katika AFCON 2027, gharama za mradi zilipanda kutoka Sh187 bilioni hadi Sh330.8 bilioni.
“Katika kiwango hiki ipo kodi ya Sh52 bilioni, hivyo ukitoa inabaki kama Sh286 bilioni,” alisema Makonda.
Waziri huyo alikataa ulinganifu wa gharama za ujenzi wa uwanja huo na viwanja vingine, akisisitiza kuwa tathmini inapaswa kuzingatia mabadiliko ya mahitaji na gharama za mradi. Aliwataka Watanzania kutopotoshwa na taarifa zinazotolewa bila kuzingatia maelezo hayo.
“Tunapojenga uwanja wa mpira wa AFCON hatujengi uwanja wa michezo, tunajenga uwanja ambao dunia yenye viwango vyake watakuja kucheza. Kwa hiyo, tulifanya ulinganifu huu ni muhimu sana kuthamini kazi nzuri na heshima iliyofanywa na Serikali, tusipotoshe,” alisema.
Kwa mujibu wa Makonda, hakuna ubadhirifu uliofanyika katika ujenzi wa uwanja huo. Alisema dhamira ya kuujenga haikuanza na maandalizi ya AFCON, bali ilianzia na kuasisiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliongeza kuwa Uwanja wa Arusha umeandaliwa kuruhusu michezo kuendelea hata wakati mvua inaponyesha, tofauti na Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao, kwa mujibu wake, hauwezi kutumika kuchezea soka wakati wa mvua.
Kuhusu hoja ya zabuni kutolewa kwa mzabuni mmoja bila ushindani, Makonda alisema utaratibu huo ulifuatwa kwa sababu Serikali ilitumia takribani miezi sita kukamilisha mchakato wa kumpata mzabuni huyo, akiongeza kuwa kanuni zinaruhusu utaratibu huo.