Barker, Mpanzu watamba tuzo Ligi Kuu Oktoba
Muktasari:
- Mpanzu ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika michezo mitatu ambayo Simba ilicheza mwezi Oktoba na kufunga mabao matatu.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB),leo Novemba 5,2026 imetangaza washindi wa tuzo ya Mchezaji Bora na Kocha Bora wa mwezi Oktoba 2026, huku tuzo hizo zikienda kwa nyota wa Simba, Elie Mpanzu na kocha wake Steve Barker.
Mpanzu ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika michezo mitatu ambayo Simba ilicheza mwezi Oktoba na kufunga mabao matatu.
Kiungo huyo mshambuliaji aliwashinda Iddi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba ambao pia waliingia fainali ya tuzo hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora, Barker amewazidi Florent Ibenge wa Azam FC na Juma Mgunda wa Namungo baada ya kuiongoza Simba kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo.
Ushindi huo uliiwezesha Simba kupanda kutoka nafasi ya pili hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Katika tuzo nyingine, Kamati ya Tuzo imetangaza wachezaji watatu wanaowania tuzo ya Bao Bora la mwezi Oktoba ambao ni Hassan Mubiru wa Azam FC, Elie Mpanzu wa Simba na Selemani Bwenzi wa Mashujaa FC.
Mabao ya wachezaji hao yatapigiwa kura na mashabiki ili kumpata mshindi wa tuzo hiyo.
Pia, Jackson Mwendwa ametangazwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja wa mwezi Oktoba kutokana na kufanya vizuri katika usimamizi wa matukio ya mechi pamoja na kushughulikia masuala ya miundombinu ya uwanja.
Katika Ligi ya Championship ya NBC, Ramadhan Kalanje wa KMC ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba, akiwashinda Abdulkarim Segeja wa Kigamboni United na Hamdani Ally wa Transit Camp.
Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba katika ligi hiyo, Awadh Juma wa Mtibwa Sugar ameibuka mshindi baada ya kuwazidi Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC.