Majeruhi waitibulia Kagera Sugar
MZIMU wa majeraha umeendelea kuitesa Kagera Sugar baada ya wachezaji sita wa kikosi hicho kukumbwa na kadhia hiyo, huku mshambuliaji, Kassim Fekha huenda akakosekana msimu huu mzima wa 2026-2027.
Nyota huyo amefanyiwa upasuaji wa goti baada ya kuumia katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Black Stars iliyochezwa Agosti 19, 2026, jambo litakalomwweka nje kwa takribani miezi saba hadi tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Kagera Sugar, Abel Shindika amesema mchezaji huyo aliumia vibaya walipocheza dhidi ya Singida Black Stars, japo tayari amefanyiwa upasuaji na atakuwa nje kwa muda wa miezi saba hadi tisa.
"Ni kipindi kigumu sana kwetu sisi benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe kwa sababu ni mtu muhimu sana kikosini, awali ilionekana ni jeraha dogo tu lakini baada ya vipimo tukagundua ni kubwa na kumfanyia upasuaji huo," amesema Shindika.
Aidha, Shindika amesema mwingine ni kiungo wa kati wa timu hiyo, Freddy Tangalo ambaye kwa sasa atakaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili, baada ya kuvunjika mfupa wa paja katika mechi dhidi ya maafande wa Mashujaa FC, Agosti 27, 2026.
"Wachezaji wengine ni Said Kipao, Abdul Mohamed na Ally Salum wanaosumbuliwa na kifundo cha mguu na baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA watarejea, huku, Deus Malilo akiuguza majeraha ya goti," amesema.
Kwa upande wa meneja wa kikosi hicho, Bernard Samson Sikira, amesema wakati wa kipindi hiki cha mapumziko wanaendelea na kupambana kwa ajili ya kupata vibali vya wachezaji watatu wa kimataifa, ambao wameshindwa kuonekana hadi sasa uwanjani.
Wachezaji hao ni beki wa kati, Boniface Onyango kutokea Kakamega Homeboyz ya kwao Kenya, kiungo mshambuliaji, Emmanuel Mvuyekule aliyetokea Vision FC ya kwao Burundi na mshambuliaji Mkenya Collins Maina aliyetoka Fortune Sacco FC.
Kagera inayofundishwa na Kocha Mkuu, Juma Kaseja imeanza vibaya msimu wa 2026-2027, kwani tangu ipande daraja, imecheza mechi sita za Ligi Kuu Bara na kati ya hizo imetoka sare mbili na kuchapwa nne, ikiwa nafasi ya 15 na pointi mbili.