Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibenge kula sahani moja na Simba, Yanga

IBENGE Pict

Muktasari:

  • Ibenge amesema Azam imeingia msimu huu ikiwa na dhamira ya kuboresha nafasi ya tatu iliyomaliza msimu uliopita huku akisisitiza ushindani wa kweli ndio unaoweza kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa bora na yenye mvuto zaidi.

KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge amefichua hawapo tayari msimu huu wa 2026-2027 kuwa sehemu ya wasindikizaji wa Simba na Yanga kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la CRDB, wamejipanga kula nao sahani moja.

Ibenge amesema Azam imeingia msimu huu ikiwa na dhamira ya kuboresha nafasi ya tatu iliyomaliza msimu uliopita huku akisisitiza ushindani wa kweli ndio unaoweza kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa bora na yenye mvuto zaidi.

Kocha huyo raia wa DR Congo ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia mwenendo wa timu yake katika mechi za mwanzo za msimu na Azam imecheza sita, ikishinda nne dhidi ya Namungo (2-0), Kagera Sugar (2-0), Pamba Jiji (2-1), TRA United (2-1) na kutoka sare mbili dhidi ya Polisi Tanzania (1-1) na Geita Gold (2-2).


SIO MBAYA

Ibenge anasema licha ya Azam kushindwa kushinda mechi zote sita, bado anaona mwanzo wa msimu si mbaya kutokana na mazingira ambayo timu yake imekutana nayo.

“Ukichukua hivyo, tumecheza mechi sita, tumeshinda nne na tumetoka sare mbili. Sio mbaya. Tunataka kufanya zaidi, lakini kwa maandalizi yetu na mazingira ya mechi hizo, tunakubali sare,” anasema Ibenge.

Kocha huyo amedai katika mechi hizo mbili ambazo Azam ilitoka sare, timu yake iliadhibiwa kwa penalti mbili ambazo kwa mtazamo wake hazikustahili kutolewa.

“Tumekubali sare, lakini tulifungwa kwa penalti mbili ambazo nadhani hazikuwa penalti. Ukiziondoa hizo, tungekuwa na ushindi wa mechi zote tano. Lakini mambo yamekuwa hivyo na tunakubali,” anasema na kuongoza;

“Tunataka kushinda kila mchezo, lakini tunafanya tunachoweza. Kwa ujumla, tunaweza kuridhika na mwanzo wa msimu kwa sababu bado tunataka kufanya zaidi,” anasema.


IBENG 04

WAGENI BADO WANAZOEA

Kuhusu wachezaji wapya ikiwemo John Mano, Lupini Dieumerci, Hassan Mubiru na Henri Stanic walioongezwa kwenye kikosi hicho, Ibenge anasema wana uwezo mkubwa lakini bado wanahitaji muda ili kuendana na mfumo wa timu na mazingira ya soka la Tanzania.

Anasema baadhi yao walijiunga na timu wakiwa wamechelewa na hawakuwa katika kiwango kizuri cha utimamu wa mwili, hivyo hawezi kutarajia waonyeshe uwezo wao wote mara moja.

“Wana ubora, ndiyo maana tuliwasajili. Lakini kuna suala la kuzoea. Siyo rahisi mchezaji kuja na kuzoea kila kitu moja kwa moja,” anasema.

Ameongezal, kadiri msimu unavyoendelea, mashabiki wataanza kuona mchango mkubwa zaidi kutoka kwa wachezaji hao.

“Wanaendelea kuimarika. Baadhi yao hawakuwa fiti kimwili kwa sababu walisaini mikataba wakiwa wamechelewa. Hatukuwa katika kiwango sawa, hivyo tunawapa muda kidogo, lakini nina uhakika wataongeza ubora zaidi kwenye timu,” anasema.


IBENG 01

MICHUANO YA CAF

Azam imepata nafasi ya kushiriki tena hatua ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya msimu uliopita kufanya vizuri katika hatua ya makundi.

Kwa Ibenge, hiyo ni hatua nzuri, lakini si mwisho wa safari yao.

“Ni jambo zuri. Msimu uliopita tulicheza vizuri kwenye hatua ya makundi, labda ndio maana tumepata nafasi hii. Lakini lengo letu siyo kucheza tu raundi ya pili,” anasema.

Ameweka wazi Azam inalenga kurudi kwenye hatua ya makundi na safari hii kwenda mbali zaidi kuliko ilivyofanya msimu uliopita.

“Lengo letu ni kufika tena hatua ya makundi na kufanya vizuri zaidi kuliko mwaka jana. Tunataka kufika robo fainali,” anasema.


IBENG 05

FEISAL? IBENGE ATULIZA

Kuhusu taarifa na tetesi zinazomhusisha kiungo Feisal Salum na uwezekano wa kuondoka Azam, Ibenge amesema hilo halimsumbui kwa sababu mchezaji huyo ni wa kiwango kikubwa na ni kawaida kuzungumzwa na klabu mbalimbali.

Amesema jambo kama hilo lilitokea pia msimu uliopita, lakini Feisal alibaki Azam licha ya tetesi nyingi zilizokuwa zikizunguka.

“Ni mchezaji mzuri, kwa hiyo watu lazima wazungumze. Watu wanazungumza kuhusu wachezaji wazuri, hivyo kwangu sio jambo jipya,” anasema.

Ibenge anasema kila mwisho wa msimu kumekuwa na taarifa nyingi kutoka mitandaoni kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo.

“Msimu uliopita ilikuwa hivyo hivyo. Kila mtu aliponiona aliniambia Feisal atasaini timu hii au ile, lakini aliheshimu mkataba wake na akabaki. Msimu huu ni hivyo hivyo. Watu wanazungumza sana kwenye mitandao, lakini bado yupo hapa,” anasema.


IBENG 01

SIMBA, YANGA

Akizungumzia ushindani wa Azam dhidi ya Simba na Yanga, Ibenge anasema timu yake imeamua kupunguza pengo lililokuwepo na kuendelea kuwa tishio kwa timu hizo.

Msimu uliopita Azam ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye ligi ikiwa na pointi 64, lakini kocha huyo anasema haitoshi kwa timu yenye malengo makubwa.

Msimu uliopita Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 75 huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 73.

“Tunataka kuboresha. Hatutaki kucheza kwa sababu tu ni mpira. Sisi ni washindani na unapokuwa mshindani unataka kushinda,” anasema.

Ibenge anasema msimu uliopita kulikuwa na pengo kubwa kati ya Simba na Yanga dhidi ya timu nyingine, lakini Azam ilianza kulipunguza.

“Katika msimu uliopita tuliona pengo lilikuwa kubwa sana kati ya Simba, Yanga na timu nyingine. Tulikuwa mbali, lakini tuliamua kucheza na kupunguza hilo pengo. Mwaka jana tulifanya hivyo na mwaka huu tupo kwenye mtazamo huo huo,” anasema.


IBENG 02

UTAKUWA WASUMBUFU

Ibenge anasema Azam haitaki tena ligi ambayo Simba na Yanga ndio pekee zinazozungumziwa, akitaka timu nyingine nazo ziingie kwenye vita ya ushindani wa juu.

“Hatupaswi kucheza ili kuwaangalia Simba na Yanga. Tunataka pia kuwa wasumbufu. Tunataka kuleta ushindani na kufanya ligi iwe na mvuto zaidi,” anasema.

Anaongeza, kama Azam, Tanzania Prisons, Singida Black Stars na timu nyingine zitaweza kupambana kwa nguvu, ligi itakuwa na ushindani mkubwa zaidi.

“Unapojua kila wakati ni Yanga tu au Simba tu, sio jambo linalofanya ligi iwe ya kuvutia sana. Lakini Azam ikija kufanya usumbufu, Tanzania Prisons ikaja, Singida ikaja, hapo ligi inakuwa na mvuto zaidi na kuwa moja ya ligi bora,” anasema.


LIGI INAPANDA

Ibenge anasema kiwango cha ushindani katika Ligi Kuu Tanzania kinaendelea kuongezeka, lakini amezitaka timu nyingine kubadili mtazamo na kuingia uwanjani kwa dhamira ya kushinda kila mchezo.

Anasema baadhi ya timu hazipaswi kuridhika na kupigania nafasi za katikati ya msimamo, bali zinapaswa kuwa na malengo makubwa.

“Ushindani unaongezeka, lakini ni kama nilivyosema. Timu nyingine lazima ziwe na nia ya kushindana, sio kucheza tu kwa ajili ya kumaliza nafasi ya nne au tano,” anasema.

Anasisitiza soka linapaswa kuonyesha maadili ya ushindani, uaminifu, kuheshimiana na kupambana kwa nguvu zote.

“Lazima tupambane katika kila mchezo. Soka lina maadili mengi mazuri. Kuna kupambana, kutodanganya, uaminifu, urafiki, pia ushindani. Kama hakuna ushindani, hiyo sio soka halisi,” anasema.


VIJANA WA AKADEMI

Ibenge pia amefichua milango ya kikosi cha kwanza cha Azam iko wazi kwa vijana wanaofanya vizuri kwenye akademi na hakuna sababu ya mchezaji mwenye uwezo mkubwa kubaki kwenye umri wake kwa sababu tu hajafikisha kiwango fulani cha umri.

Anasema falsafa yake msimu huu imejikita kwenye vitu viwili: heshima na kufanya vizuri.

“Nimewaambia wachezaji wangu kabla ya msimu kuanza kwamba tunachotaka ni heshima na uwezo wa kufanya vizuri. Heshima kwa kila kitu, kwa mali, kwa mashabiki na kwa wachezaji wenzako. Halafu tunataka kiwango,” anasema.

Ibenge anasema mfumo wa Azam una timu za vijana kuanzia U-15, U-17 na U-20, lakini mchezaji anayefanya vizuri anapaswa kupandishwa bila kujali umri wake.

“Kama unafanya vizuri sana U-15, unatakiwa kwenda U-17. Kama unafanya vizuri zaidi, unatakiwa kwenda U-20. Na kama una uwezo wa kucheza na timu ya wakubwa, kwa nini usicheze?” anahoji.


AMTAJA KIJANA WA MIAKA 16

Ibenge anafichua Azam ina kijana mwenye umri wa miaka 16 anayefanya mazoezi moja kwa moja na kikosi cha kwanza na tayari amevutiwa na kiwango chake.

“Tunaye mmoja wa U-15, sasa ana miaka 16, ambaye anafanya mazoezi na timu ya wakubwa. Siyo U-17 wala U-20, yupo na timu ya kwanza na anafanya vizuri sana,” anasema.

Kocha huyo anasema kikwazo kikubwa kwa kijana huyo ni kanuni za mashindano zinazomzuia kutumika katika baadhi ya michezo ya ligi.

“Ningependa kama kungekuwa na uwezekano wa kumtumia. Kama nikipata nafasi ya kumtumia, mtamuona uwanjani. Ana ubora mkubwa sana,” anasema.

Ibenge anasema kijana huyo ana uwezo wa kucheza dhidi ya wachezaji wenye uzoefu wa timu za taifa, jambo linalomfanya aamini Tanzania inapaswa kuharakisha mchakato wa kuwapa nafasi vijana wenye vipaji.

“Anacheza dhidi ya wachezaji wangu ambao ni wa timu za taifa. Ukimuangalia, ana kiwango kinachokaribia chao. Kwa nini tumsubiri? Kwa nini tupoteze muda wake akicheza U-15 au U-16 wakati anaweza kucheza juu zaidi?” anasema.


ANGALIENI LAMINE YAMAL

Ibenge anatumia mfano wa Lamine Yamal wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania kueleza umuhimu wa kuamini vipaji vya vijana wenye uwezo mkubwa.

Anasema umri haupaswi kuwa kikwazo pale mchezaji anapoonyesha kiwango kinachostahili.

“Angalia mfano wa Lamine Yamal. Kama Lamine Yamal anaweza kucheza Barcelona na timu ya taifa ya Hispania akiwa mdogo, basi huyu kijana anaweza pia kucheza timu ya taifa ya Tanzania. Kwa nini tusimpe nafasi?” anahoji.


IBENG 03

NAMBA TISA

Ibenge pia amezungumzia mabadiliko ya soka la kisasa, hasa nafasi ya mshambuliaji wa kati ambaye kwa sasa anaonekana kushuka ndani zaidi kusaidia kujenga mashambulizi.

Anasema mabadiliko hayo hayamaanishi nafasi ya namba tisa imekufa, bali timu zinabadilisha namna wachezaji wanavyotumika.

“Soka limebadilika. Mara nyingi inategemea namna unavyowapanga wachezaji wako. Wachezaji wanatembea na kubadilishana nafasi,” anasema.

Ametolea mfano Bayern Munich, akisema mshambuliaji anaweza kurudi ndani ya eneo la kiungo na kuanza kujenga mashambulizi badala ya kusubiri mipira kwenye boksi.

“Ukiangalia baadhi ya michezo ya Bayern Munich, unaona mshambuliaji anarudi mpaka kwenye eneo lake kuanza kujenga mchezo. Soka linabadilika na lazima uwe makini na mabadiliko hayo,” anasema.

Ibenge anasema kocha anatakiwa kutumia aina ya wachezaji alionao na kutafuta namna bora ya kupata mabao.

“Kama una mshambuliaji wa aina hiyo, utamtumia hivyo. Kama huna, utabadilisha mfumo na kutengeneza nafasi za kufunga. Kama mshambuliaji hafungi, labda winga atafunga. Muhimu ni kushinda,” anasema.


AZAM YAOTA UBINGWA WA AFRIKA

Akizungumzia kama siku moja timu ya Tanzania inaweza kushinda taji la Afrika, Ibenge anasema hilo linawezekana, akitolea mfano Simba na Yanga ambazo zimewahi kufika hatua za juu katika mashindano ya CAF. Anasema Azam nayo inaamini inaweza kufikia hatua hiyo.

“Ndiyo, inawezekana. Simba na Yanga tayari zimefika nusu fainali, kwa hiyo haziko mbali sana. Tunazitumia kama rejea tunapozungumzia soka la Tanzania, lakini sisi Azam pia tuna dhamira ya kushinda Kombe la Afrika."