Mafunzo inavyojipanga kuikabili Zimamoto ZPL
Muktasari:
- Wapambanaji hao ni mshambuliaji Abdul Hakim Naim aliyekaa nje misimu mitatu akiwa na majeraha, kiungo Kassim Suleiman Mikidadi, Mshambuliaji James Mlange kutokea Fufuni na Salum Said Konde kutokea Chipukizi United.
WAKATI Agosti 30, 2027 Mafunzo ikifungua msimu wa 2026-2027 kwa kucheza mechi ya Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya Zimamoto, timu hiyo imeanza mikwara kwa kushusha wapambanaji wapya.
Wapambanaji hao ni mshambuliaji Abdul Hakim Naim aliyekaa nje misimu mitatu akiwa na majeraha, kiungo Kassim Suleiman Mikidadi, Mshambuliaji James Mlange kutokea Fufuni na Salum Said Konde kutokea Chipukizi United.
Wengine ni mshambuliaji Ikram Katembo kutoka Junguni United, beki Peter Zakaria, mshambuliaji Abdallah Alagwa Ndame na kipa Ali Athuman Khalfan.
Katika wachezaji nane waliotambulishwa na timu hiyo, wanne ni washambuliaji yakiwa ni maboresho makubwa kwa kikosi hicho kwani msimu wa 2025-2026 Mafunzo haikuwa vizuri eneo la ushambuliaji.
“Karibuni sana, wachezaji hawa wanajiunga nasi kwa ajili ya mapambano msimu wa 2026-2027, tupo tayari kuona ukali wao uwanjani na mabao ya ushindi,” ilisema taarifa hiyo katika utambulisho wa wachezaji hao.
Mafunzo ilimaliza msimu wa 2025-2026 ikiwa nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 42, sawa na ilizokuwanazo Muembe Makumbi iliyomaliza nafasi ya 10. Timu hiyo ilifunga mabao 34 ikiwa ni timu ya 11 iliyokuwa na mabao mengi sawa na Chipukizi United, kati ya timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo.