Madadi atoboa Simba ilivyokwepa hila za Yanga kijanja Zanzibar

Muktasari:
Hatimaye Madadi alisusia kuendedelea kuisimamia Simba katika mchezo ambao ulikuwa upigwe usiku wa siku hiyo na kutaka kuondoka hadi pale alipozuiwa kwenye geti la Hoteli ya Bwawani ili arudi.
KUANZIA Ijumaa, Mwanaspoti limekuwa likikuletea makala maalumu za Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi.
Kiongozi huyo anasilimua mikasa aliyokutana nayo wakati akikinoa kikosi cha Simba mwaka 1992.
Mwandishi MOHAMMED KUYUNGA alifanya mazungumzo na Madadi katika ofisi za TFF na kiongozi huyo akafunguka mambo ambayo huko nyuma hayakuwahi kuandikwa.
Baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya wafadhili wa Simba na Madadi, hatimaye kikafanyika kikao kizito kilichoamua hatma ya wachezaji sita wa Simba ambao walitakiwa kufukuzwa kambini.
Wafadhili wa Simba hawakutaka wachezaji hao wacheze mchezo wa fainali wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki kati ya Simba na Yanga uliopigwa Uwanja wa Amaan, Mjini Zanzibar.
Wafadhili wa Simba, walidai wachezaji hao walikuwa wamepewa pesa na mfadhili wa Yanga wakati huo, Abbas Gulamali ili kuihujumu klabu hiyo.
Hatimaye Madadi alisusia kuendedelea kuisimamia Simba katika mchezo ambao ulikuwa upigwe usiku wa siku hiyo na kutaka kuondoka hadi pale alipozuiwa kwenye geti la Hoteli ya Bwawani ili arudi.
Madadi alirudi na kuwekwa kiti moto na bado alibaki na msimamo wake hadi pale Mwenyekiti Juma Salumu alipopewa kura ya veto kuamua jambo hilo.
Nini kiliendelea?
VIGOGO WASALIMU AMRI, MADADI AIBUKA KIDEDEA
Tayari ilishatimu saa 10 Alasiri na mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, kati ya Simba na Yanga ilitakiwa kupigwa saa 1:00 usiku.
Madadi alitoka kwenye kikao hicho na moja kwa moja akaenda kwenye kambi ya Simba iliyokuwa katika Hoteli ya Kilimani.
“Niliwarudisha Twaha Hamidu na Mwameja (Mohammed) kambini nikaanza kuwajenga kisaikolojia upya.
“Niliwaambia kama kuna mchezaji amepewa pesa hizo ni za kwake. Mimi nataka mcheze mpira pesa nyingine zitakuja baadaye.
Niliwaambia sikutaka kumuona kiongozi yeyote au mfadhili kambini kwa sababu wangeleta ahadi za gari na vitu vingine,”anasema Madadi
Madadi anasema hakutaka wachezaji wake wawaze fedha au magari wakiwa kiwanjani kutokana na ahadi za viongozi hao.
Anasema wachezaji wote walirudi na kuwa kitu kimoja na wakamwahidi kuwa watafia uwanjani.
KIVUMBI UWANJANI
Hadi inatimu saa 11:30 Madadi alishamaliza kuwaweka sawa wachezaji wake na saa 12:00 timu ilianza kuelekea uwanjani ikiwa na hali mpya kabisa.
Kingine Madadi anasema hakulipa kipaumbele suala la utendaji kwenye mchezo ule kama ilivyokuwa desturi za timu za Simba na Yanga.
“Binafsi niliweka akili kwenye ufundi zaidi, sikuyapa kipaumbele mambo hayo,” anasema.
Madadi anasema kikosi chake kilicheza katika mfumo wa 5-3-2 kikiwa na Mohammed Mwameja, Kassongo Athuman, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Fikiri Magosso, George Masatu, Ramadhan Lenny/Hamza Maneno, Michael Paul ‘Nylon’/Issa Kihange, Hussein Marsha, Gebo Peter, Damian Kimti na George Lucas ‘Gazza’.
Yanga kilikuwa na Steven Nemes, David Mwakalebela, Kenneth Mkapa, Salum Kabunda ‘Ninja’, Said Mwaibambe ‘Zimbwe’, Issa Athuman, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, Hamis Gaga “Gagarino, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’/Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Said Mwamba ‘Kizota’ na Thomas Kipese/Joseph Lazaro.
Ndani ya uwanja wachezaji walionyeshana ubabe sana na kusababisha mchezo kuwa mgumu.
Simba ilitangulia kupata bao lililofungwa na Hussein Marsha katika dakika ya 54 akiunganisha krosi ya Twaha Hamidu kabla ya Yanga kuchomoa kupitia kwa Kizota katika dakika ya 63.
MZIRAY ATOLEWA NJE, PAKA ATAWALA
Mara kadhaa kulitokea kutoelewana kati ya mwamuzi na benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha Syllersaid Mziray ‘Super Coach’ a.k.a Mwanangu aliyekuwa akisaidiwa na Charles Boniface Mkwasa.
“Nadhani Yanga walishapaniki baada ya Simba kuongoza kwa bao la Marsha. Wakaanza kumrushia mwamuzi maji kitendo kilichosababisha Mzaray kutolewa kwa kadi nyekundu,” anakumbuka Madadi.
Mara baada ya Mziray kutolewa, pale aliibuka kutoka upande wa Yanga na kuzua gumzo kubwa uwanjani hapo.
Mashabiki walilihusisha tukio hilo la paka na imani za kishirikina. Mara ya kwanza paka huyo aliibuka kipindi ambacho Mziray anatolewa lakini mara ya pili aliibuka wakati Kizota alipofunga bao la kusawazisha dhidi ya Simba.
MAJANGA KWA SIMBA, YANGA
Madadi ambaye katika benchi la ufundi hakuwa na msaidizi zaidi ya kocha wa makipa, alipata majanga baada ya mchezaji wake muhimu Hussein Marsha alipopata majeraha.
“Aliumia na kuomba kutoka. Isingewezekana kwa kuwa tulishamaliza wachezaji wa akiba. Nilimtaka endelee kucheza katika sehemu ya duara la katikati ili azugezuge tu.
“Nilijua wachezaji wa Yanga wasingeweza kupita sehemu hiyo. Ni kweli tulifanikiwa.
Kwa upande wa Yanga, beki wake mahiri, Kenneth Mkapa naye alipewa kadi nyekundu dakika ya 31 tu.
Baada ya Mkapa kutolewa Yanga ilimuingiza beki Joseph Lazaro na kumtoa winga, Kipese aliyemwaga chozi kwa kitendo hicho cha kutolewa uwanjani.
ZAMALIZA DAKIKA 120
Baada ya dakika 120 za mchezo huo, timu hizo zikiwa sare ya bao 1-1 na kuamriwa kupigiana penalti tano tano.
Baada ya kwenda sare katika penalti hizo, ndipo Simba ilipoiobuka kidedea baada ya kushinda mikwaju 5-4.
Beki wa kulia wa Yanga, David Mwakalebela aliyeingia kipindi cha pili, ndiye aliyeikosesha timu yake penalti na Simba ikafanikiwa kutwaa ubingwa. Hiyo ilikuwa ni penalti ya nane ambapo Kabunda, Kizota na Sure Boy nao pia walikosa kwa Yanga.
Kwa upande wa Simba, waliokosa ni Noriega, Kassongo na Kimti.
Wafungaji wa penalti za Simba walikuwa Masatu, Maneno, Magosso, Kihange na Gazza, huku za Yanga zikifungwa na Zimbwe, Issa Athumani, Tingisha na Gagarino.
Yanga ilibaki na wachezaji 10 kwa dakika 89 kati ya 120 za mechi hiyo baada ya Kenneth Mkapa kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 31.
MSIKIE MADADI SASA
Kocha Madadi anasema kilichomsadia kufika hapo ni msimamo aliokuwa nao.
“Kama sivyo, Simba ingefungwa kirahisi sana kwa ujanja mdogo wa Gulamali,” anasema.
Pia, Madadi anasema hajawahi kuona shamrashamra za ubingwa kama zile tangu ameanza kazi ya ukocha.
“Zanzibar ilifanya maandalizi mazuri ya mashindano yale sijawahi kuona. Sherehe za ubingwa zilichukua wiki nzima kuanzia Zanzibar hadi Dar es Salaam. Watu walizungumzia mpira tu na kusahau matatizo yao yote,” alihitimisha Madadi.