Mabula: Ofa za Algeria zilinipa presha
Muktasari:
- Mabula ambaye alitambulishwa hivi karibuni kwenye kikosi cha JS Kabylie ya Algeria akitokea Shamakhi FC ya Ligi Kuu Azerbaijan, amefichua kuwa timu hiyo na USM Alger zote zilikuwa zikimtaka, huku ofa nono zilizowekwa mezani zikifanya uamuzi wake kuwa mgumu.
KAMA kuna usajili ambao uliwahi kumpa presha kubwa kiungo Mtanzania, Alphonce Mabula katika kufanya uamuzi, basi unaweza kuwa dirisha hili ambalo anakiri kuwa alijikuta kwenye wakati mgumu kuchagua kati ya ofa mbili nono kutoka Algeria.
Mabula ambaye alitambulishwa hivi karibuni kwenye kikosi cha JS Kabylie ya Algeria akitokea Shamakhi FC ya Ligi Kuu Azerbaijan, amefichua kuwa timu hiyo na USM Alger zote zilikuwa zikimtaka, huku ofa nono zilizowekwa mezani zikifanya uamuzi wake kuwa mgumu.
Hata hivyo, mwisho wa siku JS Kabylie ndiyo iliyofanikiwa kunasa saini yake baada ya kuweka mezani mkataba wenye thamani kubwa pamoja na marupurupu mbalimbali ambayo yaliongeza uzito wa dili hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mabula alisema ofa alizopokea zilikuwa nzuri, lakini ya JS Kabylie ilikuwa na vitu vya ziada.
“Ofa zao zote zilikuwa nzuri, lakini hii ya Algeria ilikuwa nzuri zaidi. Imenifanya mpaka mimi mwenyewe iwe ugumu kuamua wapi niende,” alisema Mabula.
Mabula aliongeza kuwa, amepewa mkataba wa miaka miwili ambapo mshahara wake jumla ni Dola 870,000 (Sh2.3 bilioni), ambapo kwa mwaka mmoja ni dola 435,000 (Sh1.1 bilioni) huku kwa mwezi ikiwa Dola 36,250 (takriban Sh95.8 milioni).
Lakini si mshahara tu, Mabula pia amewekewa mazingira ya kifedha na kiutendaji yanayokwenda sambamba na mkataba huo, ikiwemo makazi ya ghorofa, gari, tiketi za ndege, bima pamoja na bonasi kama atafanya vizuri na kuonyesha kiwango bora.
Mabula ameelezea kuwa wakati JS Kabylie ikimvizia, USM Alger ilikuwa kwenye harakati za kumnasa. Ikumbukwe USM Alger msimu huu inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakati JS Kabylie haipo mashindano ya CAF. Mabula mwenyewe amethibitisha kuwa, klabu hiyo iliweka ofa ya takribani Dola 750,000 kwa miaka miwili (tariban Sh1.9 bilioni), kiasi ambacho nacho kilikuwa kikubwa na kufanya ushindani wa kumsajili uwe mkali.