Mabadiliko Simba hayakwepeki
Mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji ‘MO’.
Muktasari:
- Yanga imekuwa ikiwanyanyasa mtaani na kejeli hizo zinazotokana na Simba kushindwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo, pia ikishindwa kukata tiketi ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa tangu mwaka 2013.
HAINA ubishi wanachama wengi wa klabu ya Simba wanataka mabadiliko juu ya uendeshaji wa klabu yao wakiamini kwamba, hiyo ndio njia sahihi ya kuepuka kebehi za kuitwa wa mchangani na wamatopeni na watani zao, Yanga.
Yanga imekuwa ikiwanyanyasa mtaani na kejeli hizo zinazotokana na Simba kushindwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo, pia ikishindwa kukata tiketi ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa tangu mwaka 2013.
Mkutano mkuu wa wanachama wa Simba uliofanyika Jumapili iliyopita uligubikwa na wimbi la wanachama hao kutaka mabadiliko yatakayoruhusu mfumo wa uendeshaji wa timu yao.
Simba ndio inayoshikilia rekodi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania, imefika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1974 na kucheza fainali za Kombe la CAF mwaka 1993. Hivyo kejeli na manyanyaso ya kuyumba kwao kwa misimu minne imewachoshwa na kuamua kwa kauli moja, mabadiliko.
Pamoja na kwamba wanachama wa Simba wako tayari kwa mabadiliko, ila uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais Evans Aveva, unaonesha kuwa haujawa tayari ndio maana licha ya kauli ya mabadiliko kukubalika bado haijaeleweka itatekelezwa vipi.
Licha ya hali hiyo, lakini hiyo ni hatua moja mbele ya kuifanyia Simba mabadiliko ya uendeshaji ili kuwa katika hali ya ubora zaidi na kuwa ya kiushindani zaidi.
Kazi kwa MO
Wanachama wa Simba katika mabadiliko wanayoyataka wanahitaji tajiri na mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji ‘MO’ akabidhiwe timu hiyo wakiwa na imani kwamba ataleta mabadiliko na kuiwezesha kufanya vizuri.
MO ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL), ameshasema dhamira yake ya kutaka kununua hisa asilimia 51 katika Klabu ya Simba na kuwekeza Shilingi 20 Bilioni.
Mfanyabiashara huyo ambaye amechukua mikoba ya kuiongoza kampuni hiyo kutoka kwa baba yake, Ghullam Dewji alieleza kuwa Simba itafanya biashara na kuwa na bajeti ya kuendesha timu ya Sh. 5 Bilioni kwa mwaka.
Iwapo wazo hilo la MO litafanikiwa ni dhahiri kwamba Simba itakuwa ndio Klabu yenye bajeti kubwa zaidi Tanzania na Afrika Mashariki na kwa hiyo kuondoa tatizo la sasa la bajeti ya kuunga unga ambapo wanashindwa kufanya manunuzi na kusajili wachezaji wenye gharama kubwa.
Simba kwa sasa inaendeshwa na wadhamini wachache iliyonao na michango kutoka kwa baadhi ya wanachama wapya wenye uwezo jambo ambalo linawapa wakati mgumu wa kuendesha timu kwa ufanisi.
Baada ya maamuzi hayo ya wanachama sasa ni wakati muafaka kwa MO kupeleka mezani maombi yake ya kuitaka Simba na kueleza uchanganuo wake wa jinsi ambavyo anataka klabu hiyo iendeshwe.
Baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kuupata mchanganuo huo nayo inatakiwa kukaa na kujadili na kuona kama unafaa na unatekelezeka na kuusahihisha kama kuna upungufu wowote ili suala hilo litekelezwe mara moja bila ya kupoteza muda.
Baada ya hapo pande zote mbili zinapaswa kukutana na kujadiliana ili waweze kufikia muafaka ambao utaleta mabadiliko katika uendeshaji wa Simba na kazi itakayobaki itakuwa ni ya kuwajulisha wanachama na kuubariki.
Migogoro idhibitiwe
Ni muhimu mkubwa kwa uongozi na wanachama wa Simba kuendesha masuala hayo ya mabadiliko kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kwamba hauleti mvutano wala hauzui mgogoro wa aina yoyote ile.
Kama inavyosema kauli mbiu ya klabu hiyo kuwa Umoja ni Nguvu ni muhimu kwa wanachama wa Simba kuwa watulivu katika kipindi cha mpito kuelekea mabadiliko ili umoja wao usitetereke.
Umoja ni muhimu katika kuleta maendeleo na ndicho kitu ambacho MO kimemvuta katika kutaka kuwekeza katika Simba kwa vile ina mashabiki wa kutosha ambao anaamini kwamba watatimiza malengo yake.
Kama MO angekuwa haihitaji wingi wa mashabiki ni dhahiri kwamba kuna klabu kadhaa ambazo angeweza kuzinunua au kuanzisha ya kwake, lakini ameheshimu wingi wa mashabiki wa Simba kwa hiyo wakiendelea na umoja na mshikamano itakuwa jambo la faraja.
Simba izaliwe upya
Kuingia katika mabadiliko ni jambo moja, lakini jambo la muhimu zaidi ni kuleta mafanikio katika Simba jambo ambalo ndilo litakalowavutia na kuwapendeza mamilioni ya washabiki wa Klabu hiyo.
Kwa hiyo mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika yawe na dhamira ya kuijenga upya Simba na kuiondolea utegemezi na kuwa na kikosi imara ambacho mbali na kuuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara itafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na hata kuchukua ubingwa wa Afrika.
Mabadiliko hayakuwa na maana ikiwa Simba itaendelea kuwa legelege na kumaliza Ligi Kuu Bara ikiwa katika nafasi ya tatu au chini zaidi kama ilivyokuwa kabla ya mabadiliko hayo.
Uwanja, Hosteli zijengwe
Moja ya matunda ya kwanza ya mabadiliko katika Simba ni kuiwezesha klabu hiyo kuwa na Uwanja angalau wa kufanyia mazoezi kwa kuanzia kwa timu zao ili kuondokana na mtindo wa sasa wa kukodi viwanja vya mazoezi.
Jambo la pili ni kujenga hosteli ambayo itatumika kuweka kambi kwa timu yao ikiwa katika maandalizi ya msimu mpya au mechi jambo ambalo litapunguza gharama za kukodi hoteli na pia litaongeza utulivu kwa wachezaji.
Pia Simba inaweza kutumia hosteli hiyo kama kitega uchumi pale ambapo timu yao hawaitumii au kama nafasi inatosha kuzikodisha timu zingine zinazohitaji huduma hiyo.
Usajili uwe wa kimataifa
Dili hili kama litafanikiwa, itaiwezesha Simba kuachana na usajili wa wachezaji kwa kuokoteza na badala yake itafanya usajili wa wachezaji kwa uhakika na kimataifa.
Kwa miaka kadhaa Simba imekuwa inapigwa bao na watani wake wa jadi Yanga linapokuja suala la kumuwania mchezaji hodari kwani wapinzani wao huwazidi kete kutokana na mtaji wa fedha.
Muda umefika wa Simba kuachana na kadhia hiyo ambayo imewasumbua muda mrefu pale wanapoanza mazungumzo na mchezaji kwa lengo la kumsajili lakini wenzao Yanga wakawapiku.
Mbali na Simba kufikiria kuuza wachezaji wake nje lakini muhimu katika mabadiliko haya iweke dhamira ya kuuza vipaji vya vijana kwa njia moja zaidi na ya kisasa kwa kuwa na Academy inayoendeshwa kitaalamu.
Academy hiyo itazalisha wachezaji ambao Simba itawavuna kwa kikosi chake cha juu na wengine kuuza kwa timu zingine za ndani na nje na iwapo mikataba itafungwa vizuri wachezaji hao wanaweza kuwa kitega uchumi cha muda mrefu.
Wanachama wapewe hisa
Mabadiliko yatasaidia Simba kuvuna mataji na kutamba katika mchezo wa Soka lakini pamoja na watu mbalimbali mbali na MO ambao watajitokeza kununua hisa utaratibu utengenezwe ili wanachama waliopo hivi sasa wapewe hisa kiasi fulani.
Ni muhimu wanachama waliopo wasichwe solemba bali nao wagaiwe hisa za bure na wale wenye uwezo wa kifedha waongeze idadi ya hisa zao kwa kupewa ruhusa ya kununua hisa zaidi.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020