Lulu Kayage kuzikwa kesho Jumatatu
Muktasari:
- Lulu alifariki dunia baada ya kukabiliwa na changamoto za kiafya, ingawa aina ya maradhi yaliyosababisha kifo chake haijawekwa wazi.
MAZISHI ya bondia maarufu wa kike hapa nchini, Lulu Kayage, yanatarajiwa kufanyika kesho Jumatatu Novemba 30, 2026, katika eneo la Kisemvule, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, kufuatia kufariki dunia Ijumaa ya Novemba 27, 2026.
Msiba wa bondia huyo upo nyumbani kwa dada yake eneo la Kisemvule, karibu na Msikiti Mweupe, ambapo ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa mchezo wa ngumi wamekuwa wakikusanyika kutoa pole na kushiriki katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Lulu alifariki dunia baada ya kukabiliwa na changamoto za kiafya, ingawa aina ya maradhi yaliyosababisha kifo chake haijawekwa wazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, bondia Debora Mwenda, amesema Lulu Kayage atazikwa Kisemvule na mabondia wenzake wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele.
"Kwanza alikuwa mtu wa watu na ni bondia aliyekuwa na upendo, sisi kama mabondia wenzake tumepokea kwa masikitiko makubwa na tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele," amesema Mwenda.
Kwa upande wa Igne Kayange, amesema tasnia ya ngumi za wanawake imepoteza mtu muhimu kwani mchango wake bado unakumbukwa.
"Mungu ampumzishe salama kwenye nyumba yake ya milele, alikuwa mtu muhimu sana kwenye tasnia ya ngumi za wanawake na tunamuombea sana," amesema.
Lulu Kayage alianza safari ya ngumi za kulipwa Juni 16, 2013, kwa mujibu wa rekodi za Boxrec, akianza kwa kumshinda Mariam Abdallah kwa pointi katika pambano lililofanyika Dar es Salaam. Hata hivyo, kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa alikuwa ameanza mazoezi ya mchezo huo akiwa na umri wa miaka 18. Ushindi wake wa kwanza wa kimataifa aliupata mwaka 2013 nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Lulu Kayage alicheza mapambano 27, akishinda nane, kupoteza 15 na sare manne, huku akicheza katika uzito wa Flyweight. Miongoni mwa ushindi wake ni dhidi ya Winnie Mphahlele wa Afrika Kusini mwaka 2015 na Sarjubala Devi wa India mwaka 2022.