Lulu, beki aliyekacha ualimu kulitumikia soka
Muktasari:
- Hata hivyo, staa huyo anakiri kuwa haikuwa kazi nyepesi kufanya uamuzi huo kutokana na jamii ilivyomtafsiri, licha ya kwamba familia yake ilimpa nguvu na sapoti katika safari yake ya matumaini.
MBEYA; “SIJUTII mpira.” Hiyo ni kauli ya nyota wa Ceasiaa Queens, Lulu Kihombo akielezea maisha yake ya mpira baada ya kuhitimu elimu ya ualimu katika Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) na kuamua kuikacha kazi ya ualimu ili kuendeleza kipaji chake.
Hata hivyo, staa huyo anakiri kuwa haikuwa kazi nyepesi kufanya uamuzi huo kutokana na jamii ilivyomtafsiri, licha ya kwamba familia yake ilimpa nguvu na sapoti katika safari yake ya matumaini.
Autaka ukocha
Beki huyo wa kati anasema kwa sasa hajafikiria kustaafu mpira na kama itatokea anahitaji kufikia ndoto yake ya kuwa Kocha kutokana na uhaba anaouona kwa kundi hilo ikilinganishwa na wanaume.
Anasema anaamini kabla ya kutundika daluga, anahitaji kwenda shule kuo-ngeza elimu ya ukocha, akifafanua kuwa malengo yake ni kuona kipaji hicho anakisambaza kwa vijana wa baadaye.
“Bado sijafikiria kustaafu na kama nitafanya hivyo nataka nianze kuongeza elimu ya ukocha ili kipaji hiki nilichonacho kisipotee bure badala yake niwape vijana wengine wanaochipukia,” anasema.
“Hii naiona kama fursa mpya kwakuwa nikiangalia makocha wa kike nchini ni wachache sana, inaweza kuwa platifom mpya kwangu kutimiza ndoto kwangu na kizazi kijacho huko mbeleni.”
Ulipokuwa Mtihani
Ni wazi kuwa baadhi ya wazazi na walezi hufikiria baada ya watoto wao kumaliza elimu haswa Chuo Kikuu ni kupata ajira serikalini na ilikuwa hivyo hivyo kwa Lulu ambaye baadhi hawakuamini uamuzi wake.
Katika mahojiano maalumu, beki huyo anasema baada ya kumaliza elimu ya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), 2019, akaanza kucheza mpira, hali ambayo baadhi ya jamii walimtafsiri tofauti.
Anasema wazazi wake licha ya kumpa sapoti na matumaini, walimshauri kuendelea kuomba kazi serikalini au kujitolea ili kuendeleza taaluma yake, lakini ilikuwa tofauti na alivyoamua.
“Jamii kwanza ilitafsriri tofauti kwa kuwa miaka hiyo baadhi waliona kama sehemu ya uhuni kwamba inakuwaje mwanamke anacheza mpira, ila nashukuru kaka yangu alinipa nguvu na sapoti kuendeleza kipaji.
“Kwa ujumla sijutii kucheza mpira badala ya kuomba ajira serikali, kwanza niliona mfumo mgumu na ninacho kipaji cha mpira nikaamua kucheza soka kwanza kwakuwa vyeti vipo elimu haipotei,” anasema
Mpira dili
Staa huyo tegemeo kikosini anabainisha kuwa mpira umekuwa sehemu ya mafanikio makubwa kwake kutokana na maisha aliyonayo hivi sasa, akikiri kuwa soka ni dili na linalipa iwapo mchezaji atatilia mkazo kama kazi.
Ana-eleza kuwa kupitia mpira amepata koneksheni nyingi ukimtambulisha kwa watu wa makundi mbalimbali, lakini kumfanya kuijua Tanzania kutokana na kutembea maeneo mengi. “Nimepata faida kubwa, kujuana na watu, nimeijua Tanzania kwakuwa nimetembea mikoa yote, mpira pia unalipa hata kama si fedha nyingi lakini si haba kwa kile ninachokipata kuendesha maisha,” anasema.
Anafichua kuwa hata ikitokea akapata kazi serikalini, hatarajii kuacha mpira badala yake atahakikisha anapanga vyema ratiba zake kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa ikiwa ni kufundisha shuleni.
Awatolea uvivu wanawake
Mchezaji huyo ambaye ni msimu wa saba akicheza Ligi Kuu ya Wanawake, anawataka wasomi wa kike kutobweteka kusubiri ajira za serikali badala yake kutumia ujuzi, kipaji kujikwamua kiuchumi.
Anasema wazazi na walezi wanaochukulia mpira kama kitu cha kawaida kuachana na dhana potofu bali kuweka mazingira rafiki na kutoa sapoti kwa wasichana kucheza soka kwani faida ni kubwa.
“Mpira ni ajira tosha, wale wenzangu wana-omaliza elimu hata ya chuo kikuu wasikae kizembe kusubiri ajira za serikali, fursa ni nyingi kwenye mpira wanaweza kujikwamua kiuchumi na kufurahia maisha,” anasema Lulu.
Haziwazii Simba, Yanga
Tofauti ilivyo kwa wachezaji wa soka la wanaume kuzitamani Simba na Yanga, Lulu anasema hana ndoto wala mpango wa kuzichezea timu kongwe za Simba Queens na Yanga Princess.
Anasema kiu yake ni kuendeleza soka popote akieleza kuwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma soka la Wanawake kutokuwa na mvuto, kwa sasa mambo ni mazuri na sapoti ni kubwa.
Anasema kuwa anachopambania ni kuona anakuwa na namba ya uhakika kikosini na mazingira mazuri alipo katika kikosi cha Ceasiaa Queens lakini kwenda na wakati kwa kufikiria kesho yake.
“Sijawaza wala kufikiria kuzitumikia hizo timu labda niende kuziongoza lakini nachoangalia ni maisha yangu ya huko mbeleni, mpira unao muda wake kimsingi ninayo nia na ndoto za kufika mbali,” anasema mchezaji huyo.
“Mpira wa sasa kwa soka la wanawake umebadilika, sapoti ipo na maslahi yapo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ninachofikiria ni kuona namaliza safari yangu kwa kuacha alama kwenye kwa jamii.”
Ushindani
Akiwa mchezaji mwandamizi katika kikosi cha Ceasiaa Queens, Lulu anakiri ugumu wa ligi akieleza kuwa timu zote zinaonesha upinzani, huku akipongeza wenzake na uongozi kwa namna walivyopambana kulinda heshima ya timu.
Anasema misimu mitano wakishiriki Ligi Kuu ya Wanawake si jambo jepesi akielezea tukio la msimu wa 2021/22 waliponusurika kushuka daraja kutokana na vita kali waliyokutana nayo.
“Ligi ni ngumu, kila timu inakuja imejipanga na siwezi kusahau tukio la kuumia goti msimu wa 2021/22 mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Oysterbay na kuwa nje kwa msimu mzima,,” anasema beki huyo.
“Mchezo huo ndio ulikuwa umebeba hatma yetu kubaki au kushuka lakini nashukuru tulishinda na kubaki salama nashukuru wadau walitoa sapoti kubwa kunisaidia hadi kupona hadi sasa niko imara.”
Historia yake
Lulu ni mzaliwa wa mkoani Njombe alikoanzia kucheza soka akiwa bado shule ya msingi akishiriki michuano ya Umitashumta na Umisseta ambayo ilimtambulisha kwenye mchezo huo.
Baadaye alijiunga na timu ya Ruvuma Queens iliyoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake 2019 na kudumu msimu mmoja kisha kuuzwa na kuitwa Ceasiaa Queens ambayo ameendelea kuitumikia na hadi sasa.
Kitaaluma nyota huyo tegemeo kikosini ni mwalimu akipata elimu yake katika Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) mwaka 2019, ambapo aliamua kuendeleza kipaji chake akiamini ndio sehemu ya kupata mafanikio.