Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Leo leo hapatoshi Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Mchezo wa mapema utapigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kuanzia saa 8:00 mchana, ambapo wenyeji Mashujaa watawakaribisha Polisi Tanzania.

LIGI Kuu Bara inarejea leo kwa mechi tatu zitakazopigwa katika mikoa mitatu, huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu katika kuendeleza malengo yake ya msimu wa 2026/27.

Mchezo wa mapema utapigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kuanzia saa 8:00 mchana, ambapo wenyeji Mashujaa watawakaribisha Polisi Tanzania.

Mashujaa itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo la kuendeleza rekodi yake nzuri nyumbani, ambako imeshinda mechi mbili, huku ushindi mmoja ukiupata ugenini.

Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Mashujaa imeshinda tatu na kupoteza tatu, huku ikiingia kwenye mchezo wa saba baada ya kutumia mapumziko ya ligi kufanya maandalizi kwa takriban wiki tatu.

Timu hiyo itahitaji kuwa makini katika safu yake ya ulinzi, kwani katika ushindi wake huo mitatu, imecheza mchezo mmoja pekee bila kuruhusu bao ilipoichapa Coastal Union 1-0 ugenini.

Polisi Tanzania nayo itapaswa kuwa makini na Haroun Lyawatwa na Mishamo Daud, ambao wameifungia Mashujaa mabao mawili na moja mtawalia.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Amani Josiah, alisema mapumziko hayo yamewapa nafasi ya kurekebisha maeneo yaliyokuwa na mapungufu.

“Tumerejea kwenye ligi baada ya mapumziko mafupi kwa vijana, tukarudi kazini kujiandaa. Tumefanya maandalizi ya kutosha na tumeyafanyia kazi maeneo ambayo yalikuwa yanapungua,” alisema Josiah.

Polisi Tanzania, ambayo msimu huu imerejea Ligi Kuu kwa kishindo, imeanza kwa kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mbili.

Rekodi hiyo inafanya mchezo huo kuwa wa kuvutia, kwani timu zote zimewahi kushinda ugenini msimu huu.

Mashujaa itahitaji kumzuia mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Anoury Jabir, ambaye tayari amefunga mabao matatu katika mechi sita.

Kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, alisema wanatambua ubora wa Mashujaa, lakini watajaribu kutumia mapungufu yake kupata ushindi.

“Kucheza dhidi ya Mashujaa ni wazi unakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa kikosi chao. Tutajaribu kutumia makosa yao kutengeneza ushindi,” alisema Makata.


PAMBA, GEITA

Mchezo wa pili utapigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kuanzia saa 10:15 jioni, ambapo wenyeji Pamba Jiji wataikaribisha Geita Gold.

Pamba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na presha wakiwa na rekodi mbaya zaidi baada ya kufungwa mechi tano na sare kati ya sita ilizocheza.

Matokeo hayo yamemuweka katika wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkenya Francis Baraza, huku ushindi ukiwa hitaji kubwa ili kuanza kugeuza mwenendo huo.

“Tumekuwa na changamoto mbalimbali kwenye kikosi chetu na tumeyafanyia kazi. Kuna baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi ambao wamerejea. Tunajua hautakuwa mchezo rahisi, lakini tunapambana tuweze kushinda,” alisema Baraza.

Geita Gold nayo haitakiwi kupuuzwa. Timu hiyo ilianza msimu kwa kasi kabla ya kupoteza mchezo wake wa mwisho ugenini dhidi ya Yanga.

Kocha wa Geita Gold, Zuber Katwila, amesema matokeo mabaya ya Pamba hayawapi nafasi ya kubweteka.

“Tunajua wenzetu hawana matokeo mazuri, lakini hilo halitufanyi tubweteke. Tumefanya maandalizi kuhakikisha tunarudi kwenye njia ya ushindi. Tumejipanga kukutana na mchezo mgumu,” alisema Katwila.


NAMUNGO, TRA UNITED

Mchezo wa mwisho utapigwa Lindi, ambapo wenyeji Namungo wataikaribisha TRA United.

Mchezo huo pia utawakutanisha makocha wanaofahamiana vizuri, Juma Mgunda wa Namungo na Hemed Morocco wa TRA United, ambao waliwahi kufanya kazi pamoja katika timu ya Taifa Stars.

Namungo imecheza mechi saba, ikishinda mbili na kupoteza tano, matokeo ambayo yameifanya timu hiyo kuwa katika hali isiyoridhisha na kulazimika kusaka ushindi.

Kocha Mgunda amesema mapumziko ya wiki tatu yamewapa nafasi ya kujiandaa na kutafuta suluhisho la matokeo hayo.

“Tumekuwa na mfululizo wa matokeo ambayo si mazuri, lakini katika wiki hizi tatu hatujatoka bure. Tunataka kuondoa hali hii haraka. Mechi haitakuwa rahisi,” alisema Mgunda.

TRA United chini ya Morocco imeanza msimu kwa kishindo baada ya kuichapa Pamba Jiji ugenini katika mchezo wake uliopita.

Katika kipindi cha mapumziko, timu hiyo ilifanya maandalizi Zanzibar kwa lengo la kuongeza makali na sasa inataka kuendeleza kasi hiyo Lindi.

Morocco, aliyeliwahi kuifundisha Namungo, alisema anafahamu ubora wa wapinzani wao, akisisitiza kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi.

“Namungo imekuwa ikikosa matokeo mazuri, lakini ni timu nzuri na ina kocha mzuri anayejua ligi ya Tanzania. Hii si mechi rahisi,” alisema Morocco.