Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Luiza Mbutu ni Twanga Pepete, Twanga ni Luiza Mbutu

Muktasari:

Sifa kubwa ya Luiza Mbutu ni ile ya kutokuhama kwenda bendi nyingine kama wafanyavyo wengine. Tangu alipoingia Twanga Pepeta, mwaka 1998 akitokea Magoma Moto Sound, hajawahi kuhama hata mara moja.

Luiza Mbutu amekabidhiwa wadhifa wa kuongoza bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta, baada ya Asha Baraka ‘Iron Lady’ kung’atuka.
Kabla ya kupewa nafasi hiyo, Mbutu alikuwa Katibu wa bendi na amedumu nayo kwa zaidi ya miaka 20. Kwa mujibu wa rekodi ya wanamuziki wa bendi hiyo, yeye ndiye mkongwe zaidi ya wengine waliopo katika bendi hiyo.
Akiwa na furaha tele usoni kwake, Luiza alisema amepokea kwa mikono miwili majukumu alliyokabidhiwa, akaahidi kuongeza mikakati imara na kuhakikisha bendi hiyo inaendelea kufanya vizuri.
Akionesha kujiamini kwa ayasemayo, mwanamama huyo alibainisha wakati wa uongozi wake amepanga kuifanyia bendi yake mageuzi makubwa zaidi akishirikiana na wanamuziki wenzake kuhakikisha wanaibadilisha Twanga Pepeta, kuipeleka kwenye kiwango kingine cha maendeleo.
Mbutu amesema mipango ipo mingi lakini akawaasa wanamuziki wa bendi hiyo kuwa na mshikamano wa pamoja.
Historia inaonesha African Stars ilianzishwa July 01, 1994 katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam. Baadaye wakaunda Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET).

Luiza Mbutu ni nani?
Luiza Mbutu wakati wote awapo jukwaani huonekana mithili ya msichana mdogo, mwenye uso wenye tabasamu lenye furaha muda wote wakati akiimba na kunengua, licha ya haiba pamwe na umbo lake dogo ambalo hulitumia ipasavyo kulipambisha jukwaa akisaidiana na wanenguaji wenzake wa bendi hiyo.
Luiza ameeleza siri ya kutozeeka au kuchuja ni kutotumia vilevi na kufanya mazoezi.
“Kutotumia vilevi ndio mambo yanayonifanya nionekane hivi nilivyo, kingine ni mazoezi. Mimi naimba na kucheza, kwa hiyo kucheza ni sehemu ya mazoezi,” alisisitiza.
Mama huyu alianza kuonekana kwenye Luninga miaka ya 1990, alipokuwa akicheza na kuimba pamoja na mwanamuziki Chemundugwao, wimbo wa “Tulitoka wote Mahenge.”
Wakati huo alijulikana kwa majina ya Luiza Nyoni, lakini baada ya kuolewa na Faiara Mbutu, ambaye pia ni muungurumishaji mwanamuziki, sasa anajulikana kama Luiza Mbutu.
Katika maisha ya ndoa yao, wamefanikiwa kupata mtoto wa kiume kwa jina la Bryain.

Wasifu
Luiza alizaliwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, jijini Dar es Salaam. Alipotimiza umri wa kuanza shule, alipelekwa katika shule ya Msingi ya Mkamba, Kilombero nje kidogo ya Mji wa Morogoro, ambako alisoma tangu darasa la kwanza hadi la tatu.
Baadaye alihamishiwa shule ya msingi ya Mzinga, iliyopo Morogoro Mjini na kusoma darasa la sita na kumaliza darasa la saba katika shule ya msingi ya Mushono, iliyopo Arumeru mkoani Arusha.
Baada ya kumaliza elimu hiyo, alikwenda kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Fikra na mawazo yake yalikuwa ni kufanya kazi ya muziki, Luiza aliamua kwenda kujiunga katika masomo ya muziki yaliyokuwa yakitolewa na Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.
Hapo alisoma hatua ya kwanza hadi ya tatu. Kwa mujibu wa maelezo yake, kipaji chake cha kuimba kilianzia akiwa shule. Alipofika darasa la nne akawa mwimbaji kwenye kwaya ambayo aliendelea na huduma hiyo.
Luiza Mbutu alisema kwa sasa ameacha kuimba kwaya, lakini anaweza kurejea kwenye kwaya kwa kuwa anaipenda sana.
Sifa kubwa ya Luiza Mbutu ni ile ya kutokuhama kwenda bendi nyingine kama wafanyavyo wengine. Tangu alipoingia Twanga Pepeta, mwaka 1998 akitokea Magoma Moto Sound, hajawahi kuhama hata mara moja.
Aidha Luiza alieleza sababu za kutotaka kuhama kwenye bendi hiyo, kwa kuwa anapenda kuishi kwa kujifunza kutokana na baadhi ya wanamuziki ambao wakihama, baada kipindi kifupi hurejea tena katika bendi yao ya Twanga.
Amefafanua mwanamuziki anapohama hupoteza mashabiki, wengine kupotea kabisa katika tasnia ya muziki.
Katika kulelekea onyesho la bendi hiyo African Stars kutimiza miaka 20 ya mtindo wao wa Twanga Pepeta lililofanyikia Oktoba 20, 2018, jijini Dar es Salaam, Luiza alikumbuka mambo kadhaa aliyowahi kuyashuhudia kwenye bendi hiyo.
“Ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo, kwa sababu kuna wenzetu wengi tulikuwa nao, lakini wametangulia mbele za haki. Tungelipenda tunapokwenda kusherehekea miaka 20 ya Twanga, wangelikuwepo ila Mungu kawapenda zaidi, kwa hiyo naomba Mungu awape pumziko la milele, amina” anasema Luiza Mbutu.
Alitamka kuwa tatizo jingine kubwa lililowakumba hadi kufika siku waliyotarajia kwenda kutimiza miaka 20 ya Twanga, ni lile la wanamuziki kuhama na kuifanya bendi iyumbe, lakini anadai huwezi kuzikwepa changamoto hizo kwenye bendi au makundi.
Pamoja na mafanikio aliyoyapata kutokana na bendi hiyo, hakusita kuusifia uongozi wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET)
“Ninaukushukuru sana uongozi African Stars ‘Twanga Pepeta’ chini ya Mkurugenzi Asha Baraka, kwa kuendeleza kuidumisha bendi yao tangu ilipoanzishwa, Twanga Pepeta ambao ni mtindo wa bendi hiyo ndiyo ilitimiza miaka 20, lakini African Stars kama bendi ina muda mrefu zaidi,” alisema Luiza.
Mambo mengine ambayo anayakumbuka walipokuwa wakielekea miaka 20 ya Twanga Pepeta ni kupata fursa ya kutembelea mbalimbali binafsi au na bendi yake.
“Safari hizo zimenifanya nijifunze, pia nimeweza kutembea na kuona vitu vingi, hivyo kupitia hilo kwangu ni kitu kizuri sana,” alisisitiza Luiza.
Pamoja na mengine mengi kwa upande wa vitu vibaya ambavyo ilikuwa ni kushuhudia wanamuziki wanahama, akidai kilikuwa kikimpa mshtuko sana.
“ Nakumbuka marehemu Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ aliondoka Twanga na kwenda TOT, wakati huo tulikuwa tunaandaa albamu ya pili ya ‘Jirani’ akahama, haikuwa vyema japo alitupa funzo,” Luiza ghafla uso wake ulibadika na kuwa wenye huzuni kubwa alipokumbuka jambo jingine kubwa sana kwake la kumpoteza kiongozi wao marehemu Abuu Semhando.
Semhando alikuwa Kiongozi, Babu, Meneja, Katibu wa bendi, aliyekuwa akituunganisha vizuri kati ya wanamuziki na uongozi wa bendi,” aliseme Luiza.
Abuu Semhando alifariki dunia baada ya kupata ajali mbaya ya Pikipiki akitokea kazini usiku jijini Dar es Salaam.
Luiza Mbutu hadi sasa akipanda jukwaani huonekana ni mwenye furaha, mchangamfu akiwaongoza wanenguaji wenzake licha ya umri wake kuwa mkubwa, bado yupo kwenye ‘game’.
Kongole kwako kupitia makala haya, tunakutakia kila la heri katika kuliendeleza gurudumu ulilokabidhiwa.
Mwandishi wa makala hii anapatikiana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0713331200.