Liverpool yatimiza miaka 128
Muktasari:
Liverpool imetwaa jumla ya mataji 49 yanayoifanya iwe miongoni mwa timu zenye mafanikio zaidi nchini Uingereza.
Liverpool,England. Wakati ikielekea kutwaa taji lake la 19 la Ligi Kuu ya England, timu ya Liverpool jana imetimiza jumla ya miaka 128 tangu ilipoanzishwa.
Liverpool ilianzishwa mnamo Juni 3, 1892 na tangu hapo imekuwa ni miongoni mwa timu kubwa na yenye mafanikio zaidi Uingereza na duniani kwa ujumla.
Kati ya mataji hayo 47 ambayo Liverpool imetwaa, 35 ni ya ndani wakati 12 ni yale ya kimataifa.
Mataji 12 ya kimataifa ambayo Liverpool wametaa ni sita (6) ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, matatu (3) ya Kombe la Uefa, taji la Uefa Super Cup mara nne (4) na klabu bingwa ya dunia mara moja.
Kwa mataji ya ndani, Liverpool imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara 18 (18), Kombe la FA mara saba (7) na Kombe la Ligi mara nane (8).
Baada ya kuanzishwa mwaka 1892, mwaka mmoja uliofuata, Liverpool iliingia rasmi katika ligi ya soka England ikichezea mechi zake katika uwanja wa Anfield ambao inautumia hadi leo hii.
Liverpool ambayo ilianzishwa ikitokea ubavuni mwa Everton baada ya kutokea mgogoro baina ya viongozi wake ambao miongoni mwao ni John Houlding aliyeamua kuianzisha na kuipa uwanja wa Anfield ambao alikuwa anaumiliki.
Hilo limefanya Liverpool na Everton kuwa watani wa jadi na timu zenye upinzani mkubwa lakini pia timu nyingine ambayo ni mahasimu wa jadi wa Livepool ni Manchester United.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya uwekezaji wa kampuni ya Marekani ya Fenway Sports Group,LLC (FSG) ambayo pia inamiliki timu ya mchezo wa Baseball ya Boston Red Sox.
Liverpool iko katika nafasi ya saba (7) kwenye kundi la klabu kumi tajiri duniani nyuma ya Barcelona, Real Madrid, Manchester United, Bayern Munich, PSG, Manchester City, Tottenham Hotspur na Juventus
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Deloitte, Liverpool ina mapato ya kiasi cha Euro 604.7 milioni (zaidi ya Sh 1 trilioni)