Ligi Kuu Zanzibar yasimama
LIGI Kuu Zanzibar (ZPL) imesimama kuanzia leo Jumamosi ili kupisha mfungo wa mwezi wa Ramadhani, huku ligi hiyo ikiwa imesaliwa na mechi za raundi tano tu kabla ya kumalizia msimu.
Jana Ijumaa zilipigwa mechi za raundi ya 25, huku KMKM inayoongoza kwa pointi 57 ikivaana na Yosso Boys, Kisiwani dhidi ya Machomane zilizopo kwenye janga la kushuka daraja.
Yosso ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 12, Kisiwani pointi 10 na Machomane ikiwa na alama tisa tu baada ya mechi 24 na kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi ya visiwani humo ni kwamba ligi itarudi tena Mei 13 baada ya kumalizika kwa mfungo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Hashim Salum alisema; “Kwetu mwezi mtukufu ni kitu kikubwa sana na lazima tuheshimu, hivyo ni lazima ligi isimame ili kila mtu afanye ibada hiyo na itaendelea Mei 13 zikiwa zimebaki mechi tano kwa kila timu.”
Kocha mkuu wa Taifa Jang’ombe, Omary Hamis Othman ambaye timu yake inashika nafasi ya nane katika msimamo ikiwa na pointi 39 (kabla ya kucheza jana) alisema kwa kipindi hiki hakutakuwa na programu yoyote kwenye timu yake.
“Tutarejea kufanya mazoezi siku 15 kabla ya mfungo kumalizika.”
Naye Kocha wa KMKM, Ame Msimu alisema; “Tutawapa mapumziko ya wiki mbili wachezaji wazowee mfungo ndipo tutaendelea na programu ya mazoezi, kwani lazima tupambane kwani ligi ni ngumu na hatujajihakikishia nafasi ya kutetea ubingwa.” Baadhi ya wachezaji wamedai kwamba kusimama kucheza kwa muda mrefu kutawatoa kwenye ufiti waliokuwa nao.