Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ELIZABETH JOSEPH; Kiungo alikuzwa Alliance Girls, tegemeo Simba Queens

ELIZA Pict

Muktasari:

  • Miongoni mwa nyota hao ni kiungo mkabaji wa Simba Queens, Elizabeth Joseph, ameonyesha ukuaji mkubwa ndani ya muda mfupi.

KATIKA soka la wanawake Tanzania, kila msimu huibuka vipaji vipya vinavyokuja kwa kasi na kujitengenezea nafasi kwenye timu kubwa.

Miongoni mwa nyota hao ni kiungo mkabaji wa Simba Queens, Elizabeth Joseph, ameonyesha ukuaji mkubwa ndani ya muda mfupi.

Elizabeth alianza kujitengenezea jina akiwa na Alliance Girls, ambako alionyesha uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji.

Nidhamu, utulivu akiwa na mpira na uwezo wa kuusoma mchezo, vilimfanya kuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakifuatiliwa kwa karibu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).

Kiwango chake kiliwavutia viongozi wa Simba Queens ambao walimsajili Septemba 2025 kwa mkataba wa miaka miwili, wakiamini angekuwa sehemu ya kuimarisha kikosi hicho.

Tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wachezaji wapya wanaochukua muda kuzoea mazingira ya timu kubwa, Elizabeth aliingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Simba Queens na kuanza kupata nafasi ya kucheza.

ELI 03

Kila alipopewa nafasi, alionyesha utulivu, ujasiri na uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake katikati ya uwanja.

Akiwa kiungo, Elizabeth amekuwa muhimu katika kuvunja mashambulizi ya wapinzani, kurejesha umiliki wa mpira na kuanzisha mashambulizi ya Simba Queens.

Uwezo wake wa kufika kwenye matukio kwa wakati, kupoka mipira na kucheza pasi sahihi, umemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaoaminiwa zaidi na benchi la ufundi la Simba Queens.

Maendeleo hayo hayakuishia ngazi ya klabu. Kiwango alichokionyesha akiwa Simba Queens kilimfungulia milango ya kuitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars hatua inayothibitisha namna ambavyo juhudi na kazi yake zimeanza kuzaa matunda.

ELI 02

ALICHOKIFANYA ALLIANCE

Kiungo huyo alikulia Alliance ambayo ni mojawapo ya akademi zinazokuza vipaji vya vijana wengi.

Alicheza Alliance kwa misimu mitatu kabla ya kuhamia Simba Queens, akiwa kikosini hapo alikuwa mmoja wa viungo waliokuwa wakipewa nafasi chini ya kocha Ezekiel Chobanka ambaye kwa sasa anaitumikia Ceasiaa Queens.

Kiungo huyo alikuwa akiunda pacha bora na Elizabeth Nashon ambaye wako wote kwenye kikosi cha Simba Queens na Elizabeth John anayekipiga JKT Queens.

Wote waliunda utatu kwenye safu ya kiungo, baada ya misimu miwili wote wakatimkia timu kubwa baada ya kupata uzoefu na kuonyesha kiwango bora hasa wakicheza dhidi ya vigogo.

ELI 04

PACHA NA CORAZONE

Kitendo cha kupewa nafasi na kuitumia vizuri kimemfanya kuunda pacha nzuri ya kiungo na Vivian Corazone.

Wawili hao wamekuwa wakicheza kwa kuelewana zaidi kutokana na Corazone kuwa na uzoefu mkubwa akiwa Simba Queens, huku Elizabeth akiwa mgeni baada ya kuwa msimu wake wa kwanza.

Eneo analocheza wapo nyota ambao walikuwa wakipata nafasi kabla ya ujio wake akiwemo Ester Mayala ambaye yupo nje kwa matibabu akiuguza jeraha la goti.

ELI 05

SILAHA YA MGOSI

Kwenye wakati ambao kocha wa timu hiyo, Mussa Hassan 'Mgosi' alipokuwa akipambania kuurejesha ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu, hii ndio ilikuwa silaha yake ya siri.

Baadhi ya mechi ngumu za kuamua ubingwa dhidi ya JKT Queens na Yanga Princess, Mgosi alimtumia Elizabeth kuvuruga safu ya ushambuliaji ya timu pinzani jambo lililokuwa sapraizi kwao.

Hata alipopewa nafasi ya kucheza dhidi ya vigogo hao, kiungo huyo alionyesha ukomavu mkubwa na kuitumia vyema nafasi aliyopewa kama silaha ya kocha huyo.

Elizabeth hajapata umaarufu mkubwa kutokana na nafasi anayocheza lakini ni miongoni mwa viungo waliofanya kazi kubwa kwenye kikosi cha Simba msimu uliotamika.

ELI 06

TIMU YA TAIFA

Kabla ya kusajiliwa Simba Queens, awali aliwahi kuitwa kwenye kikosi cha timu za taifa za Serengeti Girls na Tanzanite Queens.

Kiwango alichoonyesha msimu huu kimemfanya kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime kumuongeza kwenye kikosi cha Twiga Stars kinachojiandaa na mashindano ya WAFCON.

Ikumbukwe kuwa kocha Shime anasifika kwa kuwapa nafasi mabinti wadogo wanaochipukia ambao wanaonyesha uwezo mkubwa.

WAFCON hii kama atapata nafasi ya kucheza na kuonyesha ubora wake, bila shaka Elizabeth anaweza kuwa moja wa nyota watakaoonekana kwenye jukwaa hilo kubwa la kuuza vipaji.

Kwa alichokifanya Elizabeth anatambulika kama mmoja wa viungo wenye mustakabali mkubwa katika soka la wanawake Tanzania.

Akiwa bado binti mdogo, ana nafasi ya kuendelea kujifunza, kukua na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Simba Queens na Twiga Stars hapo baadae.

Kutoka Alliance Girls hadi Simba Queens, safari ya Elizabeth Joseph ni ushahidi kwamba vipaji vinapopewa nafasi na kuungwa mkono, vinaweza kuonyesha viwango vya juu na kuwa mfano kwa kizazi kijacho.

ELI 01

MSIKIE MGOSI

Akimzungumzia  kiungo huyo, kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi anasema kwa uwezo wake anaona anaweza kutumika kwa miaka mingi.

"Uwezo anaouonyesha anaweza kutumika miaka mingi ijayo, ni mchezaji mzuri na anafuata yale ambayo anaelezwa kufanikisha malengo, kila anapopata nafasi anauonyesha uwezo wake ingawa bado naamini ana mengi ya kutoa," anasema Mgosi.