Lake Victoria Marathon kusaidia watoto njiti
Muktasari:
- Mratibu wa mashindano hayo, Hilda Viggo, amesema hayo jijini Mwanza, Jumamosi iliyopita, akieleza kuwa maandalizi yanalenga kuhakikisha msimu wa sita wa mbio hizo unakuwa na mafanikio makubwa.
ZAIDI ya wakimbiaji 3,000 wanatarajiwa kushiriki mbio za Lake Victoria Marathon 2026 zitakazofanyika Novemba 15, mwaka huu, katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, huku waandaaji wakilenga kuvuka rekodi ya washiriki 2,870 iliyowekwa mwaka jana.
Mratibu wa mashindano hayo, Hilda Viggo, amesema hayo jijini Mwanza, Jumamosi iliyopita, akieleza kuwa maandalizi yanalenga kuhakikisha msimu wa sita wa mbio hizo unakuwa na mafanikio makubwa.
Amesema washiriki watashindana katika makundi manne, ambayo ni mbio za kilomita 2.5 kwa watoto, kilomita tano za burudani, kilomita 10 kwa washiriki kutoka kampuni mbalimbali na kilomita 21 za nusu marathoni.
Kwa mujibu wa Hilda, mbio hizo zitaanzia na kumalizikia Uwanja wa Furahisha, zikiwa na malengo ya kukuza mchezo wa riadha, kuimarisha uchumi wa Mwanza, kuunganisha jamii kupitia michezo na kutangaza vivutio vya utalii vya Kanda ya Ziwa.
Mbali na ushindani wa riadha, mashindano hayo yanalenga pia kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, maarufu kama watoto njiti, ambao hukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya.
Hilda amesema takribani watoto njiti 10,000 huzaliwa kila mwaka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, huku kati ya 4,000 na 5,000 wakipoteza maisha. Amesema hali hiyo imewafanya waandaaji kuelekeza sehemu ya juhudi zao katika kusaidia watoto hao kwa mwaka wa pili mfululizo.
“Kati ya watoto hao 10,000 wanaozaliwa, takribani 4,000 hadi 5,000 hupoteza maisha kila mwaka. Hivyo, tumeona tutumie mbio za mwaka huu kusaidia jamii kwa kukusanya fedha za kuwasaidia watoto njiti. Tunafanya hivi kwa mwaka wa pili sasa,” amesema Hilda.
Ameongeza kuwa mbio hizo zitatoa fursa ya kuelimisha jamii kuhusu changamoto zinazowakabili watoto njiti, huku akiwataka wananchi kujisajili na kushiriki ili kusaidia kufanikisha lengo hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza, Edwin Ngonyani, amesema Lake Victoria Marathon imekuwa na mchango katika kukuza riadha, kuibua vipaji vya vijana na kutangaza vivutio vya utalii katika Kanda ya Ziwa.
Ngonyani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ufundi wa mashindano hayo, amesema mbio hizo zimehamasisha vijana kuunda vikundi vya kukimbia na kutoa fursa zaidi za kuendeleza vipaji vya riadha. “Ni furaha yetu kuona mbio hizi zikiendelea kufanyika. Tunaomba watu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kushiriki ili lengo lake lifanikiwe,” amesema Ngonyani.
Naye Meneja Biashara wa Mixx by Yas Kanda ya Ziwa, Charles Elisante, amesema kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono mashindano hayo kutokana na mchango wake katika kuhamasisha afya bora, kujenga mshikamano na kusaidia jamii, hususan watoto njiti.