KVZ yashusha mashine tano mpya Rwanda
Muktasari:
- Baada ya awali KVZ kutambulisha nyota wapya wanne huku ikiwaaga sita, timu hiyo imeendelea na maboresho ya kikosi kwa kuongeza mashine zingine tano na kufanya jumla kuwa tisa.
WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), timu ya KVZ ikijiandaa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kagame Cup yanayoanza, leo Ijumaa Julai 24, 2026 nchini Rwanda, imeonesha haitaki utani katika kuimarisha kikosi chake.
Baada ya awali KVZ kutambulisha nyota wapya wanne huku ikiwaaga sita, timu hiyo imeendelea na maboresho ya kikosi kwa kuongeza mashine zingine tano na kufanya jumla kuwa tisa.
Wachezaji waliotambulishwa hivi karibuni ni mshambuliaji Muhammed Mussa Haji ‘Banega’ kutoka Uhamiaji, kiungo mshambuliaji Mohammed Shaaban ‘Kwacha’ kutoka Malindi, kipa Hamad Ubwa ‘Baro’ kutoka Mlandege, mshambuliaji Akram Muhina Omar ‘Haaland’ kutoka KMC na beki wa kati Munir Abdu Shafi ‘Mlipili’ kutoka Kipanga.
Taarifa iliyotolewa na timu hiyo, ilisema wanayofuraha ya kuwatambulisha wachezaji hao ambao wanaamini wataandika historia kwa kuisaidia timu kufanya vizuri zaidi.
Pia, timu hiyo ilisema milango ya timu hiyo ipo salama kutokana na kumsajili kipa atakayesimama imara kulinda nembo ya KVZ.
“Tunawaamini na tunawasubiri mtuandikie historia mpya kwa kufunga mabao mengi, karibuni kwenye familia ya mabingwa ya Kikosi Cha Valantia Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo.
Mbali na hilo, timu hiyo imemuaga mshambuliaji Michael Joseph aliyejiunga na Mashujaa inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Asante kwa kujitolea, nidhamu na mchango wako mkubwa ukiwa sehemu ya familia yetu, leo tunakuaga kwa heshima huku tukikushukuru kwa kila ulilolifanya ndani na nje ya uwanja. Tunakutakia kila la kheri katika hatua yako mpya ya soka, endelea kung’ara, kuwakilisha vipaji vyako na kufikia mafanikio makubwa zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Awali timu hiyo ilitambulisha nyota wanne ambao ni Hamid Bakari Omar ‘Gaucho’, Nature Mwakilembe, Said Mussa ‘Mbeki’ na Agustino Chalamba ‘Kaseke.
KVZ ipo Kundi C na timu za Al Hilal ya Sudan, Rayon Sports (Rwanda) na Tusker (Kenya). Mechi ya kwanza itacheza Julai 26 dhidi ya Rayon, kisha Julai 29 itaikabili Al Hilal, itamaliza makundi Agosti 1 kupambana na Tusker.