KVZ yatwishwa zigo Zanzibar
Muktasari:
- Waziri huyo ameyasema hayo Julai 19, 2026 wakati akiiaga timu hiyo iliyoanza safari yake kuelekea Rwanda kwa ajili ya mashindano ya Kagame yanayoanza Julai 24, 2026 nchini humo.
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Juma Pembe, amewasihi wachezaji wa timu ya KVZ kuipambania na kuilinda heshima ya Zanzibar kimataifa.
Waziri huyo ameyasema hayo Julai 19, 2026 wakati akiiaga timu hiyo iliyoanza safari yake kuelekea Rwanda kwa ajili ya mashindano ya Kagame yanayoanza Julai 24, 2026 nchini humo.
Pembe amewatia nguvu wachezaji hao kwa kuwaambia wasikubali kushindwa kirahisi kwani Zanzibar ipo mabegani kwao.
“Nawataka mcheze mpira bila uoga, huko hamuendi kufanya majaribio badala yake mnaenda kushindana, hivyo nahitaji muwe tayari kuipigania nchi,” amesema.
Pia, waziri huyo amewasihi wachezaji hao kulinda tamaduni za Zanzibar na sio kufuata za wageni.
Naye, Mkuu wa Kikosi hicho, Kanali Said Ali Shamhuna, amesema anatambua kuwa kundi lao sio jepesi kwani limebeba mabingwa wa nchi mbalimbali lakini watahakikisha wanatoa ladha tofauti.
Amesema, timu hiyo imewekeza katika mchezo wa mpira wa miguu zaidi ya miaka 22 na hatimaye msimu wa 2025-2026 wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.
Alieleza kuwa, kikosi hicho kina hamu na kiu ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa na wanatarajia kuweka historia nzuri mwaka huu na wataweka runinga kubwa makao makuu ya kikosi hicho kwa lengo la kuwapa sapoti huko walipo.
Mkuu huyo amesema kikosi hicho kinaondoka na watu 48 kuelekea Rwanda wakiwemo wachezaji na viongozi wa timu.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali, amesema wanafurahi kupata nafasi hiyo kwani kwasasa ni ngumu kupata mechi za namna hiyo wanapojiandaa kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema, timu hiyo haendi kushiriki badala yake inaenda kushindana kama ilivyo kwa timu zingine.