Kombe la Mapinduzi sasa macho kodo
Muktasari:
Huo utakuwa ni msimu wa 10 tangu michuano hiyo ilipoanzishwa kwa mfumo mpya unaotumika sasa mnamo mwaka 2007.
MSIMU mwingine wa michuano ya Kombe la Mapinduzi umeingia ambapo kuanzia Ijumaa ya wiki hii vumbi litaanza kutimkia kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar kuashiria kuanza kwa michuano hiyo.
Huo utakuwa ni msimu wa 10 tangu michuano hiyo ilipoanzishwa kwa mfumo mpya unaotumika sasa mnamo mwaka 2007.
Michuano hii hufanyika kila mwaka ikiwa ni sehemu ya sherehe za Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964 na yamekuwa maarufu kwelikweli kutokanailivyo na mvuto uliochagizwa na ushiriki wa timu zake.
Mashabiki wa soka visiwani Pemba na Unguja, hukaa mguu sawa kwa ajili ya kutaka kuanza kwa michuano hiyo kwani hupata burudani ambao huikosa kwa muda mrefu, kuzishuhudia timu maarufu nchini za Simba na Yanga zikiumana.
Mbali na wakongwe hao, pia mialiko kwa timu za kigeni kutoka nje ya Tanzania ni sababu nyingine inayowasisimua wengi na kuwapa fursa ya kuwaona nyota ambao ni nadra kwenda visiwani kucheza mechi ya yoyote.
Katika mashindano ya msimu huu jumla ya timu tisa zitachuana, zikiwa kwenye makundi mawili, Kundi A likiwa na timu za Simba ya Dar es Salaam, URA ya Uganda, KVZ, Taifa ya Jang’ombe na Jang’ombe Boys zote za Unguja.
Katika Kundi B kuna klabu za Yanga na Azam za Dar es Salaam, Zimamoto ya Unguja na Jamhuri ya Pemba, ambapo kila kundi litatoa timu mbili za kucheza hatua na nusu fainali kabla ya kupatikana za kucheza fainali itakayopigwa Ijumaa ya Januari 13, 2017.
WAPINZANI WA JADI
Michuano ya mwaka huu inafunguliwa na pambano la wapinzani wa jadi, Taifa ya Jang’ombe na Jang’ombe Boys timu ambazo kwa sasa visiwani Unguja ndizo zenye mashabiki wengi wenye mzuka na soka.
Timu hizo zinatoka mtaa mmoja wa Jang’ombe na kufanya upinzani wao uwe bab’kubwa.
Lakini kama haitoshi pia kuna uwezekano mkubwa wa kushudiwa tena kwa pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali na hata ikiwezekana fainali, kitu kinachowafanya mashabiki sasa kukaa mkao wa kula wa kusubiri burudani ya aina yake 2017.
UTAMU ZAIDI
Ingawaje JKU safari hii haimo kwenye michuano hiyo, lakini bado kuna klabu ambazo zitaongeza utamu kwenye michuano ya msimu huu. Watetezi URA, Azam, Yanga, Simba, KVZ, Zimamoto na Jamhuri sambamba na watoto wa Jang’ombe, zote zinaonekana kuipania vilivyo michuano ya safari hii, kwani zinaendelea kujifua kwa njia tofauti.
Simba, Yanga na Azam zenyewe zinamalizia mechi zao za Ligi Kuu Bara kesho na keshokutwa kabla ya kuvuka bahari kuanza kitatange cha michuano hiyo, lakini klabu za Zanzibar zipo kwenye jaramba baada ya Ligi Kuu visiwani humo Kanda ya Unguja na Pemba kumaliza duru la kwanza.
Klabu hizo zimeongezewa chaji baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili kwa visiwani hivyo, hali inayozifanya kujiimarisha zaidi kukiwan na tambo kuwa hawataki kuliona taji hilo likivuka tena maji kwenda kwingine.
MACHO KODO
Simba na Yanga ndizo klabu zinazodokolewa macho na mashabiki wa soka, hasa kutokana na ubora wa vikosi hivyo na ujio wa makocha wapya wa kimataifa na nyota wengine wa ndani na nje ya nchi.
Simba itaenda visiwani humo safari hii ikiwa na Kocha mwingine, Joseph Omog tofauti na ilivyokuwa katika mwaka huu ambapo Wekundu wa Msimbazi walienda visiwani humo na Mwingereza, Dylan Kerr na Mganda Jackson Mayanja aliyekuwa Msaidizi na kushuhudiwa akipewa timu jumla.
Watani zao Yanga, ilienda Kombe la Mapinduzi iliyopita ikiwa na Hans Pluijm ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi, huku kikosi kikiwa chini ya Mzambia George Lwandamina akiwa wala hana muda mrefu tangu atue.
Mbali na makocha, lakini hata kwenye vikosi vya klabu hizo na Azam zitaenda Zanzibar zikiwa na sura mpya kadhaa waliosajiliwa kwenye mwanzoni mwa msimu na kwenye dirisha dogo na kufanya msisimko uwe mkubwa zaidi.
INASAIDIA MKO KLABU
Unaweza ukaichukulia poa michuano hii, lakini kwa yakini imekuwa msaada mkubwa kwa klabu wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya kimataifa ambayo huanza kila mwanzoni mwa mwaka.
Klabu za Yanga, Azam, Zimamoto na KVZ zina kibarua kigumu kwenye michuano ya Ligi a Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, uwepo wa Kombe la Mapinduzi ni msaada wao katika kufanyaa maandalizi ya Afrika.
Kuwepo kwa mseto wa timu tofauti unaweza kusaidia klabu hizo kujiweka sawa kabla ya kuanza majukumu yao mapema Februari mwakani zitakapoanza kuchezi zao za mkondo wa kwanza na pili kabla ya michezo ya hatua nyingine.
Hata klabu zisizoiwakilisha nchi zinanufaika na michuano hii katika maandalizi ya mechi za ligi zao kwa zile zisizoshiriki michuano ya kimataifa kama Simba, Jang’ombe Boys, Taifa Jang’ombe na Jamhuri ya Pemba.
Kama kungekuwa na uwezekano mkubwa, Kamati ya mashindano hayo ikafanya jitihada za kuongeza timu shiriki kutoka nje ili kuongezsa utamu zaidi na kuzinoa makali klabu zetu zinazotuwakilisha anga la kimataifa.
KULIKO PEMBA KULIKONI?
Michuano hii ya Kombe la Mapinduzi ndiyo pekee inayoweza kuzipima klabu za Pemba na Unguja kuona vikivyoimarika, hivyo ni lazima waandaji wake kuangali namna ya kutoa uwiano mzuri wa timku shiriki za visiwani hivyo.
Mara kadhaa timu za visiwani Pemba vinapotezwa kimtindo kwa mfano msimu huu kuna Jamhuri tu, huku Unguja ikiwa na klabu nne na nne nyingine zikiwa ni zinazotoka Tanzania Bara na nje ya nchi.
Kuna haja ya waandaji kufikiria hata kutumia njia mpya ya kupata wawakilishi wa Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi hata kwa kuanzisha mchujo wa awali kabla ya kupatikana zitakazoumana na vigogo kutoka nje ya visiwani hivyo.
VITU MUHIMU
Michuano ikitarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii, kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa kuifanya michuano hiyo inoge zaidi, kwanza umakini wa waamuzi watakaopichezesha.
Umakini huo utakaozingatia sheria 17 za mchezo huo zitaifanya michuano hiyo isisimue zaidi na hata bingwa atakayepatikana awe aliyetokwa na jasho na sio mipango mipango. Pia umakini wao utapunguza lawama dhidi yao kwani waamuzi wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa lawama kwa maamuzi yao tata, hata pale klabu zinapopoteza mechi kwa udhaifu wao.
Jingine ni kufanywa jitihada za kusakwa kwa wadhamini ili michuano hiyo inoge zaidi na kuonyesha ushindani kwa timu shiriki, ingawa kamati inajitahidi kwa namna inavyoendesha michuano tangu ilipoanza mwaka 2007.
Iwapo wadhamini watapatikana itakuwa rahisi zaidi suala la kuongeza idadi ya timu kutoka nje ya nchi kwani kamati ya mashindano itakuwa na uwezo wa kuzihudumia na hata uwezo wa kuongeza kiwango cha fedha cha zawadi.
Mwisho ni watazamaji na mashabiki wa soka wa ndani na nje ya visiwani hivyo kujitokeza kwa wingi kwenye mechi bila kujali nyakati, sambamba na kuwa na ustaarabu kwa muda wote ambao michuano hiyo itafanyika mpaka iishapo.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania[TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020