Kocha TRA United aanza mkwara
Muktasari:
- Pia amesema wakati ligi kuu ikisimama kupisha kalenda ya kimataifa, hawatakuwa na mapumziko ya muda mrefu kutokana na ugeni alionao kikosini pamoja na wachezaji wake badala yake lazima watumie muda mwingi kujifua.
PAMOJA na kuanza kwa ushindi mnono wa mabao 3-1, Kocha Mkuu wa TRA United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema bado timu hiyo inahitaji maboresho kuhakikisha anatengeneza muunganiko bora kikosini na kuwa tishio Ligi Kuu.
Pia amesema wakati ligi kuu ikisimama kupisha kalenda ya kimataifa, hawatakuwa na mapumziko ya muda mrefu kutokana na ugeni alionao kikosini pamoja na wachezaji wake badala yake lazima watumie muda mwingi kujifua.
Morocco alikabidhiwa mikoba ya timu hiyo akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Ettiene Ndayiragije aliyeiongoza mechi tano akivuna pointi tatu, ambapo juzi akiiongoza mchezo wa kwanza, TRA United ilishinda ugenini mabao 3-1.
Baada ya kesho Jumatano, Ligi Kuu inatarajia kuendelea Oktoba 10, ambapo TRA United itakuwa ugenini tena kukipiga dhidi ya Namungo, mchezo ukipigwa uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, ukiwa wa raundi ya nane kwa wenyeji na saba kwa vigogo hao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Morocco amesema matokeo hayo ni mwanzo mzuri kwake na haihitaji kubweteka kwakuwa ligi ni ngumu akiwapongeza nyota wake kwa kuingia haraka katika mfumo wake.
Amesema licha ya ushindi huo lakini yapo makosa binafsi aliyobaini kwa nyota wake, kwakuwa zipo nafasi zilizopatikana lakini walishindwa kuzitumia akieleza kuwa mapumziko hayo yatakuwa maalumu kwake kusahihisha na kuboresha.
“Hatutarajii kupumzika kwa muda mrefu kwakuwa bado nina ugeni na vijana, hivyo lazima tutumie muda mwingi kujifua, ligi ni ngumu na kila timu inayo malengo yake kama tulivyo sisi, kiujumla niwapongeze wachezaji,” amesema kocha huyo.
Kocha huyo ameeleza mkakati wake ni kuona wanasaka rekodi na historia mpya kwa kuzidi mafanikio waliyopata msimu uliopita, akieleza lolote linawezekana iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.