Morocco aanza kwa kishindo TRA United, Pamba Jiji hali tete
Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania aliyezifundisha klabu mbalimbali zikiwemo, Simba, Namungo FC na Geita Gold za Bara, aliteuliwa kuifundisha TRA United, Septemba 10, 2026, baada ya kuondoka kwa Mrundi, Etienne Ndayiragije.
KOCHA Mkuu wa TRA United, Hemed Suleiman 'Morocco', ameanza vyema kampeni yake ya kukiongoza kikosi hicho, baada ya leo kushinda mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji, ikiwa ni ushindi wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo, Septemba 10, 2026.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania aliyezifundisha klabu mbalimbali zikiwemo, Simba, Namungo FC na Geita Gold za Bara, aliteuliwa kuifundisha TRA United, Septemba 10, 2026, baada ya kuondoka kwa Mrundi, Etienne Ndayiragije.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ilionekana nyepesi kwa wageni baada ya kufunga mabao matatu katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, jambo lililotengeneza mazingira magumu zaidi kwa Pamba Jiji.
Katika mechi hiyo, Mnigeria Ani Prince Elijah aliifungia TRA United bao la kwanza dakika ya tano, kisha beki wa kati wa Pamba Jiji raia wa Nigeria, Nonyem Okorocha akajifunga mwenyewe dakika ya nane, akiwa katika harakati za kuuokoa mpira.
Wakati Pamba Jiji ikipambana kuhakikisha inasawazisha mabao hayo, ilishtuliwa kwa kuchapwa bao la tatu dakika ya 39, lililofungwa na mshambuliaji wa kikosi hicho, Emmanuel Mwanengo anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Yanga.
Jitihada za Pamba Jiji zilionekana dakika ya 77, baada ya mshambuliaji, Abdulkarim Yunus aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Black Bulls FC ya Msumbiji kuifungia timu hiyo bao lake la kwanza kikosini na la kufutia machozi.
Ushindi huo kwa TRA United ni wa kwanza kwa timu hiyo msimu huu katika Ligi Kuu, huku ukiwa ni wa kwanza pia kwa kocha wa kikosi hicho, Hemed Suleiman 'Morocco' aliyechukua nafasi iliyoachwa na mtangulizi wake, Mrundi, Etienne Ndayiragije.
Ndayiragije aliyejiunga na TRA, Novemba 16, 2025, akitoka Kenya Police FC ya Kenya aliyoipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2024-2025, aliondoka kikosini humo Septemba 7, 2026, kwa makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba wake.
Katika mechi tano Ndayiragije alizoiongoza TRA United kwenye Ligi Kuu msimu wa 2026-2027, alitoka sare tatu na kupoteza mbili na kuiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya 13 na pointi tatu, huku ikifunga mabao matatu na kuruhusu matano.
Ushindi wa leo unaifanya TRA kusogea hadi nafasi ya 12, ikitoka nafasi ya 13 na pointi sita, huku kwa upande wa Pamba Jiji ikiwa na mwenendo mbaya hadi sasa, baada ya kucheza mechi sita na kati ya hizo imechapwa tano na kutoka sare moja.
Pamba Jiji inayofundishwa na Kocha Mkuu, Mkenya Francis Baraza katika mechi hizo sita ilizocheza hadi sasa, imefunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13, ikiburuza mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi moja.