Kocha KMKM: Ndondo tatizo kwa wachezaji ZPL
Muktasari:
- Katika mchezo wa mwisho iliyocheza Oktoba 10, 2026, KMKM imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi.
KOCHA wa KMKM, Othman Hassan 'Kocha King', amesema ukosefu wa mapumziko kwa wachezaji baada ya kumaliza ligi ni moja ya changamoto zinazochangia kushuka kwa kiwango cha baadhi ya wachezaji Zanzibar.
Ameeleza kuwa, wachezaji wengi baada ya kumaliza msimu, huingia moja kwa moja kwenye mashindano mbalimbali ya ndondo, jambo ambalo huwanyima fursa ya kupumzika na kurejesha nguvu kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
"Hali hii huwafanya wachezaji kukabiliwa na uchovu wa mwili na kushindwa kufikia kiwango chenye ubora, jambo hili linaweza kuathiri uwezo wa timu kufanya vizuri kwenye michezo ya ushindani," amesema.
Kwa mujibu wa Kocha King, KMKM ilianza msimu huu ikiwa inakabiliwa na tatizo hilo, ambapo uchovu ulichangia timu kupoteza baadhi ya michezo katika hatua za mwanzo za msimu.
Amesema, katika kukabiliana na changamoto hiyo, benchi la ufundi limeanza kupunguza mzigo wa mazoezi na kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kupumzika ili kurejea katika hali yao nzuri ya kimwili.
Aidha, amesema benchi la ufundi linatumia mkakati wa kutokuwa na kikosi kimoja cha kudumu ili kuwapa wachezaji wengi nafasi ya kucheza, jambo linaloifanya timu kuwa bora na utayari wa kimwili wakati wote wa msimu.
Akizungumzia mwenendo wa timu baada ya kuanza kupata matokeo mazuri, kocha huyo alisisitiza kuwa bado kuna kazi ya kufanya kwani kila mchezo una changamoto zake.
Amesema, KMKM itaendelea kujenga kikosi, kusimamia hali ya wachezaji, na kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha timu inakuwa katika ushindani kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar.
Katika mchezo wa mwisho iliyocheza Oktoba 10, 2026, KMKM imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi.