Prime
Kocha Gaborone aishtukia Yanga
KOCHA wa Gaborone United, Sean Connor, amekesha akiangalia mikanda ya mechi za Yanga wakiwa nyumbani na kuthibitisha kwamba si rahisi kukabiliana na mabingwa hao wa Tanzania wanapocheza kwenye uwanja wao.
Gaborone United itakuwa na mchezo wa marudiano dhidi ya Yanga, utakaopigwa Septemba 12 kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, huku kila timu ikiwa na nafasi ya kusonga mbele baada ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Connor alisema baada ya sare ya mchezo wa kwanza amekuwa bize akiangalia mechi zilizopita za Yanga walizocheza nyumbani na kukubali kwamba si rahisi kuondoka na ushindi wanapocheza kwenye uwanja wao.
Connor alisema amezifuatilia mechi za Yanga kuanzia msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo hakuna timu iliyofanikiwa kuondoka na ushindi, huku akiitaja Al Ahly kuwa timu pekee iliyowahi kuondoka na pointi.
Kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini, alisema rekodi hiyo ya Yanga, pamoja na namna wanavyoweka presha kubwa kwa wapinzani wao, imemfanya awatahadharishe wachezaji wake kuwa makini wanapojiandaa kuja Tanzania kumalizana na mabingwa hao.
Gaborone United itatua nchini Alhamisi, Septemba 10, alfajiri, tayari kwa kukutana na Yanga, huku kila timu ikihitaji ushindi kusonga mbele, isipokuwa wageni hao wanaweza pia kusonga mbele iwapo watapata sare ya mabao 2-2 au zaidi.
“Nimekuwa nikiangalia mechi zao za nyuma na nataka nikwambie wazi kwamba si rahisi kukabiliana na Yanga ikiwa nyumbani. Wana rekodi kubwa na wanacheza kwa njaa kubwa ya ushindi. Haitakuwa mechi rahisi,” alisema Connor.
“Nimetafuta mpaka mechi ambazo wamecheza kwenye huo uwanja ambao tutautumia, nako hakuna nafuu sana. Tunatakiwa kujiandaa kukutana na presha kubwa ambayo itatoka uwanjani na kwa mashabiki wao.
“Nimewaambia wachezaji wangu tutakuwa na mchezo mgumu. Tukifanikiwa kupita hapa, tunaweza kufika mbali kwa kuwa tunakwenda kukutana na timu ambayo, kama hatutakuwa na hesabu sawasawa wakati wanatushambulia na wakati tunapounasa mpira, itakuwa kazi kubwa.”