Klabu zinaimeza Taifa Stars taratibu
Muktasari:
HAINA mvuto wowote. Kwa miaka ya hivi karibuni kila ninapoziangalia mechi za Ligi Kuu Barahuwa sipati mvuto na raha, licha ya kwamba kuna ushindani mkubwa katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
HAINA mvuto wowote. Kwa miaka ya hivi karibuni kila ninapoziangalia mechi za Ligi Kuu Barahuwa sipati mvuto na raha, licha ya kwamba kuna ushindani mkubwa katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Ligi Kuu ya msimu huu imemaliza mzunguko wake wa kwanza, lakini mechi zake zilizokuwa zikionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni, hazikuwa zikisisimua kama tunavyosisimka kwenye mechi za ligi za mataifa mengine zinazoonyeshwa kwenye runinga.
Tokea kipenga cha mwanzo hadi cha mwisho cha mwamuzi kupulizwa hujikuta sijapata raha wala faraja ambayo ilinifanya kwenda kuangalia mechi hiyo iliyochezwa.
Hali hii inanitokea zaidi timu zinazofanya vizuri kwenye ligi hiyo hivi sasa Yanga, Azam na Simba za Dar es Salaam zinavyocheza na kwa bahati mbaya ndizo ambazo mechi zao zinaoneshwa moja kwa moja katika ligi hiyo.
Hali hiyo inayonikuta hivi sasa ni tofauti na ule msisimko niliokuwa na upata wakati nikiangalia mechi za Ligi Daraja la Kwanza ambayo sasa inaitwa Ligi Kuu katika miaka ya 80 na 90 pale Uwanja wa Taifa ambao sasa unajulikana kwa jina la Uwanja wa Uhuru.
Hapa sizungumzii msisimko uliokuwa unapatikana wakati wa kizazi cha wachezaji shoka waliopatikana Tanzania miaka ya nyuma, ambao walikuwa wanaburudisha labda ni kwa vile wakati huo soka ilikuwa ni burudani na haikuwa na fedha kama hivi sasa.
Nimetafakari na kugundua kwamba sasa Yanga, Azam na Simba hawanipi burudani ninayoitaka kwa vile vikosi vyao mara nyingi huundwa na wachezaji kutoka nje ya Tanzania. Si kwamba siwapendi wageni kucheza nchini, lakini ningefurahi kuwaona kwamba wana vitu tofauti ambavyo wachezaji wazawa hawana.
Hainifurahishi timu kuwa na wachezaji saba wa kigeni katika kikosi chake, lakini ikashindwa kupata bao katika mechi hadi pale kocha atakapowapunguza wageni uwanjani na kuwaingiza wazawa ndipo bao linapatikana.
Kwa kweli wachezaji wengi wa kigeni waliopo nchini, hata katika timu nyingine mbali na hizo tatu viwango vyao vya uchezaji haviwazidi wachezaji wazawa na wakati mwengine kocha akiwa mkweli wanalazimika kusugua benchi.
Lakini kinachosikitisha wachezaji wengi wa kigeni ndio wanaosajiliwa kwa fungu kubwa la fedha na ndio wenye mishahara mikubwa na wanapata huduma za ziada kuliko wenzao wa Tanzania.
Pamoja na upendeleo huo huduma inayotolewa na wachezaji hao wa kigeni wakati mwingine unaweza kujiuliza kwa kile mchezaji anachokifanya uwanjani kama ni kweli amesajiliwa kutoka nje ya nchi.
Kuna haja kwa klabu kutafakari upya inapotaka kusajili wachezaji wa kigeni ili wasajili wa wachezaji ambao wanakiwango cha juu kwa lengo la kusaidia timu zao na pia kuwapa nafasi kwa wachezaji wa Tanzania kupata nafasi ya kujifunza kutoka kwao.
Ile hali ya klabu kusajili wachezaji wa kigeni bila kujali kiwango chao inafaa iachwe kwani haisaidii maendeleo ya soka katika nchi na wala hawasaidii kuzipa mafanikio klabu wanazozichezea.
Ni muhimu kwa klabu kuepuka kutafuta wachezaji wa bei chee katika usajili wa wachezaji wa kigeni, kwani wanapokuja nchini huwazibia nafasi wachezaji wazawa kupata nafasi ya kucheza na kuendeleza vipaji vyao.
Licha ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuweka vigezo vya mchezaji wa nje kusajiliwa nchini awe ni mchezaji wa timu ya taifa lake, lakini inadhihirisha klabu na TFF hawalitilii maanani suala hilo.
Kwa kuwa na wachezaji wengi wa kigeni hakutoi nafasi kwa wachezaji wazawa vipaji vyao kuviendeleza na kuonekana na hatimaye kupata nafasi ya kuhudumia timu yao ya Taifa na kuifanya timu hiyo kuwa legelege kila inaposhiriki michuano ya kimataifa.
Kipigo cha Taifa Stars ilichokipata hivi karibuni cha mabao 7-0 kutoka Algeria katika mechi ya hatua ya awali ya Kombe la Dunia, hakikuwa cha bahati mbaya bali kilitokana na sababu kadhaa za mipango isiyo endelevu. Sababu hiyo ya kuwa na rundo la wachezaji wa kigeni katika timu ambazo ndizo zinazotoa wachezaji wanaounda kikosi cha Taifa Stars.
Wakati umefika sasa kwa klabu za Tanzania kuingia katika mpango wa kuuza vipaji vya vijana, ili kuchukua nafasi katika timu zao badala ya mtindo wa sasa wa kusajili kundi la wachezaji kila kipindi cha usajili kinapofika.
Klabu zinatakiwa ziandae mpango ambapo katika kila usajili hasa ule wa dirisha kubwa kuwa na wachezaji angalau watano inayowasajili katika timu yake ya kwanza kutoka timu ya vijana.
Wachezaji hawa watakuwa na msaada mkubwa kwa timu husika kwani watakuwa wanaijua misingi na utamaduni wa klabu yao wanaoichezea na watacheza kwa mapenzi yao ya dhati na kutoa huduma inayostahili kwa timu yao.
Mara nyingi wachezaji wa kusajili kutoka timu nyingine hasa wa kigeni huwa hawana mapenzi ya dhati kwa timu anazochezea bali huchezea kama kazi tu kwa vile wanalipwa mishahara.
Klabu zijiandae kwa kuwa na vijana wake ambao itawakuza wenyewe na kuchukua vijana wengine kutoka Academy za nchini badala ya kung’ang’ania kusajili wachezaji wa Ligi Kuu au kutoka nje ya nchi.
Vijana hawa wakiendelezwa vizuri kwa kusajiliwa katika klabu na kupata mishahara watakuwa katika nafasi nzuri ya kuifanya Taifa Stars ing’are katika michuano ya kimataifa. Pia kuiwezesha Tanzania kutoa wachezaji wanaoweza kucheza soka lakulipwa nje ya nchi jambo ambalo litakuwa na manufaa makubwa kwa nchi na wachezaji wenyewe.
Tanzania ikiwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza nje ya nchi watapata mafunzo mazuri na kwa hiyo wataiyondoa Taifa Stars kutoka kuwa Kichwa cha Mwendawazimu na kuwa timu inayofanya vizuri katika michuano ya kimataifa na hapo nchi inaweza kucheza fainali la Kombe la Kimataifa Afrika na hata ile ya Kombe la Dunia.
Mbali na hilo wachezaji hao watakuwa wanalipwa vizuri na kuzisaidia familia zao kuondokana na umasikini na pia itawawezesha kuwa na miradi mbali mbali ambayo mbali na kuingizia pato taifa kwa njia ya kodi itatoa ajira zitakazosaidia vijana wengi wa Tanzania.
Bila kukuza soka la vijana Tanzania haiwezi kupiga hatua ya maendeleo ya maana katika mpira wa miguu kwani vijana ndio suluhisho la matatizo ya klabu zetu kutofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Nchi isipokuwa na mipango endelevu na kuendesha mambo kisayansi na klabu kuendeshwa kisasa mashabiki wa Soka wataendelea kuilaumu TFF hata ikifanya jambo gani. TFF haina muarubaini wa matatizo ya soka ya Tanzania bali klabu zikibadilika na kuendeshwa kisasa ufumbuzi utapatikana.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Bussiness Times (Mhariri Mwanzilishi wa Spoti Starehe) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF].
Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020