Kitasa IAA Aanika mipango yake
Muktasari:
- Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya ‘Play-Off’, baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.
BEKI wa kati wa IAA SC ya jijini, Arusha, Faisal Richard Mganga amesema ameamua kutafuta changamoto mpya katika maisha yake mapya na kikosi hicho, baada tu ya mkataba wake na KenGold FC ya Mbeya kufikia ukomo msimu uliopita wa 2025-2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Faisal amesema kabla ya msimu wa 2025-2026, kuisha ilikuwa ni ngumu kujua hatima yake baada ya mkataba wake na KenGold FC kufikia mwishoni, japo ofa aliyoipata ilirahisisha kuchagua kuichezea IAA SC ya Arusha.
“Nafasi niliyoipata ni muhimu kwangu ya kuendelea kuonyesha ubora wangu, nimesaini mkataba wa mwaka mmoja nikiamini kwa umoja wetu sisi wachezaji, viongozi na benchi la ufundi tutaisaidia IAA SC, licha ya ugeni wake Championship,” amesema.
Beki huyo aliyewahi pia kuichezea Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting, Namungo FC, Pamba Jiji, Ndanda FC, Tabora United kwa sasa TRA United, KenGold FC na Mbeya City, amesema ubora wa wachezaji wapya wa timu hiyo unawapa matumaini ya kufanya vizuri.
Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya ‘Play-Off’, baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.