Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipanga, JKU zavuna sita Pemba

KIPANGA Pict

KIPANGA FC na JKU SC zimeondoka kisiwani Pemba zikiwa na furaha baada ya kila moja kuvuna alama sita katika michezo miwili ya Ligi Kuu ya Zanzibar.

Kipanga imeibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mwenge SC kabla ya kuendeleza moto wake kwa kuichapa Fufuni SC mabao 3-1, na hivyo kukamilisha vyema safari yake ya Pemba kwa pointi sita, jumla inazo 15 ikiwa nafasi ya saba sawa na Muembe Makumbi iliyopo ya sita.

Kwa upande wa JKU SC, nayo imeonyesha makali kwa kuifunga Fufuni SC mabao 2-0 kabla ya kuichapa Mwenge SC mabao 3-1, matokeo yaliyoifanya kuondoka Pemba ikiwa na alama sita na kufikisha jumla ya pointi 23 ikikaa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kocha Mkuu wa Kipanga, Khamis Hassan Makame ‘Meki’, alisema amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyotekeleza majukumu yao katika safari hiyo na kuhakikisha wanaondoka na matokeo wanayoyataka.

Alisema kabla ya mchezo dhidi ya Fufuni aliwaeleza wachezaji wake umuhimu wa kucheza kwa umakini na kutumia vizuri nafasi watakazopata, akiamini wapinzani wao hawakuwa timu ya kuwachukulia kirahisi.

“Fufuni ni timu nzuri na kuifunga kunahitaji kutumia nguvu pamoja na akili. Bila kufanya hivyo unaweza kujikuta unapoteza mchezo, ndiyo maana niliwaeleza wachezaji umuhimu wa kushinda,” alisema Kocha Meki.

Aliongeza, pamoja na Fufuni kuwa na mwenendo ambao haukuwa mzuri katika siku za karibuni, Kipanga haikuruhusu hali hiyo kuifanya ishuke dimbani kwa kujiamini kupita kiasi.

“Ni kweli Fufuni imekuwa na muendelezo ambao si mzuri siku za hivi karibuni, lakini hilo halimaanishi kwamba tusiwaheshimu. Sisi tunaheshimu kila timu kwa sababu mpira una matokeo ya kushangaza,” alisema.

Wakati Kipanga ikifurahia pointi hizo sita, JKU nayo imeendelea kuonyesha ina malengo makubwa msimu huu baada ya kufanya kazi kubwa katika michezo yake miwili ya ugenini.

Kocha Mkuu wa JKU, Abdul-Saleh Mohamed Abdallah, alisema safari ya Pemba haikuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa wa timu walizokutana nazo, lakini amepongeza namna wachezaji wake walivyopambana.

Alisema wachezaji wake walijitoa, kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kutumia nafasi walizopata, jambo lililowasaidia kuondoka na ushindi dhidi ya Fufuni na Mwenge.

“Tunashukuru kwa kufanya vizuri katika michezo yetu miwili na kufanikiwa kupata alama sita. Pia tunafurahia kuwa kwenye nafasi nzuri katika ligi, kwani hilo ni miongoni mwa malengo yetu,” alisema Abdul-Saleh.

Kocha huyo alisema JKU ina malengo makubwa ya kupigania ubingwa msimu huu, hivyo matokeo ya safari ya Pemba ni sehemu ya hatua wanazochukua katika kutimiza ndoto hiyo.