Kipa apigwa nne, mashabiki wamkataa
Muktasari:
- Mabadiliko hayo yalifanyika katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar kati ya Kipanga na Polisi, uliochezwa Novemba 14, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.
KIPIGO cha mabao 4-1 kutoka kwa Polisi, kimeilazimisha Kipanga kufanya mabadiliko ya kipa dakika 10 kabla ya mechi kumalizika, kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.
Mabadiliko hayo yalifanyika katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar kati ya Kipanga na Polisi, uliochezwa Novemba 14, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.
Baada ya Polisi kuitembezea Kipanga kichapo hicho huku mchezo ukiwa unaelekea ukingoni, mashabiki wa timu hiyo walianza kupiga mayowe wakilitaka benchi la ufundi, linaloongozwa na Kocha Khamis Makame ‘Meki’, kufanya mabadiliko wakihofia mabao kuongezeka.
Mwanaspoti lilikuwepo uwanjani na lilishuhudia dakika chache baadaye, benchi hilo likimtoa kipa Hassan Dau na kumuingiza Rajab Abdallah, baada ya Dau kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Wakati Kipanga ikijiandaa kufanya mabadiliko hayo, mashabiki wa Polisi waliinuka kwa furaha na kumpigia makofi Dau alipokuwa akiondoka uwanjani.
Kipa huyo alionekana kuanza kupoteza morali baada ya kuruhusu bao la tatu lililofungwa kwa mpira wa adhabu, kabla ya Polisi kuongeza la nne na kuongeza presha kwa Kipanga.
Polisi walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0, kabla ya kuongeza mabao mengine mawili kipindi cha pili, huku Kipanga ikipata bao lake la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti. Katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mao A, JKU iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Raskazone, uliokuwa na ushindani mkubwa wa kutafuta nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
JKU ilikuwa ikihitaji ushindi huo ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuongoza msimamo, huku Raskazone ikisaka pointi za kuipandisha hadi nafasi ya tisa na kujiongezea nafasi ya kusalia Ligi Kuu.
Katika mechi nyingine iliyopigwa Gombani, Pemba, KMKM iliifunga Wembe mabao 3-0.