Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

King Kibaden : Mzaramo aliyepewa uchifu Songea-2

Muktasari:

  • Anabainisha kuwa mfumo huo haukuwafanya wawe na fedha za kutosha lakini uliwajengea heshima kwani hata wanachama nao walikuwa wakiwathamini na wengi walijitolea kwa ajili ya wachezaji na klabu.

WIKI iliyopita, tuliona jinsi nyota wa zamani wa Taifa Stars, Simba na Majimaji ya Songea, King Kibadeni ‘Mputa’ alivyojivunia heshima na utukufu katika medani ya soka kiasi cha kubatizwa majina mbalimbali, endelea….

Kocha huyo aliyezaliwa katika familia ya watoto wanane, anasema soka la wakati huo ilikuwa ni zaidi ya uwanjani, timu inayokusajili ilikuwa pia inajivika jukumu la kuhakikisha unapata ajira na makazi, vitu ambavyo viliwezekana kutokana na mapenzi ya mashabiki waliokubali kujitolea.

“Unaajiriwa kwa ajili ya soka na mshahara wako wa kazini ndio malipo ya kuitumikia klabu, mshahara utapata kazini kwako,” anasema na kuongeza kuwa zama hizo mchezaji ulikuwa pia ni mwanachama wa klabu na si kama ilivyo sasa.

Anasema kuichezea Simba au Yanga lazima uwe mwanachama hali hiyo ilisababisha ugumu kwa mchezaji kuhama klabu kwenda nyingine kwani ni sawa na kubadili uanachama.

“Ikitokea mchezaji akatoka Simba au Yanga na kwenda klabu mojawapo kati ya hizo anakuwa amepoteza uaminifu, hataaminika na daima anahesabiwa kuwa hana msimamo,” anasema.

Mchezaji huyo ambaye ana elimu ya ufundi magari Daraja la Pili (Motor Vehicle Mechanics Grade II) amewahi kuajiriwa katika kampuni mbalimbali, ajira ambazo kupatikana kwake kulichangiwa na kipaji chake cha soka.

Kocha huyo anasema kazi lilikuwa jambo mojawapo ambalo viongozi wa klabu wa wakati huo walilipa kipaumbele kutokana na ukweli kuwa klabu hazikuwa zinalipa wachezaji mishahara zaidi ya kugawana viingilio.

“Kuhama timu ilikuwa pia ni pamoja na kubadili au kuacha ajira ya awali jambo ambalo lilikuwa na mlolongo mrefu kidogo na labda hali hiyo ilichangia wachezaji kuchezea timu moja muda mrefu,” anasema.

Anabainisha kuwa mfumo huo haukuwafanya wawe na fedha za kutosha lakini uliwajengea heshima kwani hata wanachama nao walikuwa wakiwathamini na wengi walijitolea kwa ajili ya wachezaji na klabu.

“Zamani watu walikuwa na mapenzi ya kweli kwa klabu na moyo wa kujitolea ulikuwa mkubwa na ndio maana hata majengo ya klabu za Simba na Yanga yalijengwa kwa nguvu za makundi yote.”

Bao tatu, mechi moja

Kibadeni anajivunia mengi Simba tangu wakati huo ikiitwa, Sunderland, sifa hizo zinabebwa na historia ya Simba katika mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga pale walipowachapa mabao 6-0 mwaka 1977, ushindi ambao umeendelea kuwa rekodi ya kipekee na ya kujivunia katika historia ya Simba ambayo Yanga bado haijafanikiwa kuivunja.

Mechi hiyo iliyokuwa kama ya kulipa kisasi cha mabao 5-0 ambayo Simba walifungwa na Yanga mwaka I968, Kibadeni alipachika wavuni mabao matatu peke yake. Mengine yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ na Adam Sabu na moja beki wa Yanga, Seleman Sanga alijifunga akiokoa krosi ya Ezekiel Grayson ‘Jujuman’.

Kibadeni anabainisha kuwa mechi hiyo ilimrudisha miaka kadhaa nyuma wakati anajiunga Simba, alikerwa baada ya Simba kufungwa 5-0 na Yanga mwaka I968.

Anawataja wenzake waliounda kikosi kilichoiua Yanga iliyokuwa katika mgogoro uliozaa klabu ya Pan African ni Omar Mahadhi aliyekuwa langoni wakati wengine ni  Daud Salum ‘Bruce Lee’ na Mohammed Kajole ‘Machela’. Pia alikuwapo Athumani Juma, Aloo Mwitu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Aluu Ally, Iddi Kibonye, Ezekiel Grayson, Ismail Mwarabu, Abdallah Mwinyimkuu, Willy Mwaijibe, Abbas Dilunga na Martin Kikwa.

“Kilikuwa kikosi bora katika historia ya Simba,” anasema na kuongeza kuwa kipigo hicho kimebaki katika historia ya mechi za watani hao wa jadi.

Anaongeza kuwa msiba mkubwa ulikuwa wa Kipa Bernad Madale wa Yanga ambaye alitupiwa lawama lukuki lakini kimsingi walizidiwa.

Kibadeni anasema kona na mipira ya kurusha ya Kajole, uwezo wa Martin Kikwa na Adam Sabu wa kufunga mipira ya vichwa ilikuwa burudani ya aina yake na ingawa alikuwa na umbo dogo lakini alikuwa gumzo kutokana na kasi, wepesi na uwezo wake wa kumiliki mipira.

Siri ya mafanikio

Kocha huyo ambaye alikuwepo katika kikosi cha timu hiyo kilichofikia fainali za kwanza za Klabu Bingwa Afrika mwaka I974 akipachika bao la pili na la ushindi wa 2-0 dhidi ya klabu ya Hearts of Oak ya Ghana, mechi iliyochezwa nchini humo anasema siri ya mafanikio yake ni mazoezi.

Kibadeni ambaye pia alirudi Simba akiwa kocha mkuu na mwaka I993 kuiwezesha timu hiyo kufikia fainali katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), anasema mazoezi bila kuchoka, kumsikiliza mwalimu, nidhamu, kujituma ndani na nje ya uwanja ndio msingi wa yote.

“Mazoezi ya kukimbia ufukweni, vilimani na kwingineko yana maana sana ukifanya wewe mwenyewe na si kusubiri programu za kocha,” anasema na kuongeza kuwa nidhamu ni jambo lingine ambalo mchezaji ni lazima kuwa nalo ili kuweza kumudu kucheza kwa mafanikio vinginevyo ni kazi bure.

Kibadeni anasema kujituma huko na uthubutu ni vitu vilivyomfanya atue Majimaji kwa ajili ya kuichezea akiwa kocha mchezaji na huko ndipo alipopewa uchifu wa Kabila la Wangoni, heshima ya juu ambayo iliambatana na hafla ya kutawazwa rasmi kushika wadhifa huo.

Anasema alitua Majimaji akiiacha Simba ikiwa na ubingwa wa Bara na kwenda kwake katika klabu hiyo kulichangiwa na ushawishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wakati huo Lawrence Gama ambaye alitaka kuhakikisha mkoa wake unakuwa na timu katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu).

“Yule mkuu wa mkoa (Gama) alikuwa na mapenzi makubwa katika soka, licha ya mimi kuna wachezaji wengine aliowaita kutoka klabu tofauti ili kuipandisha timu hiyo daraja la kwanza,” anasema na kuwataja wachezaji hao kuwa ni kipa Hamisi Malumbo, Adam Sabu, Ephrahim Chawinga, Iddi Pazi, Peter Tino, Hussein Mwakuruzo, Mchunga Bakari na wengineo. Anabainisha kuwa wakati huo kutokana na mazingira yalivyokuwa na miundombinu duni ambayo yaliufanya uonekane upo mbali sana na Dar es Salaam lakini ulikuwa na neema ambayo ilichagizwa na Gama ambaye pia aliiwezesha Majimaji kufundishwa na kocha kutoka Bulgaria, Dimitary Samsarov. Mwanzoni mwa miaka ya 1980 alirudi Dar es Salaam akiiacha Majimaji ikiwa katika kilele cha mafanikio kupitia kocha huyo aliyekuwa na programu ya kutembelea mikoani kusaka vipaji.

Baada ya yeye kuondoka Samsarov alikuwa akisaidiana na Ray Gama ambao waliingiza damu changa kutokana na imani yake kwamba soka linatakiwa kuanzia chini.

Anawataja wachezaji aliowaacha wakati huo na wengine kwenda baadaye kuwa ni Stephen Names, John Bosco, Shaibu Kambanga, Peter Mhina, Ibrahim Mbuzi, Abdalah Wasswa, Iddi Chama, Allan Shomari, John Kabisama, Octavian Mrope, Willy Kiango na Celestine ‘Sikinde’ Mbunga ambao waliifanya timu hiyo kuwa gumzo nchini.

Kibadeni anafafanua kuwa uzoefu wake na ule alioiba kwa Samsarov vilimfanya awe na nafasi kubwa ya kuitumikia kikamilifu nafasi ya ukocha.

Ukocha na soka la vijana

Kibadeni ni muumini mkubwa wa soka la vijana, anasema alianza mafunzo ya ukocha akiwa Majimaji na kusoma ngazi mbalimbali nje na ndani ya nchi huku baadhi ya mafunzo hayo yakiendeshwa na wakufunzi kutoka nje kwa uratibu wa Fifa. Kwa Kibadeni msingi wa soka sehemu yoyote duniani ni uwekezaji kwa vijana na hicho ndicho kitu ambacho Simba inafanya wakati huu, kutoa kipaumbele kwa vijana.

Kocha huyo aliyewahi kuifundisha Fanja FC ya Falme za Kiarabu na timu za Taifa za vijana na ile ya wakubwa, anasema soka ni biashara kubwa ambayo ikifanywa vizuri itatoa ajira na kuongeza pato la Taifa.

Anataka wadhamini kuziangalia pia klabu nyingine ili kukuza ushindani badala ya Simba na Yanga pekee.

Mwandishi anapatikana katika 0767826468