Kimoto: Sasa Singida Black Stars imeiva
Muktasari:
- Mbali na ligi, Singida imekuwa na mwanzo mzuri katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, ambako ilivuka raundi ya kwanza kwa kishindo dhidi ya Al-Ghazala ya Sudan Kusini.
KOCHA wa Singida Black Stars, Papy Kimoto amesema ameridhishwa na namna kikosi chake kilivyoimarika baada ya kupata muda wa kutosha kuingiza falsafa yake mpya kwa wachezaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kimoto amesema muda walioupata kambini umemsaidia kuwafanyia maboresho mbalimbali wachezaji wake na kuhakikisha wanaelewa kile anachotaka kukiona ndani ya uwanja.
Amesema hatua hiyo imeonekana katika mechi mbili za kirafiki walizocheza dhidi ya Mbuni inayoshiriki Championship na Polisi Tanzania, ambapo Singida Black Stars ilishinda michezo yote.
“Tumepata muda mzuri wa kufanya kazi na kikosi, hasa katika kuingiza falsafa yangu. Nimeridhishwa na hatua ambayo wachezaji wamepiga katika kipindi hiki kwa sababu wamekuwa wakielewa kile tunachotaka,” amesema Kimoto.
Amesema ushindi katika mechi hizo za kirafiki umempa picha nzuri kuhusu utayari wa kikosi, huku akiamini kurejea kwa wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa kutakifanya kikosi kuwa imara zaidi.
“Tumefanya kazi kubwa na nimeona mabadiliko. Wachezaji waliokuwa kwenye timu za taifa nao wamerudi salama, hivyo naamini tutakuwa kwenye kiwango bora zaidi kwa sababu sasa tunakuwa na kikosi kamili,” amesema.
MALENGO
Kimoto amesema lengo lake ni kuhakikisha muda walioupata wa kufanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki unazaa matokeo mazuri pindi mashindano yatakaporejea.
“Tunataka yale tuliyofanya kambini yaonekane kwenye mashindano. Wachezaji wamepata muda wa kuelewa mfumo na falsafa, hivyo sasa ni kuhakikisha tunaiendeleza kazi hii na kuwa bora zaidi,” amesema Kimoto.
Singida imeanza msimu wa Ligi Kuu kwa kucheza mechi sita, ikishinda tatu, sare moja na kupoteza mbili. Timu hiyo ilianza kwa kuifunga Fountain Gate 3-0, ikatoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar, ikapoteza 2-1 dhidi ya Simba, kabla ya kuifunga Polisi Tanzania 4-2 na Namungo 3-2, kisha kupoteza 2-1 dhidi ya Mashujaa.
Katika michezo hiyo sita ya ligi, Singida imefunga mabao 13 na kuruhusu tisa, ikiwa na pointi 10 kabla ya kuendelea na ratiba ya ligi baada ya mapumziko.
Mbali na ligi, Singida imekuwa na mwanzo mzuri katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, ambako ilivuka raundi ya kwanza kwa kishindo dhidi ya Al-Ghazala ya Sudan Kusini.
Singida ilishinda 7-1 katika mchezo wa kwanza ugenini, kabla ya kushinda tena 3-0 kwenye mchezo wa pili, hivyo kwenda hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 10-1.