Kilio cha viwanja Pemba
Muktasari:
- Katika matumizi ya viwanja kwa ajili ya mazoezi, amesema klabu zitatozwa Sh500,000 kwa mwezi, huku akademi zikilipia Sh100,000 kwa mwezi.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mattar Zahor Massoud amesema bado kuna mwitikio mdogo kutoka kwa wananchi wa Pemba katika kutumia viwanja vya michezo vilivyojengwa na Serikali.
Amesema licha ya Serikali kuwekeza katika ujenzi wa viwanja mbalimbali kwa lengo la kukuza michezo na kuwapa vijana fursa za kufanya shughuli za michezo katika mazingira bora, matumizi ya viwanja hivyo kisiwani Pemba bado ni madogo ikilinganishwa na Unguja.
Mattar alitoa kauli hiyo Novemba 12, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa wizara hiyo, Migombani, mjini Unguja.
“Viwanja vya Pemba havina mwitikio mkubwa ikilinganishwa na Unguja, kwani maombi tunayopokea kutoka kwa watu wenye uhitaji wa kuvitumia ni machache zaidi,” amesema.
Alifafanua viwanja hivyo vimejengwa kwa lengo la kuongeza fursa kwa vijana kushiriki michezo katika mazingira bora yenye huduma muhimu.
Amesema katika kuhakikisha viwanja hivyo vinatumika ipasavyo, Serikali imeweka utaratibu wa matumizi pamoja na bei elekezi kwa viwanja 17 vilivyojengwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ili kuondoa mkanganyiko wa gharama za matumizi.
“Serikali iliamua kuviendesha viwanja hivyo kwa utaratibu wa ubia na wawekezaji ili kuhakikisha vinatunzwa na kuendelea kutoa huduma kulingana na malengo yaliyokusudiwa,” amesema. Amesema baadhi ya viwanja hivyo tayari vimeanza kutumika, lakini wizara imekuwa ikipokea malalamiko kuhusu gharama za matumizi, hali iliyoifanya kuandaa bei elekezi zitakazowasaidia wananchi kufahamu viwango vinavyotakiwa kulipwa.
Akizungumzia gharama za matumizi ya Uwanja wa Mao Zedong, ambao sasa uko chini ya usimamizi wa Baraza la Jiji Zanzibar, amesema mechi za kirafiki zitakazochezwa Jumatatu hadi Ijumaa, kuanzia asubuhi hadi jioni, zitatozwa Sh150,000, huku matumizi ya usiku yakigharimu Sh200,000 kwa kila mechi.
Amesema michezo ya taasisi itatozwa Sh1.2 milioni kwa matumizi ya mchana na Sh1.5 milioni kwa matumizi ya usiku. Kwa upande wa shughuli nyingine, matamasha yatakayofanyika kuanzia asubuhi hadi usiku yatatozwa Sh2.5 milioni, huku mahafali yakigharimu Sh5 milioni. Aidha, amesema mashindano yanayoandaliwa na wizara yatakuwa bure, wakati yale yanayoandaliwa na wadau wengine yatatozwa Sh100,000. Mashindano ya Ligi Kuu, Kanda na Mkoa yatachangia asilimia 20 ya makusanyo.
Katika matumizi ya viwanja kwa ajili ya mazoezi, amesema klabu zitatozwa Sh500,000 kwa mwezi, huku akademi zikilipia Sh100,000 kwa mwezi.