Nini kimeikumba Fufuni SC?
Muktasari:
- Msimu uliopita, Fufuni ilikuwa miongoni mwa timu zilizofanya vizuri na kumaliza nafasi ya sita, baada ya kushinda mechi 14, sare sita na kupoteza 10 katika michezo 30.
BAADA ya kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita, Fufuni SC imejikuta ikipitia mwanzo mgumu kabisa wa msimu wa 2026-2027, huku ikiwa bado haijapata ushindi hata mmoja baada ya kucheza mechi 10.
Msimu uliopita, Fufuni ilikuwa miongoni mwa timu zilizofanya vizuri na kumaliza nafasi ya sita, baada ya kushinda mechi 14, sare sita na kupoteza 10 katika michezo 30.
Katika kipindi hicho, Fufuni ilifunga mabao 43, ikaruhusu 30 na kukusanya jumla ya pointi 48, takwimu zilizowafanya mashabiki wake kutazamia makubwa zaidi msimu huu.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Baada ya mechi 10 za mwanzo za msimu huu ukiwa ni wa pili kushiriki Ligi Kuu Zanzibar, Fufuni imekusanya pointi mbili pekee na kujikuta mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.
Kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Kipanga katika mchezo wa 10 kimeongeza maumivu kwa Fufuni, ambayo sasa imecheza jumla ya dakika 900 bila kuonja ladha ya ushindi.
Katika mechi hizo 10, Fufuni imetoka sare mbili na kupoteza nane, huku ikitafuta kwa nguvu kubwa jibu la kurejea kwenye kiwango kilichoifanya kuwa moja ya timu bora msimu uliopita.
WALIVYOWASHA MOTO MSIMU ULIOPITA
Mwanzo wa Fufuni msimu wa 2025-2026 ulikuwa tofauti kabisa na hali inayoonekana sasa.
Katika mechi 10 za mwanzo, Fufuni ilikusanya pointi 18 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, baada ya kushinda mechi tano, kutoka sare tatu na kupoteza mbili.
Timu hiyo ilifunga mabao 12 na kuruhusu nane, ikionyesha uimara katika safu ya ushambuliaji pamoja na ulinzi.
Matokeo yao katika kipindi hicho yalikuwa: Fufuni 2-1 Kipanga, Fufuni 0-2 Malindi, Fufuni 1-3 Mafunzo, Fufuni 3-0 Zimamoto, Polisi 0-1 Fufuni, Fufuni 0-2 Mlandege, Fufuni 1-1 Junguni, Fufuni 1-0 Chipukizi, Fufuni 1-1 New King na Fufuni 1-0 KVZ.
Ni mwanzo uliowafanya wengi kuamini Fufuni ingeendelea kuwa tishio kubwa, lakini picha ya msimu huu imekuwa tofauti kabisa.
MECHI 10, USHINDI SIFURI
Hadi sasa, Fufuni imepoteza uwezo wa kuendeleza ubora wake na imejikuta ikihangaika kutafuta pointi.
Katika mechi zake 10 za msimu huu, matokeo yamekuwa hivi: Wembe 1-0 Fufuni, Polisi 2-1 Fufuni, KVZ 3-0 Fufuni, Uhamiaji 2-1 Fufuni, Muembe Makumbi 1-0 Fufuni, Raskazone 0-0 Fufuni, Fufuni 2-2 Black Sailors, Fufuni 0-1 Chipukizi, Fufuni 0-2 JKU na Kipanga 3-1 Fufuni.
Matokeo hayo yanaonyesha tofauti kubwa na mwanzo wa msimu uliopita, huku safu ya ulinzi na ushambuliaji zikionekana kupoteza makali yaliyowapa Fufuni matokeo mazuri.
Timu pinzani zimeonekana kupata nafasi kubwa ya kuisoma Fufuni kimbinu, huku kikosi hicho kikishindwa kubadilisha ubora wa uchezaji kuwa matokeo.
KOCHA AWEKA WAZI CHANZO
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Fufuni, Vuai Silima, amekiri wana mwenendo mbaya wa matokeo, lakini amesema bado ana imani wanaweza kubadilisha hali hiyo.
Kwa mujibu wa kocha huyo, mabadiliko makubwa ya kikosi yamechangia hali wanayopitia, akisema wengi wa wachezaji waliokuwepo msimu uliopita hawapo tena.
Amesema kati ya wachezaji waliopo sasa, ni mmoja pekee mwenye uzoefu mkubwa wa kucheza katika ligi hiyo.
Kocha huyo amesema awali klabu haikuwa na mdhamini, hali iliyosababisha kukosekana kwa uwezo wa kifedha wa kufanya usajili wa wachezaji wenye ushindani mkubwa.
“Timu yetu ipo kwenye kiwango kibaya sana na tuna mwenendo mbovu wa matokeo usioridhisha, lakini bado tuna matumaini kwamba tutakaa sawa,” amesema Silima.
Amesema kwa sasa timu imepata mdhamini na uongozi una matumaini ya kutumia dirisha dogo la usajili kufanya maboresho ya kikosi.
SULUHU NI NINI?
Silima amesema eneo la ushambuliaji ndilo linalohitaji kupewa kipaumbele zaidi katika maboresho wanayotarajia kuyafanya.
“Tunataka kufanya maboresho zaidi, hasa kwenye eneo la ushambuliaji kwa sababu tunaona ndipo penye changamoto kubwa,” amesema.
Mbali na mipango ya usajili, Fufuni sasa inaelekeza nguvu zake katika michezo mitano iliyobaki ya mzunguko wa kwanza.