Kigogo Mtibwa Sugar ataja mawili akisisitiza kurudi Ligi Kuu
Muktasari:
- Bayser amesema matarajio yake ni Mtibwa Sugar kurejea Ligi Kuu, akieleza kwamba anaamini utapatikana uongozi bora na kufanya usajili wa kuifanya timu kuwa imara.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser, amesema matarajio yake ni kuona timu hiyo inarejea Ligi Kuu Tanzania Bara huku akitaja mambo mawili.
Mtibwa Sugar ilishuka daraja msimu uliopita 2025-2026 ikidumu kwa msimu mmoja tu baada ya kupanda, matokeo ambayo yameamsha maumivu kwa uongozi na mashabiki wake kutokana na kukosa uhondo wa Ligi Kuu msimu ujao.
Hata hivyo, hivi karibuni uongozi wa timu hiyo uliweka wazi nia ya kumsaka Mtendaji Mkuu atakayeiongoza Mtibwa Sugar huku ukimtaja Bayser kuhitaji huduma yake ukielezea mafanikio yake kikosini.
Katika utawala wa Bayser, aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu miaka miwili mfululizo akifanya hivyo 1999 na 2000, huku akiipa tena taji la Kombe la Shirikisho (kwa sasa CRDB) msimu wa 2020-2021.
Akizungumza na Mwanaspoti leo Agosti 2, 2026, Bayser amesema timu hiyo itarudi kwa ubora wake na kufanya vizuri katika Ligi ya Championship msimu ujao wa 2026-2027 na kurejea Ligi Kuu akiwatoa hofu wadau na mashabiki.
Amesema matarajio yake ni kuona timu hiyo inapata uongozi imara na kufanya usajili bora ambao utaisaidia msimu ujao kufikia malengo yake akieleza kuwa mashabiki wasiikatie tamaa.
"Naamini timu itarudi vizuri na kupanda tena Ligi Kuu, mambo ni mawili tu, uongozi imara na usajili bora ndio vitaiwezesha kufikia malengo na uwezekano upo, mashabiki wasiikatie tamaa," amesema Bayser.
Kuhusu msimamo wake wa kurejea katika nafasi ya Mtendaji Mkuu, kigogo huyo amesema atabaki kuwa sehemu ya uongozi wa kawaida na atakuwa tayari kusaidia pale watakapohitaji msaada wake wa kushauri.
"Siyo kwamba sipo, nipo na nitatoa ushauri wangu pale nitakapohitajika, nitakuwa karibu na uongozi na ninaamini atapatikana kiongozi aliye bora kuliko mimi," amesema bosi huyo.