Kesi ya Kazimoto yapigwa kalenda
Mchezaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto
Muktasari:
Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga, Rahim Mushi anayesikiliza kesi hiyo, alisema amepokea barua na kwamba itaendelea tena Mei 2.
KESI ya kumshambulia Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Mwanahiba Richard, inayomkabili mchezaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto imepigwa kalenda hadi Mei 2.
Mshtakiwa huyo aliandika barua ya kuomba udhuru kupitia wakili wake kwa madai ya kuteuliwa timu ya taifa, Taifa Stars iliyopo Chad.
Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga, Rahim Mushi anayesikiliza kesi hiyo, alisema amepokea barua na kwamba itaendelea tena Mei 2.
“Kesi hii itaendelea Mei 2, kama upande wa mshitakiwa kutakuwa na udhuru kwa tarehe iliyopangwa taarifa itolewe mapema kabla ya wiki moja,” alisema Hakimu Mushi.
Awali Wakili wa Serikali, Upendo Shemkole alitoa angalizo kuwa upande wa mlalamikaji anatoka mbali na anatumia gharama kubwa kwenye usafiri hivyo anaiomba mahakama kuliangalia hilo kutokana na kesi kuahirishwa.
Kazimoto anakabiliwa na kesi ya Kudhuru Mwili dhidi ya Mwanahiba kitendo alichofanya kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Februari 10 mwaka huu mara baada ya kumaliza kufanya mazoezi.