Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kazi moja Simba

Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi

MWANDISHI WETU KOCHA wa Simba, Patrick Lieweg amesema kikosi chake kina kazi moja tu kesho Jumapili mbele ya Recreativo Libolo ya Angola. Liewig aliitaja kazi hiyo kuwa ni kushambulia kwa nguvu ili kupata mabao mengi na kutotoa upenyo wowote kwa washambuliaji wao kupata bao. Simba inatupa karata yake ya kwanza kesho Jumapili kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya mabingwa hao wa Angola huku Azam ikicheza leo Jumamosi dhidi ya Al Nasri ya Sudan Kusini katika mechi ya Kombe la Shirikisho. Libolo ambao wamepiga kambi kwa wiki moja sasa kwenye Hoteli ya Double Tree, Masaki jijini Dar es Salaam wamekuja na fungu kubwa kwani wamekuwa wakiishi maisha ya kifahari ingawa wanajilinda kila dakika kwa hofu ya kuhujumiwa na Simba kwani wamegoma hata kuzungumza na waandishi mazoezini. Simba ambayo imemwita kocha Talib Hilal ili kuwaongezea nguvu Lieweg na msaidizi wake Jamhuri Kihwelu' Julio' inahitaji ushindi kwa zaidi ya mabao mengi ili kujiweka salama kwa mechi ya ugenini jijini Luanda ambako kwa mujibu wa wazoefu timu zinazokwenda huko hukumbana na mizengwe na michezo mingi ya kisaikolojia yenye lengo la kumkatisha tamaa mgeni. Akiizungumzia mechi hiyo, Lieweg ambaye jana Ijumaa timu yake ilikutana na wanachama wa Friends of Simba kwenye Hoteli ya Saphire kupanga mikakati ya mwisho alisisitiza kwamba lazima kieleweke na atatumia uzoefu wake wa miaka zaidi ya kumi Afrika kuipa Simba ushindi. "Hii ni mechi muhimu kwa Simba kama timu, mashabiki na wachezaji wenyewe. Tunahitaji kufanya kazi sana kila mmoja kwa akili na nguvu zake kuhakikisha tunashinda, hizi ndio mechi za kuonyesha thamani na heshima ya Simba na Tanzania kwa Waafrika na duniani. Tunahitaji kupambana,"alisema Lieweg. "Nina ufahamu kuhusiana na wapinzani wetu ni timu iliyojijenga sana na inayocheza soka la kushambulia na wana watu wazoefu, tunachohitaji kufanya sisi ni kutulia kuanzia wachezaji wenyewe, viongozi mpaka mashabiki, tuwe kitu kimoja tuwe na mtazamo wa ushindi. Tunahitaji kushambulia kwa nguvu kuwapa presha ili tuwafunge mabao mengi na pia tuzibe ukuta wetu wasipate nafasi ya kufunga. "Tukiwapa nafasi itakuwa mbaya sana kwetu kwa kuwa tunakwenda kumalizia ugenini, nimekaa kwenye benchi na klabu tofauti za Afrika mechi hazipungui 52 kwenye haya mashindano ya Afrika najua mambo ya nyumbani na ugenini yanavyokuwa, tunahitaji ushindi tu. "Najua mashabiki hawana raha kutokana na matokeo ya hizi mechi mbili zilizopita za ligi ya ndani, lakini nimekaa na wachezaji nimewaambia mambo ya msingi wamenielewa, naomba mashabiki watupe sapoti. "Hii ni mechi muhimu kwa heshima ya Simba, mashabiki wasitukane au kuzomea wachezaji hata wanapokosea wawape sapoti wafanye vizuri kwa vile wakiwazomea watatoa faida kwa wageni na itakuwa hasara kwetu. Tumejiandaa vizuri, watupe sapoti tunaahidi hatutawaangusha," alisisitiza Liewig ambaye amekaa na Simba kwa mwezi mmoja tu. Lilobo wapo Dar es Salaam huku wakijua kuwa Simba ndio timu pekee ya Tanzania iliyowahi kufika fainali ya Kombe la CAF na walitolewa na timu ya Stella ya Ivory Coast kwa kufungwa mabao 2-0 nyumbani licha ya suluhu mjini Abidjan mwaka 1993. Waangola wamefunua kurasa za vitabu wakagundua kuwa Simba ndio timu ambayo iliwatoa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek ya Misri na kutinga hatua ya makundi mwaka 2003. Kwa upande wa Azam itakayocheza leo Jumamosi kocha wake, Stewart Hall amesisitiza kuwa wako vizuri kisaikolojia ingawa anatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa Nasri ambao alisema ni timu yenye vijana chipukizi ingawa hawavumi sana. Kabla ya mechi ya Azam kutakuwa na burudani za wasanii mbalimbali wa muziki wakiongozwa na Juma Nature. Hii ni mara ya kwanza kwa Azam kushiriki michuano hiyo mikubwa ambayo Tanzania imekuwa ikifanya vibaya kupitia klabu za Simba na Yanga kwenye miaka ya hivi karibuni.