Kaseja ajiandaa kisaikolojia Kagera
Muktasari:
- Kaseja ametoa kauli hiyo wakati Kagera Sugar ikihaha kusaka ushindi wake wa kwanza katika Ligi Kuu, ikiwa imecheza mechi tano sawa na dakika 450 bila kuibuka na pointi tatu, hali inayoongeza presha kwenye benchi la ufundi.
KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amesema amejipanga kisaikolojia kwa lolote litakalotokea kwenye kibarua chake, ikiwamo kuondolewa kutokana na matokeo yasiyoridhisha, akisema mwenendo wa ligi umeanza kushuhudia baadhi ya makocha wakiondoka kwenye timu zao.
Kaseja ametoa kauli hiyo wakati Kagera Sugar ikihaha kusaka ushindi wake wa kwanza katika Ligi Kuu, ikiwa imecheza mechi tano sawa na dakika 450 bila kuibuka na pointi tatu, hali inayoongeza presha kwenye benchi la ufundi.
Kocha huyo mwenye historia ya mafanikio katika soka la Tanzania kipindi anacheza, alisisitiza kuwa matokeo ndiyo yanayoamua hatma ya makocha, hivyo naye hawezi kujihakikishia kuendelea kuwepo kwenye benchi hilo endapo hali itaendelea kuwa mbaya.
Amesema katika soka kila jambo linawezekana, akitolea mfano wa timu ambazo tayari zimeanza kuachana na makocha wao baada ya kushindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.
“Kila timu inatamani kupata matokeo mazuri, hali ikiwa tofauti ndio mtu anafikia hatua ya kuondoka kupisha wengine. Mpira ndio kazi yetu, hivyo ukishinda ndio furaha hata kwa waajiri, kuondoka ni kawaida,” amesema Kaseja.
Hadi sasa, TRA United ndiyo timu iliyofikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa kocha wake, Ettiene Ndayiragije, baada ya kuiongoza katika mechi tano na kuvuna pointi tatu na tayari wamemtambulisha Hemed Morocco.
Kaseja, ambaye anakumbukwa kwa kuirejesha Kagera Sugar ligi kuu baada ya kuishusha 2024-2025, licha ya kuanza vibaya msimu huu, amesema anafahamu ukubwa wa presha inayotokana na matokeo, lakini hilo halimfanyi kukata tamaa.
“Kuondoka, kurudi au kwenda sehemu nyingine ni maisha ya mpira, wala haipunguzi heshima kwa kocha. Huenda bahati ikakosekana kwa wakati huo, unapoenda kwingine ukafanya vizuri,” amesema Kaseja.
Licha ya hali hiyo, Kaseja amesema anaamini kikosi chake kina uwezo wa kubadilisha mwenendo huo pindi kitakapopata ushindi wa kwanza, akisema kiu ya wachezaji ni kubwa na hakuna timu itakayokuwa rahisi kuizuia.